23.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Waziri azinyooshea kidole kampuni tatu mgomo malori

Na Mwandishi Wetu
-Dar es Salaam

WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe, ametishia kuzinyima leseni kampuni tatu zilizoomba leseni kwa ajili ya kuendesha bandari kavu (ICDS) kwa tuhuma za kuhamasisha mgomo wa malori bandarini.

Wamiliki wa kampuni hizo wanatuhumiwa kuhamasisha madereva wa malori yanayotoa mizigo bandarini kufanya mgomo kuanzia jana mchana hadi usiku kwa lengo la kuondolewa kwa mizani ya kupima uzito wa magari hayo kabla ya kuanza safari zake kwa njia ya barabara.

Kamwelwe ameyaeleza hayo leo, alipofanya ziara ya kukagua mizani hizo kuona kama inasababisha foleni kama ilivyodaiwa na baadhi ya wafanyabiashara hao na kubaini kuwa lori moja linachukua sekunde 55 hadi dakika moja kupimwa uzito.

“Nimekuja nione kama kweli hii mizani inasababisha foleni, lakini nimekuta si kweli kwa sababu kuna mizani miwili na yote ni mizima na wanatumia si chini ya dakika moja kupima na kuondoka eneo hili.

“Sasa nimeshabaini waliohusika kufanya mgomo huu ni kampuni tatu ikiwamo PrimeFuel ambao tunawaita ni ‘Wahaini’ kwa sababu lengo lao ni kukwamisha miradi ya Serikali na waliomba leseni za ICDS sasa tutawaonyesha kama sisi ni Serikali na walichofanya si sahihi” amesema Kamwelwe.

Ameeza zaidi kuwa, leseni ya wafanyabiashara wa ICDS zinatoka Julai 17 na wafanyabishara waliohusika kufanya hujuma hizo hawatapatiwa leseni zao kwa sababu wanakwamisha juhudi za Rais John Magufuli.

Pamoja na mambo mengine, Kamwelwe amesema licha ya ya shinikizo la wafanyabiashara hao kutaka mizani hiyo iondolewe amesisitiza haitaondolewa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles