23.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

WAZIRI AWAONYA WANAOKATAA VYETI VYA KUZALIWA VYA MKONO

Na FLORENCE SANAWA-MTWARA


WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, ameagiza watumishi wa Serikali wanaokataa vyeti vya kuzaliwa vilivyoandikwa kwa mkono waanze kuvitambua.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa usajili wa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano, Dk. Mwakyembe alisema kitendo cha watumishi hao kukataa vyeti hivyo, wanakiuka sheria kwa kuwa Serikali inavitambua.

“Mimi nashangaa kwa sababu kuna baadhi ya taasisi za Serikali zimekuwa zikikataa vyeti hivyo na kudai kuwa vimefojiwa, wakati si kweli.

“Vyeti hivyo ni halali kwa sababu vina alama muhimu ambayo mtu yeyote hawezi kuifoji,” alisema Dk. Mwakyembe.

Katika hatua nyingine, Dk. Mwakyembe aliyekuwa akimwakilisha Waziri wa Katiba na Sheria, Profesas Palamagamba Kabudi, alisema hadi sasa Tanzania ipo nyuma katika usajili wa watoto ikilinganishwa na nchi nyingine duniani.

“Ukijua idadi ya watu waliokwishafariki na walioko hai, inakurahisishia kujua kwa usahihi mahitaji na upungufu katika sekta mbalimbali ikiwamo afya, elimu na kwingineko.

“Ukishayajua hayo, inakuwa rahisi kupanga mipango yako ya maendeleo kwa sababu utakuwa umeshajua mahitaji katika maeneo mbalimbali,” alisema Dk. Mwakyembe.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini ( RITA), Profesa Hamis Dihenga, alisema bado uandikishaji wa vyeti vya kuzaliwa unahitaji hamasa zaidi ili kupunguza idadi ya wasiokuwa navyo.

“Kwa mujibu wa sensa yetu iliyopita, bado Tanzania Bara ina asilimia ndogo ya watu waliojiandikisha kuchukua vyeti vya kuzaliwa ambao ni asilimia 13.4.

“Lakini pia, asilimia 80 ya Watanzania hawana utambuzi wowote wa kisheria juu ya umuhimu wa kuwa na vyeti vya kuzaliwa,” alisema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Simu ya Mkononi ya TIGO, Simon Karikari, alisema katika usajili huo kwa mikoa ya Lindi na Mtwara, kampuni hiyo imetoa simu 1000 zitakazowawezesha watoaji wa huduma hiyo kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles