Waziri apiga marufuku wahitimu darasa la saba kufanya kazi za ndani

0
487

Na Mwandishi wetu-Manyara

NAIBU waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William ole Nasha, amewataka viongozi  kuanzia ngazi ya vijiji mpaka mkoa, kuhakikisha wanafunzi wanaomaliza darasa la saba hawaondoki kwenye maeneo yao  kwenda kufanya kazi za ndani wakati wakisubiri matokeo ya mtihani ya darasa la saba.

Alisema kufanya hivyo kunawaondolea fursa ya kuendelea na masomo  wanapofaulu.

Ole Nasha alitoa agizo hilo mkoani Manyara  alipozungumza na viongozi hao kuhusu hali ya elimu mkoani humo.

Aliwataka kusimamia kwa karibu suala hilo ili kutokatisha ndoto za watoto hao na wale wanaofanya hivyo hatua za sheria zitachukuliwa dhidi yao.

“Hakikisheni watoto hawa wanaposubiri matokeo, wasisafirishwe kwa sababu wanapofika huko wanarubuniwa na waajiri hata matokeo yakitoka na kuonyesha wamefaulu hawarejei kuendelea na masomo,” alisema ole Nasha.

Alisema fursa za elimu nchini ni kubwa kwa sasa kwa kuwa elimu katika shule za msingi na kidato cha kwanza mpaka cha nne ni bure hivyo hakuna kisingizio tena kuwa mtoto hawezi kusoma kwa kuwa mzazi hana fedha.

“Wazazi msiwe sehemu ya kuchangia watoto wenu kwenda mjini kwa kuwa tu wanawatumia fedha kwa ajili ya matuzi.

“Hakikisheni mnawasimamia watoto hao katika kipindi chote wanachosubiri matokeo na kuwapeleka shule  matokeo yanapotoka na kuonekana wamefaulu,”alisema ole Nasha.

Aliwataka viongozi hao kutumia sheria kuhakikisha watoto wenye umri wa kuandikishwa wanaandikishwa  ili kutokuwa na wimbi kubwa la watoto wa mitaani wasioenda shule.

Ole Nasha pia alitembelea  Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Manyara na kuwataka kupitia mitaala yao  iendane na wakati, ikidhi mahitaji ya soko lakini pia wanafunzi weweze kusoma vitu vingi kwa wakati mmoja na viwe ni vile vinavyoendana  na soko la ajira.

Awali, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, Arnold Msuya, alisema mkoa huo una mwamko mdogo wa elimu hasa   wafugaji,  hali inayosababisha kutowaandikisha shule watoto wao wenye umri wa kuanza shule.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here