24.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Waziri amsimamisha kazi meneja Tanesco Meatu

NA DERICK MILTON- MEATU.

WAZIRI wa Nishati Dk. Medard Kalemani, amemsimamisha kazi Meneja wa Shirika la Umeme (TANESCO) Wilaya ya Meatu mkoani Simiyu, Amos Mtae kwa kushindwa kumsimamia Mkandarasi Kampuni ya White City anayetekeleza mradi wa Kusambaza Umeme Vijijiji (REA) awamu ya tatu katika wilaya hiyo.

Kalemani alisema meneja huyo ameshindwa kumsimamia mkandarasi huyo na kusababisha atekeleze mradi huo kwa kasi ndogo ikiwa ni miezi mitatu tangu atakiwe kuanza kazi.

Alichukua uamuzi huo mbele ya wananchi wa Kijiji cha Mwamishali, wakati wa hafla ya kuwasha umeme kwa baadhi ya taasisi za Serikali na nyumba za wananchi zilizowekewa umeme kupitia mradi huo.

Kabla ya kuchukua uamuzi huo, alimtaka meneja huyo kumweleza ni kwa nini mkandarasi huyo hana karakana, wala mafundi wanaondelea na kazi.

“Meneja wa Wilaya nataka maelezo tangu  nimefika hapa sijaona karakana ya mkandarasi wala sioni mafundi hapa wanaoendelea na kazi.

“Ni kwa nini vitu hivyo havipo wakati huu ni muda wa kazi na wanatakiwa kuwa wanaendelea na kazi?” alihoji Kalemani.

Meneja huyo alimweleza waziri   kuwa mkandarasi bado hajaweka karakana kwenye wilaya hiyo na kuhusu   mafundi, alisema kwa mujibu wa mkandarasi, ratiba ya kazi ilikuwa katika maeneo mengine ya vijijini wilayani humo, hivyo mafundi wako vijijini.

Hata hivyo Dk. Kalemani hakuridhishwa na majibu ya meneja huyo na kuamuru aondolewe kwenye nafasi hiyo huku akimtaka Kaimu Mkurugenzi wa Tanesco,  Raymond Seya, kumtafutia kazi nyingine.

“Haujui mafundi wako wapi? Hakuna karakana sasa unakagua nini? Unasimamia nini?

“Kuanzia leo huyu meneja aondolewe na apangiwe kazi kama mtaona anafaa, lakini kazi hii imemshinda.  Serikali hii haifanyi kazi kwa mazoea tunataka watu wanaofanya kazi kwa kasi zaidi,” alisema Dk. Kalemani.

Alisema katika kutekeleza  mradi huo kwenye awamu ya tatu, Serikali haina mzaha kwa mtu yeyote atakayerudisha nyuma juhudi za   kuhakikisha watanzania wote wanapata huduma ya umeme.

“Kwa mkoa wa Simiyu tumetoa zaidi ya Sh bilioni 29 kutekeleza mradi huu na fedha zote tayari zimetolewa na serikali, lakini mpaka sasa mkandarasi hajatekeleza mradi huu ipasavyo.

“Kwa atakayetaka kuturudisha nyuma tutamrudisha yeye kwanza, kutuchelewesha, tutahakikisha tunamchelewesha yeye kwanza,” alisisitiza Waziri Dk. Kalemani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles