26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Waziri afichua mchezo mchafu zabuni ujenzi

ASHA BANI – DAR ES SALAAM

WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe, amewaumbua wanasiasa na baadhi ya watu wanaowaombea zabuni mbalimbali za ujenzi wa miundombinu wakandarasi ili waweze kugawana fedha.

Amesema wanaofanya michezo hiyo wapo viongozi wa juu serikalini ambao hakuwataja majina wala vyeo vyao na kuwataka waache mchezo huo na kama wakiendelea ipo siku atawaumbua.

Kauli hiyo aliitoa jana wakati wa kutiliana saini mkataba wa ujenzi wa daraja la Kigongo-Busisi lenye urefu wa mita 3,200 (Kilometa 3.2) ambalo linajengwa Ziwa Victoria pamoja na barabara yake ya lami yenye urefu wa kilomita 1.66.

Daraja hilo ambalo zitatumika dakika nne hadi sita kuvuka katika Ziwa Victoria litagharimu Sh bilioni 592.6.

Kamwelwe alisema mara baada ya kutangazwa kwa zabuni hiyo, yalitokea mambo ya ajabu huku baadhi ya watu wengine wakiwamo viongozi walianza kujipanga kwa lengo la kusaidia kutafuta wakandarasi ili waweze kugawana fedha jambo ambalo ni kinyume cha sheria za nchi.

Alisema kuwa watu hao wengine wana nyadhifa kubwa serikalini ikiwamo kama wa kwake pamoja na wanasiasa ambao wamekuwa wakimsumbua Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Patrick Mfugale.

“Kuna watu wanaopitapita kwenye maofisi na wengine wana nyadhifa kubwa kubwa kama mimi, pia kuna wanasiasa ambao wamekuwa wakifanya tabia hiyo kwa kumsumbua hata Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Injinia Patrick Mfugale, waache mara moja.

 â€œMsimuone hivyo, Mfugale ni wa kupongezwa sana, anapata tabu, zabuni zikitangazwa kuna watu wengine wenye nyadhifa kama mimi, wengine wanasiasa wanakuwa wakijipitisha kwa ajili ya kutaka kuwapigania baadhi ya wakandarasi ili kuweza kupata tenda hiyo na baadaye kugawana.

“Bahati mbaya au nzuri zaidi hawapiti kwangu, na kama wamejua, wanasumbua watu wengine, mimi wangekuwa wanapita kwangu hata kama ni mwanangu ningemfukuza na hata angehama nyumbani kwangu.

“Tabia hii si nzuri kwa kuwa tunataka kuwa na ujenzi unaozingatia viwango vya hali ya juu,’’ alisema Kamwelwe.

Alisema pamoja na hali hiyo, lakini bado Serikali ilisimama imara na kufanikiwa kupata wakandarasi wawili ambao ni China Engineering ambao ni wataalamu wa ardhini, ikiwamo kufanya kazi ndani ya maji ya bahari na maji baridi na CCC akiwa na ujuzi wa kujenga barabara za juu ambao Serikali imezingatia ubora wa kazi zao.

“Nasema hivi kama angetokea mtu yeyote kuja ofisini kwangu, ningemtolea maneno ambayo asingeyasahau maishani mwake au hata angekuwa mtoto wangu ni siku hiyo hiyo ndiyo ilikuwa siku ya kumfukuza nyumbani kwangu,’’ alisema.

Alisema kuna watu wengine anawaheshimu, lakini ameona katika suala hilo wanataka kumwingilia, hivyo akawataka kutambua kuwa kazi hiyo si ya wanasiasa na kwamba wanatakiwa kuiacha Serikali ifanye kazi yake.

Aliongeza kuwa Mfugale amekuwa akipambana na wakati mgumu kwa wengine kumpigia simu au hata kuandika barua mbalimbali za kumshtaki katika taasisi za Serikali jambo ambalo si sahihi kwa misingi ya ufanyaji wa kazi.

Kamwelwe pia alielezea faida itakayopatikana mara baada ya miezi 48 kukamilika kwa ujenzi huo kuwa ni pamoja na kurahisisha usafiri kutoka maeneo mbalimbali ya Kanda ya Ziwa, mfano kutoka Kagera hadi Geita.

Pia kurahisisha huduma mbalimbali za kijamii huku akitolea mfano, wagonjwa wanaokwenda katika Hospitali ya Bugando, na kuweza pia kuokoa maisha yao.

“Hii halina ubishi, kuna watu wanatoka katika maeneo mbalimbali wagonjwa walikuwa wanatumia saa 2:45 kuvuka, lakini sasa watatumia dakika 4 mpaka 6, hivyo itasaidia kwa wagonjwa kufika kwa haraka na hata kuokoa maisha yao pia.

“Niliwahi kukutana na baadhi ya viongozi wakiwa wanatoka Burundi na Uganda, nilipowauliza wakanambia kuwa wanakwenda Bugando kwa ajili ya matibabu, hivyo kwa ujenzi huu si tu kwamba kutasaidia Tanzania pekee, bali hata na mataifa ya nje pia,’’ alisema Kamwelwe.

Aliongeza faida nyingine ni pamoja na kurahisisha biashara ndani na nje ya mikoa hiyo ya Kanda ya Ziwa ikiwemo kuvusha mazao ya biashara na chakula kwa kutumia daraja hilo.

MFUGALE

Naye Mtendaji Mkuu Tanroads, Mfugale, alisema ujenzi huo utakuwa ni wa miezi 48 na utakuwa chini ya usimamizi wa Serikali kupitia Tanroads.

Alisema kukamilika kwa daraja hilo kutawezesha kupitisha magari 10,000 kwa siku na kama kutakuwa na mahitaji yatakayoongezeka, basi wataongeza vivuko vingine.

Mfugale alisema daraja hilo limepunguza urefu wa barabara kwenda Geita, Bukoba, Uganda sambamba na muda wa safari kutoka Mwanza baada ya kutumia saa 2:30 sasa watatumia dakika nne hadi sita.

Alisema ubora wa daraja hilo ni miaka 120 na kutakuwa na kupishana kwa magari na hata pikipiki kwa kuwa kutakuwa na njia ya kwenda na kurudi kwa wakati mmoja.

JAFO NA JPM

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tamisemi, Selemani Jaffo, alimpongeza Rais Dk. John Magufuli huku akisema kwa kitendo hicho na miradi mingine inayotekelezwa ni sawa na kumaliza ‘swaga’ zote.

KITWANGA

Mbunge wa Misungwi, Charles Kitwanga (CCM), alisema daraja hilo litatoa fursa ya kuwekeza na kujenga pia kituo cha uwekezaji kitakachosaidia kukua kwa uchumi na ajira maeneo hayo.

Alimpongeza pia Rais Magufuli kwa utekelezaji wake wa Ilani ya CCM, huku akieleza ubora wa daraja hilo ambalo ni kubwa lisilo na mfano Afrika Mashariki na Kati.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles