27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

WAVUVI ILEMELA WASAIDIWA ZANA HALALI ZA UVUVI

Na ANNA RUHASHA-MWANZA

VIJANA zaidi ya 12 wanaojishughulisha na uvuvi kwenye kambi ya Fuata Nyao iliyopo Mtaa wa Mihama Kata ya Kitangiri, Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza, wamesaidiwa zana halali za kuvulia samaki ili kujikwamua na umasikini.

Zana hizo zenye thamani ya Sh milioni 88.3, zilitolewa na mjasiriamali, Vedastus Msizu, juzi wilayani hapo wakati wa ufunguzi wa kambi hiyo ili kuwaongezea ajira vijana hao ambapo sherehe za makabidhiano hayo zilihudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela.

Mmoja wa wavuvi hao, Swahibu  Shebi, akisoma risala mbele ya Mkuu wa Mkoa, alisema zana hizo zitawasaidia kuachana na uvuvi haramu unaotumia zana duni na kuhatarisha maisha ya viumbe hai majini, wavuvi hao walipokea mitumbwi 14, nyavu 70 na injini moja zenye thamani ya Sh milioni 88.3 ambapo zaidi ya vijana  45 watanufaika na mpango huo ikiwemo ajira.

“Vedastus Msizu ambaye ni Mkurugenzi wa kambi hii, ameamua kufadhili zana halali za kuvulia samaki tofauti na awali tulikuwa tukishiriki katika uvuvi haramu kwa hiyo kupitia zana hizi tutaachana kabisa na uvuvi huo, ufadhili huu ni wa makubaliano maalumu ambapo tutakuwa tunarejesha kidogo kidogo kupitia hii mitaji aliyotufadhili na zana haramu tulizikabidhi kwenye uongozi pia tumetoa ushirikiano kwa Serikali kuhakikisha tunatokomeza uvuvi haramu,” alisema Swahibu.

Swahibu aliongeza kwamba kupitia ufadhili huo watazalisha ajira zisizo rasmi kwa vijana 100 ambao watajihusisha na kusafisha mitumbwi, kubeba samaki na kushona nyavu hivyo watakuwa wamesaidia kupunguza tatizo la udokozi katika mwalo huo, huku akiiomba Serikali kuwaboreshea  miundombinu ya barabara, vyoo, sehemu ya kuuzia samaki na kufanya doria nyakati za usiku ili kupambana na majangili, kupeleka dawa za kichocho, kudhibiti magonjwa ya maambukizi kwa wananchi wanaoishi kandokando ya Ziwa Victoria ambao wamekuwa waathirika wakubwa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella, alimpongeza mjasiriamali huyo kwa uzalendo wake na kuwataka wafanyabiashara wengine kuiga kwake kwa kuwekeza kwa vijana ambao hawana uwezo pale wanapohitaji msaada wa mitaji ya biashara.

Mongella aliwaagiza viongozi wanaohusika wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela akiwemo Mkurugenzi wake, John Wanga, kuhakikisha kikundi hicho kinasajiliwa na kupewa mikopo inayotolewa na Serikali ili waongeze mtaji na kurudisha mkopo kwa mfadhili bila shida yoyote.

“Haiwezekani mnakamua tu lazima maendeleo hapa yaonekane, Mkurugenzi upo hapa nikuombe ikifika Desemba mosi, mwaka huu nikirudi hapa nikute mabadiliko ya miundombinu ya vyoo, uzio, sehemu ya kupaki magari na jengo la kuuzia samaki pawe pameboreshwa, ofisa uvuvi amesema huu mwalo ni wa tatu kwa kuheshimika kutoa samaki wenye viwango na kuchangia pato la mkoa kwa asilimia kubwa kwa hiyo ni lazima paonekane,” alisema Mongella.

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles