24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

WAVULANA WANG’ARA MATOKEO DARASA LA SABA

AZIZA MASOUD NA OSCAR ASSENGA-TANGA/DAR ES SALAAM

BARAZA la Taifa la Mitihani (NECTA) limetangaza matokeo ya mitihani ya darasa la saba na kuonyesha ufaulu umepanda kwa asilimia 2.40, ukilinganishwa na mwaka jana, huku wavulana wakiongoza kwa kupata alama za juu zaidi.

Akitangaza matokeo hayo ofisini kwake Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Necta, Dk. Charles Msonde, alisema watahiniwa 662,035 kati ya 909,950 waliofanya mitihani hiyo iliyofanyika mwanzoni mwa Septemba, mwaka huu, wamefaulu kwa kupata alama 100 au zaidi kati ya alama 250, huku idadi ya waliofaulu ni sawa na asilimia 72.76, ikilinganishwa na mwaka jana iliyokuwa asilimia 70.36 na kati yao wasichana ni 341,020, ambao ni sawa na asilimia 70.93 na wavulana ni 321,015, sawa na asilimia 74.80.

“Kati ya watahiniwa 916,885 waliosajili, wasichana walikuwa 484,218, sawa na asilimia 52.81 na wavulana 432,667, sawa na asilimia 47.19. Watahiniwa 909,950 ambao ni sawa na asilimia 99.24 ya waliosajiliwa walifanya mtihani, kati ya hao wasichana walikuwa 480,784, sawa na asilimia 99.29 na wavulana walikuwa 429,166, sawa na asilimia 99. Kati ya watahiniwa 909,950 waliosajiliwa, 1,137 walikuwa na uono hafifu na watahiniwa 94 walikuwa wasioona,” alisema.

Dk. Msonde alisema watahiniwa 6,935, sawa na asilimia 0.76, hawakufanya mitihani kutokana na sababu mbalimbali, zikiwamo utoro na ugonjwa na kati ya hao, wasichana ni 3,434 na wavulana ni 3,501.

Aliwataja watahiniwa 10 (aliyeshika namba moja hadi 10) bora kitaifa na shule walizotoka zikiwa katika mabano kuwa ni Hadija Ally (Sir John), Naseem Said (Sir John), Ibrahim Shabani (Tusiime), Kadidi Kadidi (Paradise), Acius Missingo (St. Peter Claver), Insiyah Kalimuddin            (Sir John), Colletha Masungwa (St. Achileus), Mahir Mohamedy (Feza), Mbarak Faraj (Feza) na Philimon Daman (St. Achileus).

Pia alizitaja shule zilizoongoza kitaifa na mikoa zilipotoka ikiwa katika mabano kuwa ni St. Peter (Kagera) iliyokuwa na watahiniwa 46 na imeshika nafasi ya kwanza, nafasi ya pili imeshikwa na St. Severine (Kagera) iliyokuwa na wahitimu 66, Alliance (Mwanza) iliyokuwa na wahitimu 42 imeshika nafasi ya tatu, wakati nafasi ya nne ikichukuliwa na Sir John (Tanga) iliyokuwa na wahitimu 41.

Alizitaja shule nyingine kuwa ni Palikas (Shinyanga) iliyokuwa na wahitimu 53 imeshika nafasi ya tano, nafasi ya sita imeshikwa na Mwanga (Kagera) iliyokuwa na wanafunzi 43, Hazina (Dar es Salaam) imeshika nafasi ya saba ikiwa na wahitimu 41, nafasi ya nane imeshikwa na St. Anne Marie (Dar es Salaam) ikiwa na wanafunzi 43, nafasi ya tisa imeshikwa na Rwekiza (Kagera) iliyokuwa na wahitimu 114 na nafasi ya 10 imeshikwa na Martin Luther (Dodoma) iliyokuwa na wahitimu 42.

Pia alizitaja shule 10 zilizoshika nafasi za mwisho na mikoa zinapotoka ikiwa katika mabano kuwa ya kwanza ni Nyahaa (Singida) iliyokuwa na wanafunzi 69, ya pili ni Bosha (Tanga) iliyokuwa na watahiniwa 88, ya tatu ni Ntalasha (Tabora) iliyokuwa na wahitimu  69, ya nne ni Kishangazi (Tanga) iliyokuwa na wahitimu 54, ya tano ni Mntamba (Singida) iliyokuwa na wahitimu  96, ya sita ni Ikolo (Singida) iliyokuwa na wahitimu 63, ya saba ni Kamwala (Songwe) iliyokuwa na wahitimu 48, ya nane ni Kibutuka (Lindi) iliyokuwa na wahitimu 65, ya tisa ni Mkulumuzi (Tanga) iliyokuwa na wahitimu 40, huku shule ya mwisho ikiwa Kitwai ‘A’ (Manyara) iliyokuwa na wahitimu 57.

Katika hatua nyingine, Dk. Msonde alitoa tathmini ya ufaulu kimikoa na alitaja mikoa 10 iliyoongoza katika matokeo hayo kitaifa, huku Dar es Salaam ikishika namba moja ikiwa na wanafunzi 66,694, kati ya hao 58,572 walifaulu kwa alama za A hadi C,  ambayo ni sawa na asilimia 87.82.

Alitaja mkoa ulioshika namba mbili kuwa ni Geita uliokuwa na watahiniwa 36,979, kati ya hao waliofaulu ni 32,153, sawa na asilimia 86.95, Kagera ilishika namba tatu ikiwa na watahiniwa 41,984, huku waliofaulu wakiwa 35,433, sawa na asilimia 84.40.

“Iringa imeshika nafasi ya nne na kati ya watahiniwa 24,784 waliofanya mtihani waliofaulu ni 20,606, sawa na asilimia 83.14, Kilimanjaro ulikuwa na wahitimu 36,582 na waliofaulu wakiwa ni 29,884, sawa na asilimia 81.69,” alisema.

Pia alisema Njombe imeshika nafasi ya sita na kati ya watahiniwa 19,142, waliofaulu ni 15,362, sawa na asilimia 80.25, Arusha imeshika nafasi ya saba ikiwa na watahiniwa 38,306 na waliofaulu 29,624, sawa na asilimia 77.34.

Alisema Mwanza imeshika nafasi ya nane ikiwa na watahiniwa 70,367 na kufaulisha 54,367, sawa na asilimia 77.26, Katavi imeshika nafasi ya tisa ikiwa na watahiniwa 9,389, huku waliofaulu wakiwa ni 7,190, sawa na asilimia 76.58 na nafasi ya 10 imeshikwa na Tabora, uliokuwa na wahitimu 33,696, na kati ya hao waliofaulu ni 24,803, sawa na asilimia 73.61.

Pia alisema tathmini hiyo ilifanyika katika ngazi ya halmashauri na alizitaja halmashauri 10 zilizoongoza kitaifa.

Alisema Kinondoni (Dar es Salaam) ilikuwa na watahiniwa 11,701 na kati ya hao waliofaulu ni 10,884, sawa na asilimia 93.02 na imeshika namba moja katika orodha hiyo.

Alisema namba mbili imeshikwa na Moshi (Kilimanjaro) iliyokuwa na watahiniwa 3,436 na kati yao waliofaulu ni 3,191, sawa na asilimia 92.87, Arusha imeshika namba tatu na ilikuwa na watahiniwa 10,578 na kati ya hao waliofaulu ni 9,787, sawa asilimia 92.52.

Aliitaja Ilala (Dar es Salaam) kuwa imeshika namba nne, ikiwa na wanafunzi 12,778 na kati yao waliofaulu ni 11,815, sawa na asilimia 92.46, Mafinga (Iringa) imeshika namba tano, ikiwa na watahiniwa 1,887 na waliofaulu ni 1,725, sawa na asilimia 91.41.

Alisema namba sita imeshikwa na Mlele (Katavi), iliyokuwa na watahiniwa 545 na waliofaulu walikuwa 498, sawa na asilimia 91.38, Kigamboni (Dar es Salaam) imeshika namba saba, ikiwa na watahiniwa 3,077 na kati ya hao, waliofaulu ni 2,803, sawa na asilimia 91.10.

Alisema Nzega Mji (Tabora) imeshika namba nane, ikiwa na watahiniwa 1,649 na kati ya hao, waliofaulu ni 1,495, sawa na asilimia 90.66, namba tisa imeshikwa na Mpanda (Katavi), ikiwa na watahiniwa 2,332 na kati ya hao, waliofaulu ni 2,099, sawa na asilimia 90.01, Chato (Geita) ilikuwa na watahiniwa 7,246 na waliofaulu ni 6,497, sawa na asilimia 89.66.

Akizungumzia tathmini ya matokeo hayo kwa somo moja moja, alisema matokeo ya ufaulu wa watahiniwa katika masomo ya Kiswahili, Sayansi, Maarifa ya Jamii na Hisabati upo juu ya wastani.

Hata hivyo, alisema takwimu za matokeo zinaonesha ufaulu katika somo la Kiingereza upo chini ya wastani, hivyo juhudi za makusudi zinapaswa kufanyika ili kuinua kiwango cha ufaulu cha somo hilo.

Pia alisema wamefuta matokeo ya watahiniwa 10 waliobainika kufanya udanganyifu kwa mujibu wa kifungu cha 32(2)(b) cha kanuni za mtihani na wameshauri mamlaka kuwachukulia hatua wote waliohusika katika udanganyifu huo.

Alisema kuna baadhi ya matokeo yamezuiliwa kutokana na watahiniwa kuugua ama kupata matatizo na kushindwa kufanya mitihani kwa masomo yote au baadhi ya masomo.

“Watahiniwa wamepewa fursa nyingine ya kufanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi (PSLE) mwaka 2018 kwa mujibu wa kifungu cha 30 (1) cha kanuni za mtihani,” alisema.

Kwa upande wake, mwanafunzi bora aliyeongoza kwa kushika nafasi ya kwanza kitaifa katika matokeo hayo, Khadija, alisema ndoto yake kubwa ni kuwa daktari bingwa wa upasuaji, ili kuwasaidia Watanzania wenye matatizo mbalimbali, ikiwamo akina mama na watoto.

Kauli hiyo aliitoa mjini hapa jana, wakati wa mahojiano na gazeti hili yaliyofanyika shuleni hapo.

Khadija alisema sababu kubwa iliyomvutia kuamua kuwa daktari inatokana na kuwapo kwa vifo vya wajawazito na watoto vinavyoweza kudhibitiwa iwapo kutakuwapo na madaktari bingwa.

Alisema katika kutimiza ndoto hiyo, ndiyo maana aliamua kuweka mkazo mkubwa wa kuongeza bidii katika masomo ya sayansi, kuhakikisha anafaulu vizuri ili kuanza kufikia malengo aliyonayo.

“Ukiangalia leo hii watu wengi wanapoteza maisha, hususan wajawazito wanaokwenda kujifungua hospitali, lakini unaweza kukuta hilo linasababishwa na kukosekana kwa madaktari bingwa, hivyo nitakapotimiza ndoto yangu nitatoa mchango wangu kuwahudumia,” alisema.

Pia alisema siri ya mafaniko hayo ni kusoma kwa bidii, kuwaheshimu wazazi na jamii kwa ujumla, ikiwamo kuweka utaratibu mzuri wa kumuabudu Mungu, jambo lililomsaidia kuibuka kinara wa matokeo ya darasa la saba.

Naye Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Msobi Mandwa, alisema sababu iliyochangia matokeo hayo ni kujiunga na Umoja wa Shule zinazofanya vizuri Tanzania (Mems na Lareaga) kwa kushirikiana mitihani ya pamoja ili kuwapima wanafunzi hao kabla ya kufanya mitihani ya Taifa.

Alisema umoja huo umekuwa ni chachu kubwa ya kuwawezesha wanafunzi kujiandaa vya kutosha kwa mitihani yao.

Akizungumza namna alivyopokea matokeo hayo, mama mzazi wa Khadija, Jeni Kihiyo, alisema wameyapokea vizuri na mtoto wao amefuata mkondo wa ndugu zake wanaosoma ngazi za juu.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles