24.3 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

WAUAJI KIBITI WADHIBITIWA MSUMBIJI

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM


WATU wanne wanaodhaniwa kuwa ni miongoni mwa watekelezaji wa mauaji katika wilaya za Kibiti, Mkuranga na Rufiji mkoani Pwani wameuawa nchini Msumbiji.

Mkuu wa Jeshi la Polisi  (IGP) Simon Sirro amesema wahalifu waliodhibitiwa katika maeneo ya Kibiti, Mkuranga na Rufiji sasa wamekimbilia Msumbiji.

Aliyasema hayo Dar es Salaam jana   wakati wa kutiliana saini mkataba wa makubaliano na Jeshi la Polisi la Msumbiji kushirikiana kupambana na uhalifu katika nchi hizo mbili, hasa maeneo ya mpakani.

Kwa sababu hiyo, IGP Sirro amewaonya wahalifu hao kwamba hata huko hawatakuwa salama kwa sababu Jeshi la Polisi Tanzania linashirikiana na Msumbuji katika kupambana na uhalifu kwa kubadilishana taarifa.

Alisema wahalifu hao waliokimbilia   Msumbiji ambao wamekuwa wakisikika wakizungumza Kiswahili wameanza kutekeleza vitendo vya uhalifu ikiwamo mauaji nchini humo.

Akizungumzia mkataba huo, alisema utahusisha kubadilishana taarifa, mbinu na uzoefu katika kupambana na ugaidi na dawa za kulevya ambazo zinaathiri nguvu kazi katika  mataifa yao.

“Wale wahalifu waliokimbilia Msumbiji au Congo hawako salama. Majeshi yetu ya polisi yanashirikiana, ndiyo maana leo (jana) tunatiliana saini makubaliano ya ushirikiano,” alisema Sirro.

Aliwataka wahalifu hao waliokimbilia Msumbiji kuachana na uhalifu kwa sababu wakiendelea watakamatwa kwa ushirikiano wa majeshi hayo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Jeshi la Polisi la Msumbiji, Bernardino Rafael alisema nchi yake inakabiliwa na wahalifu kutoka nchi nyingine, hivyo makubaliano hayo yatasaidia kupunguza uhalifu.

Alisema wanataka kudhibiti mipaka yao dhidi ya wahalifu hao ambao wanahatarisha amani katika nchi hiyo pamoja na nchi za jirani.

“Watu wenye ualbino wanauawa kwa imani za kishirikina na taarifa zinaonyesha wahalifu hao wanatoka mataifa mbalimbali. Tutashirikiana na Polisi  Tanzania katika kubadilishana taarifa ili kukomesha mauaji hayo,” alisema Rafael.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles