28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Waturuki kuwekeza maeneo saba nchini

Na ANDREW MSECHU


   

VIONGOZI  wa kampuni saba kutoka    Uturuki wamewasili nchini kwa ajili ya kuwekeza katika maeneo saba muhimu, ikiwa ni sehemu ya kuendeleza uhusiano kati ya nchi hizo.

Akizungumzia kuwasili kwa  kampuni hizo  Dar es Salaam jana, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Damas Ndumbaro alisema wawekezaji hao watatembelea maeneo hayo kukabidhiwa sehemu ya ujenzi wa viwanda na miradi ya uwekezaji wao.

Alisema wafanyabiashara hao  wamelenga kuwekeza katika viwanda vya nguo katika Mkoa wa Simiyu, viwanda vya sukari, viwanda vya saruji, kilimo, vifaa vya ujenzi, nishati na ujenzi wa hoteli za kisasa.

“Ziara hii ni sehemu ya maendeleo ya juhudi za makusudi zilizoanzishwa na Rais Dk. John Magufuli katika kuifanya Tanzania iwe nchi ya viwanda na kufikia kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwkaa 2025,” alisema Dk. Ndumbaro.

Alisema katika ziara ya siku saba nchini iliyoanza jana, wawekeaji hao watakutana na viongozi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirkiano wa Afrika Mashariki, Wizara ya Viwanda na Biashara, Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Chama cha Wanyabiashara, Kilimo na Viwanda (TCCIA), Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji (EPZA), Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA).

Alisema pamoja na kukutana na wadau hao leo, wawekezaji hao watatembelea maeneo ya uwekezaji na kesho watakwenda Dodoma ambako wamenuia kujenga hoteli za kisasa za nyota tano pamoja na maduka makubwa ya kisasa (Shopping Mall).

Alisema Jumatano watasafiri kwenda mkoani Simiyu ambako wamenuia kujenga viwanda vya nguo na Alhamisi watakutana na uongozi wa mkoa huo ambako watafanya kikao mahususi na uongozi wa mkoa huo, kisha watarejea Dar es Salaam na kurudi kwao baada ya kukabidhiwa maeneo ya uwekezaji.

Akifafanua, Dk. Ndumbaro alisema uwekezaji katika viwanda vya nguo mkoani Simiyu utakua wa kisasa, ambao utahusisha uchakataji wa pamba katika hatua ya awali hadi ya mwisho, ikiwa ni sehemu ya kuondokana na uuzaji wa pamba ghafi nje, ambayo Uturuki ilikuwa miongoni mwa wanunuzi.

Alisema hatua hiyo imefikiwa kutokana na uhusiano mzuri baina ya Tanzania na Uturuki hasa baada ya Serikali kuamua kufungua rasmi ubalozi wa Tanzania nchini Urturuki mwaka 2016, baada ya Uturuki kufungua ubalozi wake nchini mwaka 2009.

“Tangu Serikali ilipofungua ubalozi wake Uturuki mwaka 2016 urari wa biashara umeongezeka kwa kasi na kuwa chanya zaidi kwa Tanzania na tumekuwa tukiuza vitu vingi kwao kuliko tunavyonunua kwao,” alisema.

Alieleza   mwaka 2017, Tanzania ilinunua bidhaa zinazofikia Sh   bilioni nane kutoka Uturuki lakini iliuza bidhaa zinazofikia Sh bilioni 119  kwa Uturuki.

Alisema kuwapo  safari za moja kwa moja za ndege za Shirika la Ndega la Uturuki kuja nchini pia kumeongeza idadi ya watalii nchini  kutoka watalii 2700 mwaka 2012 hadi kufikia watalii 9200 mwaka 2017.

Alisema kwa sasa kuna kampuni 48 za Uturuki zilizowekeza nchini kwa uwekezaji unaofikia Dola za Marekani bilioni 324   ambazo zimezalisha zaidi ya ajira 35,000 kwa Watanzania na uwekezaji mpya unaotarajiwa katika maeneo hayo saba yaliyotajwa, unatarajiwa kuzalisha ajira za moja kwa moja zaidi ya 1,400.

Balozi wa Uturuki   nchini, Ali Davutoglu alisema hatua hiyo ni mwendelezo wa ushirikiano baina ya nchi hizo mbili ambazo zimekuwa na ushirikiano wa biashara kwa muda mrefu.

Alisema ushirikianio huo umekuwa wa manufaa inayoendelea kuimarisha ushirikiano uliopo.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles