24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Watumishi watakiwa kutogeuza ofisi vijiwe

RAMADHAN HASSAN-DODOMA

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amewataka watumishi wa Wizara yake kutogeuza ofisi vichaka vya ubadhirifu na kuendekeza maslahi binafsi kwa kisingizo cha ukosefu wa fedha.

Kauli hiyo ameitoa wakati akifungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kilichofanyika jana jijini hapa.

“Katika kipindi hichi Serikali inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya kiuchumi hivyo kumekuwepo na matatizo ya kifedha. Hata hivyo matatizo hayo ya kifedha sio kichaka kwa watumishi wa umma kukosa uaminifu, kutumia vibaya madaraka yao, kufanyakazi kwa upendeleo na kuendekeza maslahi binafsi,” alisema.

Alisema katika mwaka wa fedha unaoishia Juni 30,  kumekuwa na mtiririko mzuri wa fedha za bajeti ambazo zimewezesha watumishi kulipwa baadhi ya stahiki zao.

Alisema mabaraza ya wafanyakazi katika kila chombo na taasisi za wizara, yanapaswa kujadili kwa uhuru na uwazi mapungufu na kuyatolea njia mbadala za utatuzi.

“Mapungufu na madhaifu yasemwe kwa uhuru na uwazi ili yafahamike na kutatuliwa,” Lugola alibainisha.

Aliwataka watumishi kuzingatia sheria, kanuni na nidhamu katika kutimiza majukumu yao kwani serikali inaendelea kuboresha mazingira bora kwa watumishi wa umma.

Kadhalika, Lugola alikemea vitendo vya baadhi ya wajumbe wa baraza hilo kuwakilishwa na watu ambao hawakuchaguliwa.

“Hapa ni kama nimeuziwa mbuzi kwenye gunia. Nimefungua kikao cha makundi mawili kwa pamoja. Kundi la wajumbe wanaowawakilisha wafanyakazi na watu ambao wanawawakilisha wajumbe ambao walipaswa kuwawakilisha wafanyakazi,” alieleza.

Makamu Mwenyekiti wa baraza hilo, Ramadhani Kailima, alisema pamoja na ajenda nyingine, kikao hicho kitajadili bajeti na changamoto za watumishi na kuishauri wizara hatua za kukabiliana na changamoto hizo.

Kailima ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, alisema changamoto zote zitapokelewa na kutekelezwa.

“Baraza hili ni chombo huru. Nawaomba watumishi wote waeleze changamoto zao kwa uwazi na tutazifanyia kazi,” alieleza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles