25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

WATUMISHI WA AFYA WAIHUJUMU SERIKALI MAGU

 

Na MASYENENE DAMIAN-MWANZA

BAADHI ya watumishi katika Idara ya Afya wilayani Magu mkoani Mwanza, wameendelea kupuuza maagizo mbalimbali yanayotolewa na Serikali kuhusu dawa za binadamu kwa kuendelea kuuza dawa za Serikali katika vituo binafsi vya afya na maduka ya dawa.

Hayo yamebainishwa katika taarifa ya udhibiti wa dawa za Serikali uliofanywa na Halmashauri ya Wilaya hiyo ikishirikiana na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) Kanda ya Ziwa kwa kipindi cha miezi minne kuelezea ukaguzi maalumu wa chakula, dawa na vipodozi ambapo jumla ya maduka 55 yalikaguliwa.

Kwa mujibu wa taarifa ya TFDA, baadhi ya maduka yalikutwa na dawa mbalimbali ambazo hazina usajili kutoka mamlaka hiyo, hivyo ubora na usalama wake kutofahamika na dawa kadhaa zisizo na usajili zilikamatwa kwa kukiuka kifungu cha 22 sheria ya chakula, dawa na vipodozi namba 3 ya mwaka 2003 ambapo vipodozi vilivyopigwa marufuku kwa mujibu wa kifungu cha 87 cha sheria hiyo vyenye thamani ya Sh 382,000 na uzito wa kilogramu 8 vilikamatwa.

Akizungumzia suala hilo juzi, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu, Lutengano Mwalwiba, alisema licha ya upatikanaji wa dawa za msingi zinazohitajika kuimarika wilayani humo, bado kuna watu wachache wanaendelea kuhujumu dawa za Serikali kwa kuiba na kuzipeleka katika vituo binafsi vya afya na maduka ya dawa.

“Ukaguzi huu tuliofanya kwa kushirikiana na TFDA na hospitali ya wilaya, tulibaini maduka manne yalikutwa na dawa za Serikali, tumechukua hatua mbalimbali ikiwemo kuwafikisha mahakamani, kuwanyang’anya leseni za biashara ambapo hawatafanya tena biashara yoyote hapa Magu,” alisema Mwalwiba.

Aliwataja wamiliki wa maduka waliokamatwa kuwa  ni Annastazia Samweli wa Kisesa, Fabian Magingi, Mbojie Majani, Ntemi Nyanda na Thereza Pauline na Queen DLDM ambao maduka yao yalikutwa yakiuza dawa zisizotambuliwa na TFDA, ambapo muuguzi Pastory Frank wa kituo cha afya Nyanguge, alikamatwa kwa kuiba kifaa cha kusaidia hewa (Oxygen Concentrator) na kukiuza jijini Mwanza.

Naye Mfamasia wa Wilaya hiyo, Sikujua Silvanus, alisema yapo maduka yaliyokutwa na dawa zilizoisha muda wa matumizi.

“Magu kuna maduka 72 tu yenye vibali halali na yaliyokidhi vigezo vyote, ukitembea mitaani utakutana na utitiri wa maduka ya dawa, tumeanzisha mkakati wa kuyafuatilia na kuyabaini kwa mujibu wa Sheria ya Baraza la Famasia ya mwaka 2011 na ile ya TFDA ya mwaka 2003.

Ukaguzi huo ulifanywa katika maduka ya dawa muhimu za binadamu 34, famasi za jumla na rejareja mbili, maduka ya dawa za mifugo matano, zahanati nne, maduka nane ya vipodozi na mashine mbili za kuchunguza magonjwa ya binadamu ambapo maduka 10 ya dawa yalifungwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles