23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Watumishi vyama vya ushirika kufanyiwa tathmini ya taaluma

Na Nyemo Malecela -Kagera

SERIKALI inatarajia kufanya tathmini ya taaluma ya watumishi wa vyama vya ushirika nchi nzima, ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kukomesha vitendo vya ubadhirifu wa mali za vyama hivyo vinavyokithiri kwa sasa.

Naibu Waziri wa Kilimo, Omary Mgumba alisema hayo juzi mkoani Kagera ambako anaendelea na ziara ya kikazi.

Alisema Serikali imelazimika kufanya tathmini kuhakiki vigezo vya kufanya kazi katika vyama hivyo, baada ya kubainika watumishi wengi wa vyama vya ushirika nchini wanajihusisha na ubadhirifu wa fedha na mali za vyama vya ushirika.

“Kutokana na kuwapo matukio ya mara kwa mara ya watumishi hao kutajwa katika ubadhirifu, nililazimika kwenda Chuo cha Kilimo cha Moshi (KNCU) ili kuchunguza kama wanafundisha ujambazi kwa wahitimu wa chuo hicho ambao wanafanya kazi kwenye vyama vya ushirika.

“Nikiwa chuoni hapo, niliambiwa watumishi wengi waliopo kwenye vyama vya ushirika hawajasoma katika chuo hicho. 

“Jambo lililotulazimu kufanya uchunguzi huo ni kutaka kubaini ni watumishi gani hawana vigezo wapo katika taasisi hizo ili tuweze kuwaondoa,” alisema.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Brigedia Jenerali Marco Gaguti, alisema msimu wa kilimo cha kahawa, mkoa huo umekusudia kukusanya tani milioni 52 na tayari zimekusanywa tani milioni 51.5.

“Kazi inaendelea hadi Mei, mwaka huu. Wilaya za Kyerwa na Karagwe tuko msimu mdogo (ndagashe),” alisema Gaguti.

Alisema kumekuwapo na malalamiko kuwa wanunuzi binafsi wa kahawa walikatazwa kununua zao hilo.

“Tulipokea maombi juu ya wanunuzi binafsi na kampuni, lakini bahati mbaya kiwango cha fedha walichotaja kilikuwa cha chini.

“Mfano wapo waliotoa ofa ya Sh 1,200 kwa kilo, hawaelezi mchanganuo wa kodi pamoja na gharama za usafirishaji kutoka kwa mkulima, wakati vyama vya ushirika vinalipa Sh 1,100 kwa kilo, baada ya kutoa huduma nyingine zote,” alisema Gaguti.

Alisema mkoa ulitarajia wafanyabiashara binafsi kutaja ofa ya bei kuanzia Sh 1,500 na zaidi kwa kilo.

Gaguti alisema kuwa alijitokeza mfanyabiashara mmoja ambaye ni Karagwe Market, lakini ilipofikia hatua ya pili ya maongezi, alisema hawezi kuhimili bei na kuishusha, hivyo naye ikashindikana.

“Pia Amri Hamza (mfanyabiashara binafsi) alitangaza ofa kwa daraja la pili na la tatu, lakini hakutaja bei yoyote. 

“Hivyo kama mkoa ulishindwa kuwalinda wanunuzi binafsi kwa sababu hawakuwa tayari kwa bei wanayoitangaza kwa mkulima.

“Hoja ya wanunuzi binafsi wamezuiliwa kununua kahawa haina mashiko sahihi, kwani tulishindwana katika bei,” alisema Gaguti.

Alisema kahawa inayonunuliwa kwa wakulima, hainunuliwi na Serikali, ni wanunuzi binafsi kutoka kwenye vyama vya ushirika.

Gaguti alisema mkoa umevitaka vyama vya ushirika kubainisha mali walizonazo ili ziweze kutumika kama sehemu ya uendeshaji wa ushirika.

“Lengo ni kutaka kuona hizo mali za ushirika zinachangia nini kwenye uzalishaji, maana vyama vingi vinategemea fedha kutoka kwenye kahawa inayokusanywa na kuuzwa,” alisema Gaguti.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles