24.5 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Watumishi hewa waanza kukamatwa

Rais Dk. John Magufuli
Rais Dk. John Magufuli

*Polisi wawabeba majumbani chini ya ulinzi makali

*Kilio chawakumba walimu wastaafu, halmashauri

Na Veronica Romwald, Dar es Salaam

NI mshikemshike. Ndivyo unavyoweza kusema  baada ya vyombo vya dola kuanza kuwatia mbaroni watumishi hewa kwa kuwafuata na pingu majumbani.

Hatua hiyo inachukuliwa ikiwa ni mkakati wa Serikali ya awamu ya tano  ya Rais Dk. John Magufuli,  kupambana na watendaji ambao wamekuwa wakiisababishia hasara  ya kulipa mamilioni ya shilingi kama mishahara kwa watumishi hewa.

Habari zinasema,  juzi mtumishi mmoja wa zamani katika  Mkoa wa Kigoma  alifuatwa na   polisi ambao walimtia mbaroni nyumbani kwao Ubungo Kibangu  Dar es Salaam.

Hilo lilifanyika juzi mchana   na kuibua hofu kwa majirani ambao waliliambia gazeti hili kuwa  askari hao walifika nyumbani kwao na mtumishi huyo na kumfunga pingu mikono na miguuni na kuondoka naye.

“Walikuja na kumkamata dada Mwajuma ambaye alikuwa hapa nyumbani kwa mapumziko ya likizo… sasa wazazi wake walipohoji amefanya nini waliambiwa kama wako tayari waende Mtwara na Sh milioni 21 ambazo alilipwa kama mtumishi.

“Lakini pia inadaiwa awali alikuwa akitumia jina la mtu mwingine alipokuwa Halmashauri ya Mtwara. Alilipwa fedha hizo kwa kutumia jina hilo na  hata alipopata kazi Kigoma   alikuwa akiingiziwa mshahara kwa jina hilo hadi kufikia kiasi hicho cha fedha.

“… na malipo haya ya mishahara alikuwa akilipwa tangu mwaka 2014 na kufikia kiasi hiki ambacho inadaiwa alikopa fedha benki.

“Baada ya tukio hili kwa kweli baba na mama yake wamechanganyikiwa na kutangaza kuuza nyumba yao Sh milioni 40,” alisema mmoja wa majirani walioshuhudia tukio hilo.

Gazeti hili lilipiga kambi   jana katika eneo hilo la Mtaa wa Ubungo Kibangu   kuonana na wazazi wa ‘mfanyakazi huyo hewa’ lakini muda wote nyumba ilikuwa kimya  huku milango ikiwa imefungwa muda wote.

Ilipofika saa 9.00 alasiri mwandishi   alimuona mtu mmoja akifungua mlango na  alipoulizwa walipo wenye nyumba alijibu kwa kifupi ‘hawapo wenyewe wamekwenda Tanga’.

“Mimi mwenye ni mgeni hapa wenye nyumba hawapo wamekwenda Tanga kuna tatizo zito la familia,” alijibu   na kuingia ndani.

Mkoani Ruvuma

Wakati huohuo, taarifa kutoka wilayani Nyasa mkoani Ruvuma, zililieleza gazeti hili kuwa walimu watano wastaafu wamekwisha kukamatwa na polisi kwa madai ya kupokea mishahara hewa.

Mbali na walimu hao,   muuguzi mmoja pia alikamatwa.

Mmoja wa waliokumbwa na hali hiyo ni Marco Nyimbi ambaye ni mwalimu mstaafu wa Shule ya Msingi Muungano huko Wilaya ya  Nyasa mkoani Ruvuma.

Akizungumza na Mtanzania alisema  alipigwa  butwaa na kushangazwa na hatua ya kukamatwa yeye na wenzake watano wakidaiwa kuwa ni watumishi hewa.

“Mimi nilikuwa mtumishi halali wa Serikali. Nilistaafu kwa mujibu wa sheria Aprili 22, 2014 na nililipwa mafao yangu Sh milioni 59 bila matatizo yoyote,” alisema.

Alisema hata hivyo, Juni 12 mwaka huu, alitumiwa ujumbe kuwa anahitajika kufika katika Ofisi ya Ofisa Upelelezi Liuli kwa ajili ya kutoa maelezo ambayo hakuelezwa yalihusiana na nini.

“Sikukataa wito, nilikwenda siku iliyofuata katika ofisi hiyo lakini sikujua niliitwa huko kwenda kufanya nini na niliwakuta wenzangu Fabian Kilapilo tuliyekuwa tunafundisha naye Muungano, Ernest Ngayomba (Shule ya Msingi Mengele), Philipo Maendaenda  aliyekuwa akifundisha Shule ya Sekondari Kihesa na mwenzetu mwingine mmoja.

“Tukiwa pale tulielezwa kuwa tumeisababishia Serikali kwa kuingiziwa mishahara huku tukiwa si watumishi halali, kila mmoja alitajiwa kiasi anachodaiwa kuchukua, mimi niliambiwa kwenye akaunti yangu walibaini ziliingizwa Sh milioni 2.32.

“…kwa kweli nilishangazwa na kauli ile, niliwaeleza  kuwa kamwe siwezi kufanya hivyo hata siku moja na kwamba fedha ambazo niliingiziwa na kuzitoa ni zile za mafao yangu.

“Lakini hawakunisikiliza na wakaniamuru nivue viatu niingie ndani, waliniweka ‘lock-up’ na wenzangu wanne ambao wote tulikuwa tumestaafu kazi siku nyingi,” alisema Nyimbi.

Alisema siku hiyo walilala mahabusu na  kulipokucha saa moja asubuhi aliweza kutolewa kwa dhamana na ndugu zake.

“Nilipotolewa nilirudi nyumbani nikaenda kutazama benki (taarifa), zangu  ili nijiridhishe kama niliingiziwa fedha hizo lakini nilikuta   sikuwahi kuingiziwa fedha hizo, sasa sijui wao walitoa wapi taarifa hizo lakini ukweli imenisikitisha mno,” alisema.

Naye Fabian Kilapino, aliliambia MTANZANIA kuwa aliitwa katika ofisi hiyo kujieleza akidaiwa kuwekewa  Sh milioni 4.64 katika akaunti yake.

“Nami nilikuwa mwalimu wa Muungano nilistaafu pamoja na mwenzangu.  Niliitwa pale na niliitikia wito na nilipokwenda nilikutana na wenzangu, tulipoulizwa tulijibu kile tulichoamini ndiyo ukweli wenyewe.

“Lakini ghafla tulishangaa kuambiwa tuvue viatu na kuwekwa ndani hadi kesho yake,” alisema Kilapino.

Alisema alipotolewa siku ya pili alikwenda kutazama taarifa yake ya  benki ambako alikuta  ziliingizwa Sh 829,000 ambazo hata hivyo hakujua zilitumikaje.

“Nilipostaafu nililipwa vizuri kabisa mafao yangu   Sh milioni 56.9… ilikuwa Aprili 2014. Kwa kweli nilishangaa kukuta Sh  829,000 kwamba ziliingizwa na kutoka huku nikiwa sina taarifa hiyo,” alisema.

Kilapino alisema kutokana na hali hiyo alikubali kulipa kiasi hicho cha fedha ingawa hadi leo hajui nini kilitokea hadi zikaingizwa katika akaunti yake.

“Sielewi hadi leo (jana)  ilikuwaje fedha hizi ziliingizwa na kutolewa huku mwenyewe nikiwa sina taarifa.

“Nimekubali kuzilipa hizo fedha lakini kwa kweli tumedhalilishwa kwa sababu walitukamata bila kufuata utaratibu wa  ofisi kwani sisi tulikuwa tunasimamiwa na Mkurugenzi hivyo tunaona hii ni sawa na uhuni,” alisema.

MTANZANIA ilimpotafufa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora), Angella Kairuki,  kupata taarifa kuhusiana na staili hiyo mpya ya kamatakamata ya watumishi hew,a hakupatikana bungeni   na simu yake ilikuwa imezimwa wakati wote hadi tunakwenda mtamboni usiku.

Hivi karibuni akizungumza Dar es Salaam, Waziri Kairuki alisema serikali imewaondoa   watumishi 12,246 kwenye mfumo wa malipo ya mishahara kwa sababu mbalimbali ikiwamo umri wa kustaafu kwa lazima, kufukuzwa kazi, vifo na kumalizika  mikataba.

Waziri Kairuki alisema kuondolewa kwa watumishi hao kumeokoa Sh bilioni 25 ambazo zingelipwa kwa watumishi hao.

Alisema fedha hizo zingepotea endapo watumishi wasingeondolewa kwenye mfumo  ikilinganishwa na watumishi 10, 295 walioondolewa kwenye mfumo kuanzia Machi 15 hadi Aprili 30 mwaka huu.

Alisema pia kuwa watumishi hewa 1,951 wameongezeka ikiwa ni pamoja na Sh bilioni 1.8.

Waziri alisema  ofisi hiyo ilitoa maelekezo kwa Makatibu Wakuu, wakuu wa taasisi za umma na Mamlaka za Serikali za Mitaa  kuwasilisha taarifa ya watumishi hewa ifikapo   Juni 10, mwaka huu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles