28.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 19, 2024

Contact us: [email protected]

Watu milioni 40 waishi kimasikini Marekani

INAWEZA kuwa ngumu kuamini lakini ndio ukweli halisi, kwamba nchini Marekani masikini ni wengi lakini mamlaka husika hazijali.

Kwa mujibu wa mtafiti huru wa Umoja wa Mataifa (UN), hali hiyo inachochewa na dharau na sera za kikatili zilizopo nchini humo.

Utafiti huo unasema watu milioni 40 nchini humo wanaishi katika umaskini wa kutupa licha ya nchi hiyo kuongoza kwa kuwa tajiri zaidi duniani.

Mtaalamu wa masuala ya umaskini uliokithiri na haki za binadamu, Philip Alston, anafichua hali hiyo katika ripoti yake mpya baada ya kufanya ziara kwenye maeneo manne nchini humo.

Maeneo hayo ni California, Alabama, Georgia, Virginia Magharibi na Washington D.C ambako alishuhudia vitendo vya kikatili na dharau dhidi ya maskini vikiendana na sera za kikatili dhidi yao.

“Utawala wa Rais Donald Trump umekuja na sitisho kubwa la muda la kodi dhidi ya kampuni na matajiri huku ukipigia debe mbinu za kukata mfumo unaolenga kustawisha jamii,” anasema Alston.

Anasema mfumo huo unaonekana kuwafungia watu maskini kwa kuwa unaongeza tofauti kubwa kati ya maskini na matajiri na kuwaingiza mamilioni ya Wamarekani wanaofanya kazi na wasio na uwezo wa kufanya kazi kwenye ufukara mkubwa.

Moja ya makazi ya watu wa mji wa Escobares, Marekani

“Kinachoonekana zaidi ni dharau kwa maskini na wakati mwingine chuki dhidi ya maskini ambapo kumesheheni fikra za mshindi kuchukua vyote,” anasema mtaalamu huyo ambaye ripoti yake aliiwasilisha mbele ya Baraza la Haki za binadamu la Umoja wa Mataifa katikati ya mwezi uliopita.

Ushahidi wa dharau na chuki dhidi ya maskini upo dhahiri, akitolea mfano huko Skid Row, Los Angeles jimboni California ambako watu 14,000 wasio na makazi walikamatwa mwaka 2016 kwa kujisaidia haja ndogo kwenye eneo la umma.

Alston anasema watu hao wasio na makazi hawakuwa na la kufanya kwa kuwa katika mji huo hakuna vyoo vya umma na choo kimoja kinahudumia watu 200.

Anasema uwiano huo ni wa chini zaidi hata haufikii kiwango cha kwenye kambi za wakimbizi wa Syria zinazoendeshwa na Umoja wa Mataifa.

Halikadhalika, anagusia mfumo wa sheria wa Marekani akisema uko kwa ajili ya kukusanya mapato ya kuyanufaisha majimbo na si kusaidia maskini wanaohesabiwa kama wavivu na wasiostahili kusaidiwa.

Anatoa mfano mwingine wa wanasiasa, akisema baadhi ya aliozungumza nao wana fikra ya kwamba maskini ni matapeli na wanaishi kwa kutegemea mfumo wa ustawi wa jamii pekee.

“Marekani inaongoza kwa nchi za magharibi kwa kuwa na pengo kubwa la ukosefu wa usawa kwenye kipato na idadi ndogo ya watu wanaojitokeza kupiga kura miongoni mwa nchi zilizoendelea,” anasema.

Akihitimisha ripoti yake ya utafiti, Alston anasema mwenendo huo ni ushuhuda kuwa demokrasia ya Marekani inakabiliwa na tishio kubwa kwa sababu ya ufukara na sera zinazozidi kudidimiza demokrasia.

Ripoti hiyo inakuja huku tafiti nyingine zikifichua miji zaidi nchini humo yenye watu wengi wanaoishi katika umasikini wa kutupwa kiasi cha kutoamini kama ipo Marekani.

Miongoni mwa miji hiyo ni Escobares uliopo mpakani mwa Mexico na Marekani, ambao haujawahi kuorodheshwa kama moja ya miji masikini zaidi Marekani lakini wakazi wake wanaishi chini ya dola moja kwa siku.

Kwa mujibu wa Shirika la Kukadiria Idadi ya Watu, asilimia 62.4 ya wakazi 2,512 wa mji huo wanaishi chini ya dola moja kwa siku.

“Wakati mwingine nakosa chakula hadi nasaidiwa na jamaa zangu,” anasema Debora Hernández, raia wa Marekani aliyezaliwa na kulelewa katika mji huo.

Debora hajui kusoma wala kuandika, anasema alijifungua watoto saba lakini ni mmoja tu kati yao aliyebakia wengine wote walifariki dunia.

Alipoulizwa nini kilichosababisha vifo vyao anasema: ‘Sijui, na wala sikuambiwa kilichowasibu.”

Alipokuwa mdogo alipelekwa katika shule ya wanafunzi wanaohitaji huduma maalumu. Japo alikamilisha masomo ya msingi hakujifunza lolote.

Licha ya hayo yote Debora amekuwa akiishi na mume wake ambaye hana kazi kwa miaka mitatu sasa.

Paa la nyumba yao linavuja inaponyesha mvua na hali yao ya maisha kwa jumla inamfanya mtu kujiuliza iwapo kweli ipo siku mambo yatabadilika.

“Inabidi utoke hapa kila siku kutafuta kibarua vinginevyo utalala njaa,” anasema.

Mji wa Escobares uko mbali na miji iliyo na shughuli nyingi za kiuchumi na wakazi hawana njia nyingine ya kujikimu kimaisha.

“Wale waliyo na stakabadhi zinazohitajika, wanafanya kazi katika eneo la kaskazini,” anasema Homero Rosales.

“Cha kusikitisha ni kuwa lazima utengane na familia yako kwa miezi kadhaa kwenda kutafuta ajira, la sivyo wapendwa wako watakufa njaa,” anasema.

Homero ambaye ni baba wa watoto wanne anafanya kazi ya kujenga mabomba ya mafuta katika mji wa Pecos uliyopo Texas Magharibi.

“Mwanangu mkubwa alilazimika kuacha shule ili kufanya kazi na mimi,” anaeleza.

Wale ambao hawafanyi kazi ya ujenzi wa mabomba ya mafuta wanafanya vibarua katika miji mingine au wanategea msaada wa serikali kwa jamii, kununua chakula.

“Watu wanaoishi maeneo ya kusini mwa Marekani wanakabiliwa na viwango vya juu vya umasikini,” anasema Rakesh Kochhar, mtafiti katika kituo cha utafiti cha Pew mjini Washington.

Kituo hicho kinasema kiwango cha umasikini nchini Marekani kimefikia asilimia 12.3 na takriban watu milioni 40 wameathiriwa nao.

Watu masikini zaidi nchini Marekani wanaishi miji ya Mississippi, Louisiana na New Mexico, wengi wao wana asili ya ‘Uhispania na Afrika, ambao katika historia ya nchi hiyo wamekabiliwa na umasikini kwa muda mrefu,” anasema Rakesh Kochhar.

Miaka 13 iliyopita, Mji wa Escobares haukuwapo lakini mwaka 2005 ulitambuliwa kuwa moja ya miji nchini Marekani, kabla ya hapo watu walioishi sehemu hiyo hawakuwa chini ya mamlaka yoyote ya mji.

Baada ya Marekani kusikia kuwa mji wa karibu wa Rome ulikuwa na mpango wa kunyakua sehemu ya Mji wa Escobares, mambo yalibadilika.

Baadhi yao walizaliwa mjini humo na wengine wamepewa urai wa Marekani lakini kuna wale ambao hawana “stakabadhi rasmi” waliotoroka mauaji na utekaji nyara katika Jimbo la Tamaulipas.

Ukiwa mgeni katika Mji wa Escobares ni vigumu kubaini kuwa ni moja ya miji masikini nchini Marekani.

Hakuna visa vya watu kuishi mitaani kama vile vinavyoshuhudiwa mjini Los Angeles, au kukutana na watu wanaoishi katika hali ngumu kutokana na ubaguzi wa rangi katika miji ya Detroit na Baltimore.

Lakini watu wa Escobares wanaishi ndani ya mabaki ya treni au trela ambayo yameguzwa kuwa nyumba, yanayoweza kuhamishwa kutoka sehemu moja hadi nyingine.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles