27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Watu 7 familia moja wauawa kinyama

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza* Wakatwa mapanga usiku wa manane

* Mama alitakiwa kutoa sh 40, 000

 

Na Anna Luhasha, Sengerema

VILIO, simanzi na taharuki vimetawala katika Kijiji cha Sima, Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza, baada ya watu saba wa familia moja kuuawa kinyama kwa kukatwakatwa mapanga usiku wa kumkia jana.

Familia hiyo ilivamiwa na watu ambao idadi yao haijafahamika juzi usiku wa manane wakiwa wamelala katika nyumba tofauti.

Taarifa zilizopatikana wilayani Sengerema na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi, zinasema mauaji hayo huenda yamefanywa na watu wawili au mmoja na chanzo chake hakijajulikana.

Akizungumza na MTANZANIA akiwa eneo la tukio jana, Kamanda Msangi alisema taarifa za awali zinasema tukio hilo lilitoka juzi saa 9 usiku.

 

 

NDUGU ASIMULIA

Mmoja wa wanafamilia, Patrick John akielezea tukio hilo mbele ya Kamati ya Ulinzi na Usalama, alisema wavamizi hao baada ya kuingia ndani wakiwa na mapanga waliwaua wanafamilia hao kikatili.

Alisema wauaji wakiendelea kufanya unyama huo, ndugu yao Bestina Nasoro (10) alisalimika baada ya kujificha uvunguni na kujifunika nguo.

Aliwataja waliouawa kuwa ni pamoja na Augenia Kutega (64), mama wa familia hiyo ambaye kabla ya kushambuliwa na mapanga hadi kupoteza uhai, alilazimishwa kutoa Sh 40,000.

Wengine ni Mariam Philipo ambaye ni mdogo wa Augenia, watoto Leonard Alloys na Leonard Thomas ambao ni wanafunzi wa Shule ya Msingi Sima, Donald na Samson ambao walikuwa wafanyakazi wa shambani.

“Samson na Donard ni wafanyakazi wa hapa, lakini wao ni wenyeji wa Wilaya ya Ngara mkoani Kagera.

“Wakati wanavamiwa, kati yao mmoja alijaribu kupambana na wauaji, akazidiwa nguvu na wauaji… hali haikutulia kabisa ndipo wakalekeza mashambulizi kwa wengine,” alisema.

 

MKUU WA MKOA

Kutokana na mauaji hayo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella alifika kijijini hapo akiwa na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na kuagiza Jeshi la Polisi kuwasaka wahusika na ndani ya saa 48 wawe wamekamatwa wakiwa hai au marehemu.

Mongella alisema kamwe mauaji hayo ya kinyama hayatavumiliwa, atahakikisha wahusika wote wanasakwa kwa udi na uvumba.

“Polisi hakikisheni mnawasaka wauaji hawa ndani ya saa 48, lazima wakamatwe sheria ichukuwe mkondo wake… mauaji haya ya kinyama hatuwezi kuyavumilia,” alisema.

Mili ya marehemu wote, imehifadhiwa Hospitali Teule ya Sengerema kwa ajili ya uchunguzi ikiwa ni pamoja na kusubiri taratibu za mazishi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles