24.3 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

WATU 13 WAUAWA KIBITI

Na Mwandishi Wetu -DAR ES SALAAAM

*Ni katika mashambulizi ya polisi

*Mtandao wa ufadhili hadharani

JESHI la Polisi limefanikiwa kuwatia mbaroni na kuwajeruhi watuhumiwa 13 katika eneo la Gari Bovu, Kijiji cha Chamiwaleni, Wilaya ya Kibiti, Mkoa wa Kipolisi Rufiji, ambao walifariki dunia wakati wakipelekwa hospitali.

Taarifa iliyotolewa jana na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Simon Sirro, ilieleza kuwa kabla ya tukio hilo, jeshi hilo lilimkamata Abdallah Mbindimbi maarufu kwa jina la Abajani baada ya kupata taarifa za kiintelijensia kwamba anahusika na vitendo vya kufadhili, kusaidia, kuhifadhi na kushiriki uhalifu wa ujambazi maeneo mbalimbali.

IGP Sirro alisema kuwa Abajani alikutwa akiwa na majeraha maeneo mbalimbali ya mwili wake.

Inadaiwa mtuhumiwa huyo alionekana akijitibu majeraha hayo kwa njia za kificho.

“Mtuhumiwa huyu, alikamatwa kutokana na kuwepo kwa taarifa za kiintelijensia kuhusu yeye kuhusika na vitendo vya kufadhili, kusaidia, kuhifadhi na kushiriki uhalifu wa ujambazi maeneo mbalimbali,” alisema.

 

MAJIBIZANO YA RISASI

IGP Sirro alisema kuwa mtuhumiwa huyo alipohojiwa kuhusu tuhuma zinazomkabili, alikubali na alionyesha dhamira ya kwenda kuonyesha ngome yao.

“Saa tatu usiku katika mapori ya Kijiji cha Rungungu, mtuhumiwa akiambatana na askari polisi, alikwenda kuonyesha ngome ya watuhumiwa wenzake aliokuwa anashirikiana nao kufanya uhalifu.

“Baada ya kukaribia eneo la tukio, ulitokea upinzani mkali wa majibizano ya risasi jambo lililopelekea hata Abdallah Mbindimbi kujeruhiwa na risasi sehemu mbalimbali za mwili wake,” alisema IGP Sirro.

Alisema katika majibizano hayo, askari polisi walifanikiwa kuwajeruhi wahalifu 13.

Kwamba jitihada zilifanyika kuwapeleka hospitali majeruhi wote, lakini baadaye walifariki dunia kwa nyakati tofauti wakati wakipelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam.

“Walifariki kutokana na kuvuja damu nyingi zilizosababishwa na majereha ya risasi sehemu mbalimbali za miili yao,” alisema IGP Sirro.

Alisema kuwa miili ya marehemu imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

“Watuhumiwa saba kati ya 13 waliopoteza maisha kutokana na majibizano ya risasi, wametambuliwa kuwa ni

Hassani Njame, Abdallah Mbindimbi, Saidi Kilindo, Abdulshakuru Ubuguyu, Issa Mseketu,

Rajabu Thomas na Mohamed Kadude,” alisema na kuongeza kuwa miili ya watu wengine sita haikuweza  kutambulika mara moja.

 

SILAHA ZILIZOKAMATWA

IGP Sirro alisema kuwa watuhumiwa hao walikutwa na bunduki aina ya SMG tano ambazo ni mali ya Jeshi la Polisi zilizoporwa kwenye eneo la Mtengeni – Jaribu Mpakani, Wilaya ya Kibiti mkoani Pwani.

“Mbali na hizo, pia walikutwa na risasi za SMG 158, bomu la kurusha kwa mkono moja na mabomu ya kutuliza ghasia manne pamoja na pikipiki mbili,” alisema IGP Sirro.

Alisema kwa mujibu wa taarifa za utambuzi wa vielelezo vilivyopatikana eneo la tukio na baadhi ya miili ya watuhumiwa waliofariki dunia, inaonyesha kuwa walishiriki matukio ya uhalifu maeneo mbalimbali.

IGP Sirro aliyataja matukio hayo ambayo watuhumiwa hao wanadaiwa kuhusika nayo kuwa ni mauaji ya Mkuu wa Upelelezi (OC CID) na watumishi wawili wa Idara ya Maliasili katika tukio la Jaribu Mpakani.

Alisema pia wanahusishwa na kuuawa kwa askari polisi wanane katika tukio la Mkengeni wilayani Kibiti na trafiki wawili katika tukio la Bungu “B”.

“Watuhumiwa hao pia wanahusishwa na matukio ya mauaji ya Diwani wa zamani wa CCM katika tukio la Kibwibwi na Ofisa Mtendaji na Mwenyekiti wa Kijiji cha Mangwi wilayani Kibiti,” alisema Sirro.

 

WITO KWA WANANCHI

Kutokana na hali hiyo, IGP Sirro pamoja na mambo mengine aliwaondoa hofu wananchi akisema kwamba eneo hilo ni salama.

“Nawaomba wananchi waendelee kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi na kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu. Aidha nawaomba wananchi kutoa taarifa mara moja kwa Jeshi la Polisi wanapohisi kuna jambo lolote wanalolitilia shaka.

“Natoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Pwani, hususani maeneo ya Mkuranga, Kibiti na Ikwiriri, kuendelea na shughuli zao mbalimbali za kujiletea maendeleo.

“Nawasihi kwa dhati kabisa waendelee kutupatia taarifa zitakazosaidia kumaliza kabisa uhalifu kwenye eneo hili.

“Nitumie fursa hii kuwashukuru sana wananchi wa maeneo ya Mkuranga, Kibiti na Ikwiriri kwa ushirikiano mnaotupatia ambao umesaidia sana kuwadhibiti wahalifu,” alisema.

Alizitaka mamlaka za hospitali, zahanati, vituo vya afya, maabara za afya ya binadamu na maduka ya kuuza dawa za kutibu binadamu, zijiepushe na utaratibu wa kutoa matibabu kienyeji au kificho kwa watu waliojeruhiwa bila kufuata taratibu za kisheria ikiwamo kupata taarifa ya polisi kupitia fomu maalum ya kuruhusu matibabu (PF. 3).

IGP Sirro alisema wahalifu wakijeruhiwa ni lazima watafute matibabu, hivyo ni muhimu kwa idara hizo kutoa ushirikiano ili kuwezesha kuwakamata watuhumiwa maana baadhi yao wamekutwa na majeraha sehemu mbalimbali za miili yao na walikuwa wanaendelea kujitibia kwa kificho kwa kutumia dawa za hospitali.

“Napenda kuujulisha umma kwamba wapo baadhi ya watuhumiwa, wafadhili na washirika wa uhalifu na wahalifu wa ujambazi maeneo haya ambao bado hawajakamatwa.

“Jambo la kufurahisha ni kwamba taarifa zao zipo Jeshi la Polisi nchini na zinaendelea kufanyiwa kazi ili waweze kukamatwa na kufikishwa kwenye mkono wa sheria mara moja,” alisema.

 

WAFADHILI

IGP Sirro aliyataja majina ya watu wanaodaiwa kuwa wafadhili wa matukio hayo kuwa ni Anafi Kapelo, maarufu kama Abuu Mariam, Hassan Kyakalewa maarufu Abuu Salma, Shujaa au Dokta, Haji Ulatule, Sheikh Hassan Mzuzuri na Rashid Mtutula.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles