WATOTO WAFARIKI DUNIA KWA KUANGUKIWA UKUTA Z’BAR

0
2298

Na KHAMIS SHARIF-ZANZIBAR                 |                        


WATOTO wawili wamefariki dunia na wengine watatu kujeruhiwa baada ya kuangukiwa na ukuta wa boma la nyumba katika eneo la Bububu Kihinani Wilaya ya Magharibi “A” Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Thobias Sedoyeka alisema tukio hilo lilitokea jana saa 10 jioni.

Alisema watoto hao walikuwa wakicheza karibu na eneo hilo ndipo nyumba hiyo ilipoanguka na kusababisha vifo vyao.

Aliwataja watoto waliofariki dunia kuwa  ni Ali Kondo (4) na Mwajuma Hamada Denge (5) ambao wote ni wakazi wa Kihinani.

Alisema miili ya watoto hao ilizikwa jana Matemwe na Donge Mkoa wa Kaskazini Unguja huku majeruhi wa ajali hiyo wakiendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Mnazi Mmoja   Zanzibar.

“Wakati mwingine watoto unaweza kuwa huwaoni ukiamini kuwa wanacheza kumbe wapo kwenye eno hatarishi bila ya mzazi wala mtu yoyote kujua,” alisema Kamanda Sedoyeka.

Kutokana na tukio hilo, Kamanda Sedoyeka alitoa mwito kwa wazazi na walezi kufuatilia mienendo na mazingira ambayo hucheza watoto wao ikuwanusuru na matatizo yanayoweza kuepukika.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here