WATEULE MSAIDIENI RAIS KUTATUA KERO ZA WANANCHI

0
929

KWA muda mrefu sasa, Rais Dk. John Magufuli amekuwa akilia na wasaidizi wake kwa kile anachodai wapo ambao hawamuelewi.

Mbali ya kutomwelewa, wapo ambao wameshindwa kuendana na kasi ya Serikali ya kutatua kero za wananchi katika maeneo yao, hadi wanapokwenda viongozi wengine wa kitaifa.

Mambo haya amekuwa akiyasisitiza kwa muda mrefu, huku akichukua hatua kadhaa zikiwamo za kutengua baadhi ya teuzi za viongozi na kuweka watu wengine ili kuleta tija katika utendaji.

Kutokana na hali hiyo, tangu wiki hii imeanza, Rais Magufuli amekuwa na ziara ndefu aliyoianza mkoani Mwanza na wilaya zake, huku akizundua miradi na kuibua madudu mengi.

Baadhi ya miradi mingi imegundulika kuwa na madudu mengi, kwa mfano fedha nyingi zimetumika, lakini ufanisi hauonekani hata kidogo, jambo ambalo amewaagiza wasaidizi wake kuchukua hatua mara moja.

Baada ya juzi kuwasili mkoani Mara, Rais Magufuli alitembelea maeneo kadhaa kabla ya kuzungumza na maelfu ya wakazi wa mji wa Musoma na vitongoji vyake.

Katika mkutano huo, Rais alionekana kukerwa zaidi na tabia ya viongozi kushindwa kupanga ratiba ya kusikiliza kero za wananchi, kuanzia mkuu wa mkoa, wakuu wa wilaya na wakurugenzi.

Kutokana na hali hiyo, aliagiza kila kiongozi kwenye idara yake kupanga siku moja walau kwa wiki kwa ajili ya kuwasikiliza wananchi ili mwisho wa siku waweze kuendelea na maisha yao.

Jambo jingine ambalo limekuwa sugu katika Mkoa wa Mara, ni migogoro ya ardhi ambayo imesababisha kuwapo na mvutano kati ya vijiji na vijiji, huku wakuu wa wilaya na mamlaka zingine zikishindwa kumaliza migogoro hiyo.

Lakini pia, Rais amesikitishwa na miradi mikubwa kama ule wa maji katika Wilaya ya Bunda kutumia mamilioni ya fedha, lakini haujakamilika kwa miaka 10, huku wananchi wakiendelea kutaabika.

Hali hiyo, ilimsababisha Rais bila kificho kutamka hadharani kuwa  kuna mfanyabiashara mmoja mkoani humo, ‘amewatia mfukoni’ viongozi wa dola kuanzia mkuu wa mkoa hadi chini ndiyo maana wameshindwa kumchukulia hatua.

Tunaungana na Rais kuwa mtu mbadhirifu hakubaliki katika jamii na kwamba sheria lazima ichukuwe mkondo wake, kwa sababu hakuna mwana CCM aliyeko juu ya sheria na kama sheria ni msumeno utamkata tu bila kujali utajiri wake.

Tunaamini sasa, ziara hii itakuwa imefungua ukurasa mpya kwa watumishi wa umma kujitafakari zaidi na zaidi na kuona wapi wamejikwaa katika kutekeleza majukumu yao ya kuwatumikia wananchi wanyonge.

Sisi MTANZANIA, tunasema Rais amekuwa akisisitiza uwajibikaji kwa muda mrefu, sasa umefika wakati wa wateule wake kumuelewa na kutanguliza uzalendo wa kutatua matatizo makubwa yanayosibu wananchi.

Kwa mfano, katika suala la migororo ya ardhi, eneo hili linapaswa kushughulikiwa ipasavyo, hatupendi kuona matatizo yaliyotokea miaka 10 iliyopita ya wakulima na wafugaji kuuwana yanajirudia.

Kila kiongozi akitimiza wajibu wake kama miongozo yao inavyowaelekeza hakuna jambo litaloshindikana kutatuliwa na kujikuta Tanzania inaandika historia mpya ya kuondokana na migogoro hii isiyokuwa na tija.

Tunamalizia kwa kusema maagizo mazito ya Rais yatekelezwa haraka na si kusubiri kuagizwa kama watoto wadogo, wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi tunamini mmemsikia vizuri bosi wenu, tunategemea kuona mabadiliko makubwa kuanzia sasa badala ya kusubiri kusukumwa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here