26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

WATENDAJI MAHAKAMA TEKELEZENI MAAGIZO YA JAJI MKUU


MIONGONI mwa habari zilizopo katika toleo letu la leo ni kauli ya Jaji Mkuu, Profesa Ibrahimu Juma, kwamba lugha ya Kiingereza inayotumika mahakamani ni kikwazo kinachowazuia wananchi kupata haki, kwa kuwa wengi wanatumia Kiswahili.

Kwa mujibu wa Profesa Juma, aliyekuwapo mjini Arusha katika kikao cha kazi kinachojumuisha watendaji na wataalamu wa mahakama wanaotathmini utekelezaji wa mpango mkakati wa miaka mitano (2015-2020) na utekelezaji wa mradi wa maboresho ya utoaji huduma za mahakama na changamoto ambazo Benki ya Dunia (WB) ilizibaini na kuzitaja kuwa ndizo zilizosababisha ikubali kushirikiana na Serikali katika mradi wa kuifadhili Mahakama ya Tanzania, ni kwamba pia andiko la benki hiyo lilirejea utafiti uliogundua kwamba, asilimia 60 ya watumiaji wa mahakama walisema tovuti za mahakama hazitoi taarifa za kutosha kuhusu mashauri yao.

Pia kwa mujibu wa Profesa Juma, tovuti za mahakama bado hazizungumzi lugha ya Kiswahili. Kwamba bado kuna baadhi ya nyaraka zinawekwa katika lugha ya Kiingereza inayowatenga watumiaji wengi wa mahakama.

Sisi MTANZANIA Jumamosi tunaunga mkono kauli ya Profesa Juma, kwa sababu kuna baadhi ya watu wamewahi kuhoji siku za nyuma suala la lugha ya Kiingereza kutumika katika mahakama zetu.

Tunasema si vibaya kutumia lugha ya Kiingereza katika mashauri mbalimbali mahakamani, lakini ukweli utabaki palepale kwamba, matumizi ya lugha hiyo yanawalenga zaidi wanasheria kuliko wananchi wanaoshitaki au kushitakiwa.

Pia tunaunga mkono kauli ya Profesa Juma kwamba, tovuti za mahakama zetu zinatakiwa ziongee Kiswahili, ambayo ndiyo lugha ya Watanzania wengi hapa nchini na itakuwa ni msaada mkubwa kwa wananchi wa kawaida na hiyo itakuwa njia mojawapo ya kuendelea kuikuza.

Tunawaomba watendaji wa mahakama kuacha kuficha upungufu wao na waanze kutekeleza maagizo ya Profesa Juma, ikiwamo kujitathmini ili wapate nafasi ya kujirekebisha na wasirudie makosa yao.

Pia wawasaidie wananchi wapate haraka taarifa, kwa kuwa hiyo ni nyenzo muhimu katika kuwawezesha kupata haki zao mahakamani, kuwaongoza kufungua mashauri na ada stahiki.

Pia tunawaomba waendelee kuwasaidia wananchi, kwa kuwa hawajui sekta mbalimbali za kisheria zinahusikaje katika uendeshaji mashauri na utoaji wa haki.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles