31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Watanzania watatu wauawa shambulio la kigaidi Somalia

KISMAYO-SOMALIA

WATANZANIA watatu, mgombea wa urais katika uchaguzi ujao katika jimbo la Jubaland na mwandishi wa habari ni miongoni mwa watu 26 waliouawa katika shambulio linalodaiwa kutekelezwa na kikundi cha kigaidi cha Al-shabab  katika hoteli maarufu ya Asasey iliyopo Kismayo nchini Somalia usiku wa kuamkia jana.

Wengine waliouawa katika tukio hilo ni raia watatu wa Kenya, Wamarekani wawili, na raia mmoja kutoka Uingereza, Canada na China.

Majina ya raia hao wote waliouawa katika shambulio hilo hayajatajwa isipokuwa lile la Mwandishi wa habari na mgombea urais huyo wa Jubaland ambao wote ni raia wa Somalia.

Tayari kundi la Al-shabaab, limekiri kuhusika na shambulizi hilo la risasi na kujitoa muhanga lililojeruhi watu zaidi ya 30.

Katika shambulio hilo mwandishi wa habari maarufu mwenye uraia wa Canada na Somalia Hodan Nalayeh (43) na mumewe waliuawa.

Walioshuhudia tukio hilo wanasema maofisa wa ngazi ya juu wa kisiasa akiwemo mgombea wa urais katika uchaguzi ujao katika jimbo la Jubaland pia aliuawa.

Jana vikosi vya usalama katika mji wa mwambao wa kusini mwa Somalia vilimaliza makabiliano ya usiku kucha na wanamgambo walioishambulia hoteli hiyo maarufu.

Miili ya watu waliouawa imeondolewa kutoka kwenye hoteli hiyo huku msako ukiendelea kufuatia shambulio hilo kubwa zaidi kuwahi kutokea mjini Kismayo kwa miaka kadhaa.

Shambulio hilo lilianza kwa mlipuko wa bomu la kutegwa ndani ya gari lililokuwa kwenye lango la hoteli ya Asasey lilidumu kwa muda wa saa kadhaa.

Wanamgambo wa Alshaabab wanadaiwa  kugonga  gari lililokuwa limesheheni milipuko.

Walioshuhudia wanasema kuwa walisikia milio ya risasi baada ya bomu lililokuwa ndani ya gari hilo kulipuka.

Maafisa na wale walionusurika wanasema kuwa mlipuaji wa kujitolea muhanga aligongesha gari lililojaa milipuko katika Hoteli ya Asasey katika bandari ya Kismayo kabla ya washambuliaji hao kuvamia jengo hilo.

Vikosi vya usalama vililazimika kukabiliana na wapiganaji waliokuwa na silaha nzito hadi jana asubuhi.

BBC liliandika haijulikana iwapo washambuliaji hao walisalia ndani ya hoteli hiyo baada ya mlipuko huo au la.

Baada ya shambulio hilo wakazi wa mji wa Kismayo wameshuhudia uharibifu mkubwa, huku majengo ya hoteli ya Hoteli ya Asasey na magari yakiwa yameharibika vibaya.

Kwa mujibu wa Afisa wa vikosi vya usalama Mohamed Abdiweli, tayari hali katika hoteli hiyo imedhibitiwa na mmoja wa magaidi katika shambulio hilo alipigwa risasi na kufariki.

Ofisa huyo, alisema huenda idadi ya waliokufa ikaongezeka kutokana na ukubwa wa mlipuko katika shambulio hilo.

Hoteli iliyoshambuliwa ilikuwa na wageni wafanyabiashara na wanasiasa.

Afisa wa usalama wa Somalia, Abdi Dhuhul aliliambia shirika la habari la AFP kwamba waziri mmoja wa utawala wa eneo hilo pamoja na wakili ni miongoni mwa waliofariki.

Kundi la wapiganaji wa al-Shabab liliondoshwa mjini Kismayo 2012 na bandari hiyo imekuwa na amani katika miaka ya hivi karibuni ikilinganishwa na maeneo mengine ya kusini na katikati ya Somalia.

Wapiganaji hao wamekuwa wakitekeleza mashambulio ya mara kwa mara katika mji mkuu wa Mogadishu , licha ya kuwepo kwa idadi kuu ya wanajeshi wa Umoja wa Afrika pamoja na wale wa Somalia waliofunzwa Marekani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles