25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Watanzania watakiwa kutumia Kiswahili

Na RAMADHAN HASSAN, DODOMA

WATANZANIA wametakiwa kukitumia kiswahili kama bidhaa ili kiwasaidie kujikwamua kiuchumi.
Ushauri huo umetolewa jana mjini hapa na Dk. Athumani Ponera kutoka Idara ya Kiswahili ya Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) katika mahafali ya Chama cha Wanafunzi wa Kiswahili Afrika Mashariki (Chawakama), Tawi la St John.

Mahafali hayo yaliyodhaminiwa na Mfuko wa Pensheni wa Watumishi wa Umma (PSPF), yalihusisha pia utoaji wa vyeti kwa wanafunzi waliofanya vizuri katika masomo ya kozi ya Kiswahili chuoni hapo.
“Kiswahili ni bidhaa, lakini wenye bidhaa hawajui kama ni bidhaa ndiyo maana kinaonekana kuwanufaisha watu wengine.

“Ndugu zangu, fursa ya kukitumia kiswahili kama bidhaa ipo kila sehemu, lazima tukitangaze kwa sababu hata Wakenya wanatushinda kukitangaza,” alisema Dk. Ponera.

Wakati huo huo, Dk. Ponera alipokuwa akiwasilisha mada inayohusu Kiswahili na falsafa za ajira, alisema Watanzania wanatakiwa kukitumia Kiswahili katika maeneo mbalimbali ili kiweze kujulikana zaidi.
“Sisi ndio wa kwanza katika Kiswahili na tunatakiwa tukitumie kibiashara na tuwe wa kwanza kunufaika katika kila tunachofanya ila tunaonekana tumedumaa kiakili.

Awali, akisoma risala, Felister Ndolomi, ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa tatu wa kozi ya Kiswahili chuoni hapo, aliiomba Serikali iunge mkono jitihada za Chawakama katika kukuza na kuendeleza kiswahili katika nchi za Afrika Mashariki.

“Changamoto yetu kubwa zinazotukabili ni ukosefu wa kompyuta ya kuhifadhia nyaraka zetu na gharama za usafiri na chakula pindi tunapoenda katika makongamano mbalimbali.

“Kwa hiyo, tunaomba Serikali iangalie namna ya kuzitatua ikiwa ni pamoja na kuangalia jinsi ya kuendeleza Kiswahili katika nchi za Afrika Mashariki,” alisema Ndolomi.

Naye Ofisa Uendeshaji kwa Watumishi wa Umma wa PSPF, Kahenga Maulid, alisema wameamua kudhamini mahafali hayo kutokana na kujua umuhimu wa Kiswahili kwa nchi ya Afrika Mashariki.

“Tumeamua kudhamini kwa kuwa tunajua wahitimu hawa bado wana ndoto kubwa katika maisha yao. Hivyo, kupitia PSPF, ndoto zao zitaweza kutimia kwani pamoja na mkopo wa elimu pia tunatoa mikopo katika ujasiriamali, mafao ya uzazi, mikopo ya viwanja na mikopo ya nyumba zilizojengwa na PSPF,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles