27.5 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Watanzania wanapaswa kuwa makini kuelekea Uchaguzi Mkuu

TAIFA linajiandaa na Uchaguzi Mkuu ambao umepangwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.

Imekuwa ni kawaida nyakati kama hizi za kuelekea Uchaguzi Mkuu, kusikia tambwe za hapa na pale kutoka  kwa wanasiasa wanaotaka kuwania nafasi mbalimbali.

Nyakati kama hizi wale wenye matamanio ya kuwania nafasi hizo, huwa ni waungwana kuliko kipindi chochote kile.

Watu ambao wamekuwa wakifuatilia siasa za hapa nchini watakubaliana nasi kwamba, nyakati kama hizi, wanasiasa ambao walikuwa hawapokei simu za wananchi wao kwa ajili ya kusikiliza kero zao, sasa wanapokea.

Wale ambao walikuwa hawapatikani kwenye vikao vya kutatua kero za mitaa, kata, vijiji au vitongoji  sasa wanapatikana kuliko ilivyokuwa mwanzo.

Ni nyakati kama hizi wananchi hushuhudia misaada mingi ya hali na mali kuliko wakati mwingine wowote.

Si tu misaada pia nyakati kama hizi hushuhudia utekelezaji wa ahadi kemkem na wakati mwingine sio ahadi bali zile kero ambazo zinaonekana zitakuwa kikwazo wakati wa Uchaguzi Mkuu.

Wanapofanya hayo sasa kwa baadhi ni rahisi kuonekana wanajali, wanatekeleza ahadi au wanawapenda sana wananchi.

Wananchi wengi  si kwamba ni wasahaulifu hapana la hasha! Wanashindwa kufanya uchambuzi rahisi kwamba kipindi hiki kikipita wale wanaopatikana na kupeleka misaada hawataonekana tena kwa muda fulani baada ya kushinda mioyo yao.

Tumelazimika kuandika jambo hili sasa kukumbusha wananchi na hasa wale wapiga kura kuwa macho katika kipindi hiki dhidi ya wale wanaopita kuwahadaa ilihali wana sifa za ovyo ili wawachague wakati wa Uchaguzi Mkuu.

Watanzania wanapaswa kutokubali kuchaguliwa au kufanyiwa tathimini na vyama siasa juu ya wagombea wanaowataka na wenye sifa zinazostahili za kuweza kuivusha nchi hatua nyingine mbele.

Wagombea wenye sifa za ovyo ikiwemo kashfa  kuwanyanyasa, kuuza ardhi za wananchi na wenye mwenendo isioaminika, wachumia tumbo hawa hawapaswi kupewa nafasi wala kufikiriwa katika wakati huu hata kama watajipitisha na kutoa misaada mingi kiasi gani.

Tunawaasa Watanzania kuanza kuwaangalia kwa mapana viongozi wa kuwachagua ambao watakuwa na sifa zinazostahili.

Watanzania wanapaswa kutambua kwamba mustakabali wa taifa uko mikononi mwao, hivyo uamuzi wowote ambao wataufanya sasa au baadae wajue utakuwa na athari huko tunakoelekea.

Wafanye hivyo wakitambua kwamba Tanzania bado ni taifa maskini linalokabiliwa na changamoto lukuki kama uhaba wa makazi bora, dawa, barabara na vingine vingi.

Kwa sababu hiyo ndio maana sisi tunaona wananchi wanahitaji kuanza kuwatupia jicho wale wenye maono ya kuitoa nchi ilipo na si wale wachumia tumbo ambao wanaishia kujipitisha na kutoa tumisaada nyakati kama hizi za kuelekea Uchaguzi Mkuu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles