26.9 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

WATANZANIA WAKAMATWA WAKIENDA KUJIUNGA AL-SHABAAB

Na MWANDISHI WETU-KENYA


WAPELELEZI wa Kikosi cha Polisi cha Kupambana na Ugaidi (ATPU) cha hapa, wamewakamata Watanzania wawili wanaotuhumiwa walikuwa safarini kwenda nchini Somalia kujiunga na kundi la kigaidi la Al-Shabaab.

Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Isiolo, Charles Ontita, jana alisema Watanzania hao; Omar Mwalimu Kasambe maarufu kama Juma Abbas Zuberi (28) na Ali Juma Kaondo (17), walikamatwa na wapelelezi wa kikosi hicho katika Barabara ya Isiolo-Moyale karibu na makutano ya barabara za Garba na Tula.

‘‘Maofisa waliokuwa katika doria walisimamisha basi lililokuwa likielekea Moyale kutoka Nairobi na kuwakuta wageni wawili wasio na hati halali za kusafiria,’’ alisema Ontita.

Watanzania hao waliwaambia wapelelezi kuwa walikuwa wakisafiri kwenda Moyale kufanya kazi za uchungaji walizokuwa wameahidiwa.

Wakiwa hawajaridhishwa na maelezo yao, askari wakaanza kuwapekua simu zao za mkononi na kukuta mawasiliano kadhaa na simu za Somalia.

‘‘Washukiwa waliwaambia maofisa wa polisi kuwa namba hizo za Somalia zilikuwa za watu waliowasiliana nao kuhusu ofa hiyo ya kazi,’’ alisema.

Ontita alisema Watanzania hao walikamatwa na kupelekwa Kituo cha Polisi cha Isiolo.

Alisema uchunguzi wa suala hilo ambao pia utahusisha wapelelezi wa ATPU kutoka Nairobi na vyombo vingine vya usalama umeshaanza.

MTANZANIA ilimpomtafuta Msemaji wa Serikali wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mindi Kasiga ili kupata ufafanuzi kama Serikali imepokea taarifa za kukamatwa kwa Watanzania hao, simu yake iliita muda mrefu bila kupokewa.

Machi 31, 2015 Mtanzania mwingine, Ummul-Khayr Sadir Abdul (19), alikamatwa kwa ugaidi nchini Kenya katika Jimbo la El -Wak, mpakani mwa Kenya na Somalia.

Vyombo vya usalama nchini Kenya, vilieleza kuwashikilia wasichana watatu akiwamo Ummul-Khayr, kwa kile kinachodaiwa kutaka kujiunga na Al-Shabaab huko Somalia.

Kamishna wa Polisi Jimbo la El -Wak, mpakani mwa Kenya na Somalia, Nelson Marwa, alieleza kuwa Ummul-Khayr, alijieleza kuwa ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Afrika nchini Sudan.

Mtanzania huyo, mwenyeji wa Zanzibar, anatajwa kuwa kiongozi wa kundi hilo lililopanga kujiunga na Al-Shabaab.

Wasichana wengine waliokamatwa pamoja na Ummul-Khayr, ni Maryam Said Aboud na Khadija Abubakar Abdulkadir wote raia wa Kenya.

Tukio jingine lilitokea Aprili 10, mwaka huu wakati Mtanzania mwingine, Rashid Charles Mberesero, alipofikishwa mahakamani na kuwekwa kizuizini kwa mwezi mmoja, polisi wakiendelea kukusanya ushahidi dhidi yake.

Mtuhumiwa huyo ambaye pia anafahamika kwa jina la Rehani Dida, alirejeshwa Nairobi kutoka Garissa alikopelekwa awali kuhojiwa baada ya kukiri kujihusisha na Al-Shabaab.

Mahakama jijini Nairobi ilisema kuwa mtuhumiwa huyo ambaye hakutakiwa kujibu tuhuma hizo na wenzake wanne, watalazimika kuwa chini ya uchunguzi mkali wa polisi kwa kipindi cha mwezi mmoja na baadaye wanaweza kusomewa mashtaka ya kuhusika katika shambulizi hilo lililoua watu hao, wengi wao wakiwa ni wanafunzi.

Mwendesha Mashtaka, Daniel Karuri, aliiambia mahakama kuwa Mtanzania huyo ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha tano, alikuwa amepanga safari ya kuelekea Somalia kujiunga na makundi ya kigaidi.

Karuri aliiambia mahakama hiyo kuwa polisi walikuwa wakifuatilia kwa karibu uhusiano baina ya wale waliofanya shambulizi hilo na mfanyabiashara mmoja anayemiliki hoteli mjini Garissa, na inasemekana kuwa watu hao waliotekeleza shambulio hilo, walikuwa wamelala katika hoteli hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles