30.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

WATANZANIA WAKAMATWA NA DAWA ZA KULEVYA SWAZILAND

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM

WATANZANIA watatu wamekamatwa nchini Swaziland wakisafirisha kilo 30 za dawa za kulevya aina ya heroin.

Akizungumza jana, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Rogers Siyanga, alisema dawa hizo zilikuwa zikisafirishwa kuelekea Afrika Kusini.

Aliwataja watu hao kuwa ni Issa Rashid Ally (39), Chande Ally Chande (32) na Mohamed Nasser Katala (37).

“Tunafuatilia taarifa hizi na tunashirikiana na wenzetu wa Afrika Kusini. Taarifa za kiuchunguzi zinaonyesha dawa hizi zilikuwa zinasafirishwa kutoka Msumbiji kuelekea Afrika Kusini, na baada ya kuimarisha operesheni hapa kwetu watu wengi wamekimbilia Msumbiji.

“Kuna watu maalumu ambao kazi yao ni kutafuta vijana na kuwarubuni kwamba watakwenda kuwatafutia maisha lakini huanza kwa kuwabebesha mizigo ya dawa za kulevya,” alisema Siyanga.

Taarifa kutoka Swaziland zinaeleza kuwa tayari Watanzania hao wamefikishwa mahakamani.

MAREKEBISHO YA SHERIA

Kamishna Siyanga alisema wanatarajia kuwa ndani ya siku 21 marekebisho ya Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya yaliyopitishwa na Bunge wiki iliyopita yatafikishwa kwa Rais Dk. John Magufuli.

Alisema sheria hiyo imelenga maeneo muhimu 16 na kwamba inatarajiwa kuanza kutumika rasmi baada ya kusainiwa na Rais.

“Marekebisho ya sheria hii yamelenga kuipa uwezo mamlaka kushughulikia pia makosa mengine yenye uhusiano wa moja kwa moja na biashara na matumizi ya dawa za kulevya.

“Marekebisho yanaipa nguvu mamlaka ya kupata taarifa muhimu kutoka vyanzo mbalimbali na ni kosa kwa mkuu wa taasisi au mtu anayehusika kutotoa taarifa endapo atatakiwa kufanya hivyo,” alisema Kamishna Siyanga.

Alisema marekebisho hayo ya sheria yameongeza fursa kwa watumiaji kupata matibabu na huduma nyingine badala ya kuhukumiwa kifungo gerezani.

Alisema mamlaka ina divisheni ya kinga na tiba inayoratibu jukumu la matibabu kwa watumiaji wa dawa za kulevya badala ya kukimbilia adhabu ya kifungo kwa sababu nao ni wagonjwa kama wengine.

“Kupitia marekebisho haya sasa mamlaka itakuwa inafanya uchunguzi wa sampuli za vielelezo vinavyokamatwa na kuharakisha upelelezi wa mashauri ili yasikilizwe na kumalizika mapema,” alisema.

Naye Kamishna wa Sheria, Edwin Kakolari, alisema sheria inaipa uwezo mamlaka kushikilia akaunti za benki za watuhumiwa kwa muda ili kuiwezesha mamlaka kupambana na fedha haramu zinazotokana na biashara ya dawa za kulevya zilizoko kwenye mzunguko.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles