25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

WATAFUNA NCHI WATADHIBITIWA KWA MWENDOKASI?

valentino-mlowa

Na Dennis Luambano, Dar es Salaam

HAKUNA ziada mbovu. Kwa sababu watu mbalimbali wakiwamo wanaharakati na wanasiasa wamepaza sauti zao na kuelezea namna wajanja wachache wanavyojitajirisha kwa njia za panya.

Wameshazungumza mara chungu nzima na hawachoki kuzungumzia ujanja/ufisadi unaofanywa katika sekta mbalimbali.

Licha ya wao kupaza sauti lakini hakukatazi au hakuwafungi wengine kufanya uchambuzi wa matukio yanayotokea sasa hivi kwa kufuata misingi ya kwanini, wapi, kivipi, nani na lini kama muongozo wa safu hii ya kisa mkasa unavyosema.

Kama hivyo ndivyo, ndiyo maana nimesema hakuna ziada mbovu na kwa maana nitakachojadili leo si ziada mbovu.

Mathalani ripoti ya mwaka wa fedha unaoishia Juni 30, mwaka juzi iliyotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad, ilionyesha namna baadhi ya watumishi wanavyoendelea kuneemeka kutokana na uhodari wao wa kutafuna fedha za umma.

Ripoti hiyo ilionyesha uhodari huo baada ya kutafuna Sh bilioni 144.4 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.

Pia katika ripoti aliyoitoa bungeni Aprili, mwaka huu ya mwaka wa fedha wa 2014/ 2015, CAG ameibua uozo mwingine baada ya watumishi kuendelea kutafuna fedha katika halmashauri, taasisi za Serikali na mashirika ya umma.

Wakati Serikali ya Rais Dk. John Magufuli haijaanza kuwashughulikia waliotajwa na CAG katika ripoti yake ya mwaka 2014/2015, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), iliibuka na kumtaja mfanyabiashara mmoja kuwa ndiye kinara wa kutengeneza stakabadhi za kielektroniki kupitia mashine za EFD’s.

Kuibuka kwa Takukuru kulikuja siku moja baada ya Magufuli kueleza kuwa mfanyabiashara mwenye asili ya Asia amekuwa akifanya miamala ya fedha inayofikia Sh milioni saba hadi nane kwa kila dakika moja.

Pia Takukuru ilibaini zaidi ya kampuni 300 zinahusika katika mpango huo kutafuna fedha za Serikali na kwa pamoja zilitakiwa kulipa zaidi ya Sh bilioni 30, zinazoelezwa kuibwa kupitia mchezo wa kudurufu stakabadhi bandia zenye nembo ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Kwa pamoja, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Valentino Mlowola na Kamishna Mkuu wa TRA, Alphayo Kidata, walieleza jinsi Serikali ilivyoibiwa kupitia stakabadhi za EFD’s.

Kwamba kampuni hizo zilikuwa zikinunua stakabadhi za manunuzi bandia kutoka kwa watu wanaomiliki EFD’s ambazo hazijasajiliwa na kuzitumia na kisha kudai marejesho ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) bila kuwapo na bidhaa au stakabadhi halali iliyouzwa na muhusika.

Mchezo huo umesababisha ukwepaji kodi tangu mwaka 2010 hadi 2014 na kupoteza mapato ya Serikali kiasi cha Sh bilioni 29.2.

Huo ndiyo ukweli wa mambo. Lakini je, wanaotafuna fedha hizo watadhibitiwa kwa mtindo wa mwendokasi? Hata hivyo, sitaki kuamini kwamba kutakuwa na kigugumizi cha kuwashughulikia wanaotafuna fedha za umma. Kwamba zile lugha eti wako katika mikono salama au wanatakiwa kurejesha fedha walizoiba hazina tena nafasi.

Kwamba tunataka adhabu watakazopewa zifanane na makosa waliyofanya.

Kwa sababu vitendo vya kina Mohammed vinaakisi namna mtandao wa wajanja wachache ambao miongoni mwao ni baadhi ya wafanyabiashara wakubwa wanaoshirikiana na watumishi wa umma wasio waadilifu wanavyozidi kujiimarisha katika mamlaka za Serikali ili kuiba fedha.

Kitendo cha mtandao huo kuendelea kujiimarisha katika mamlaka hizo nyeti kama TRA huwa kinanipa maswali pasipo kupata majawabu kwamba je, ni dalili mojawapo kuwa umeshindwa kudhibitiwa au utakuja kudhibibitiwa kwa mwendokasi kama nilivyosema hapo juu?

Je, ni kweli tafsiri nyingine ya kushindwa uko kunatokana na ukweli kwamba mtandao huo umewazidi nguvu wale walio juu ya mamlaka hizo? Sitaki kuamini hivyo.

Je, ni kweli kwamba pengine sababu kubwa inayowazidi nguvu inatokana na ushawishi wa fedha waliyonayo wanapowahadaa baadhi ya watumishi hao na kuwafanya watoe uamuzi ili kuwanufaisha wao kwa maslahi yao binafsi.

Kwamba wanaotafuna fedha za Serikali wataendelea kuneemeka kwa njia ya kutoa malipo bila nyaraka, kutumia fedha nje ya bajeti na kutoa malipo bila idhini ya ofisa masuhuli wameshindikana. La hasha!

Licha ya kutoamini huko lakini pia najiuliza iweje kila mwaka wanaotafuna fedha hizo wanashindwa kudhibitiwa?

Yaani iweje kila mwaka kuwe na watumishi hewa wanaoendelea kulipwa mishahara, iweje watumishi walishafariki dunia, waliacha kazi au kufukuzwa miaka chungu nzima iliyopita lakini hadi leo bado wanaendelea kulipwa kupitia akaunti zao?

Hapa sasa ndipo kunatia shaka na kunasababisha kujiuliza kulikoni serikalini? Au kuna haja ya kurejea kauli ya Magufuli kwamba alikuta uozo mwingi serikalini.

Au pengine kuna mtandao unaohusisha watendaji nyeti serikalini ndiyo maana ubadhirifu umeshindwa kutomezwa kabisa licha ya kupungua kwa kasi ndogo?

Kimsingi, nina maswali mengi kuliko majibu. Kwamba labda mtandao huo unaohusisha watendaji nyeti serikalini ndiyo unaowapa kiburi watu hao kuendelea kutafuna fedha za umma kila mwaka kwa kuwa wanaamini hakuna hatua yoyote itakayochukuliwa dhidi yao kwa sababu tu huwa wanagawana fedha hizo.

Wakati nikiendelea kuhoji hivyo pia nampongeza Magufuli kwa juhudi zake alizofanya na anazoendelea kuzifanya za kuwadhibiti wanaotafuna fedha hizo kwa kuagiza wachukuliwe hatua kali za kisheria.

Namuomba Magufuli akiagize kikosi kazi chake kinachowashughulikia wanaotafuna fedha hizo waongeze kasi ya kuwafikisha katika vyombo vya sheria maana fedha walizotafuna ni nyingi na zingeweza kutengeneza au kuboresha miradi ya kimaendeleo katika maeneo mbalimbali.

Pia namuomba akiagize kikosi hicho kifanye kazi kwa njia za kisasa ili kuwadhibiti au kuwatokomeza kabisa wanaotafuna fedha hizo kwa sababu wanaonekana ni weledi kwa kuwa kila mwaka wanabadilisha mbinu na ushahidi wa weledi wao ni taarifa ya kiasi cha fedha za Serikali walizotafuna.

Nihitimishe kisa mkasa hiki kwa kusema kwamba vitendo vinavyofanywa na wafanyabiashara kama kina Mohammed kwa kushirikiana na watumishi wa umma wasio waadilifu vinatonesha majeraha ya vidonda vya watu wachache kuendelea kufaidi fedha za Serikali kwa njia ovu.

Kwamba wakati baadhi ya wanafunzi wa wanakaa chini kwa kukosa madawati au wazee wanashindwa kupewa dawa bure katika hospitali za Serikali kumbe kina Mohammed na watumishi wachache wanafaidika kwa kuiibia Serikali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles