26.9 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

WASIRA: SIASA ZA CHUKI NA VISASI HAZIFAI

NA ELIZABETH HOMBO

JUMAMOSI iliyopita Oktoba 14 mwaka huu, Taifa liliadhimisha miaka 18 ya kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, ambapo maadhimisho yake ambayo huambatana na Siku ya kuzima Mwenge wa Uhuru yalifanyika visiwani Zanzibar.

Kutokana na hilo, gazeti hili limefanya mahojiano na mwanasiasa mkongwe, Stephen Wasira ambaye alihudumu kwenye uongozi tangu wakati wa Mwalimu Nyerere akishika nyadhifa mbalimbali ndani ya chama na Serikali.

Wasira mwenye historia ndefu katika siasa, alipata kugombea urais ndani ya CCM katika uchaguzi uliopita lakini hakupitishwa na chama chake na baadaye akarudi kugombea jimboni kwake Bunda lakini akashindwa na Esther Bulaya wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Katika mahojiano yake na MTANZANIA kwa njia ya simu akiwa  Marekani, pamoja na mambo mengine anaelezea vikwazo ambavyo vinahatarisha umoja alioasisi Mwalimu Nyerere.

MTANZANIA: Unaizungumziaje miaka 18 bila Mwalimu Nyerere

WASIRA: Ili kujua miaka 18 bila Mwalimu Nyerere, lazima tujue kwamba alisimamia nini, alitaka nchi ya aina gani na lazima tukumbuke mambo makubwa aliyoyafanya.

Katika hilo, Mwalimu Nyerere alifanya mambo makubwa mawili; kwanza alikuwa ‘champion’ wa kudai uhuru ndiyo maana akapigania uhuru na aliamini kwamba hakuna maendeleo bila uhuru.

Pili ni Umoja; alitumia misingi gani kujenga Tanzania, bila Mwalimu hali ingekuwaje? Na sasa tuko huru kama tulivyokuwa tumekusudia?

MTANZANIA: Unadhani bado tuko huru?

WASIRA: Tuko huru lakini bado kuna kazi ya kufanya kwa sababu kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni, asilimia 33 ya Watanzania ni maskini. Kuwa na uhuru lakini kuna umaskini hiyo ni ‘problem’.

Mwaka 1962, Mwalimu Nyerere alitaja maadui watatu kuwa ni umaskini, ujinga na maradhi, sasa bila kuondoa hivyo vikwazo unaweza kupoteza uhuru kwa sababu tuna watu ambao hawajitegemei na uhuru unaweza kununuliwa kwa vile watu hawajitegemei.

MTANZANIA: Kwa mtazamo wako, unadhani miaka 18 bila mwalimu umoja bado upo?

WASIRA: Mimi naamini umoja bado upo lakini kuna matatizo katika umoja wetu.

MTANZANIA: Pengine ni matatizo gani hayo?

WASIRA: Matatizo ambayo yamejitokeza hivi sasa ni kwamba watu wameanza kuzungumza juu ya ukanda, ukabila.

Wakati wa Mwalimu Nyerere haya hayakuwapo, alipinga mambo hayo ndiyo maana alianzisha nchi ya kipekee na hatukuwachagua viongozi wetu kwa kulingana na ukabila.

Tukianza kuzungumza ukabila na ukanda pamoja na walionacho na wasionacho tutaathiri umoja na baadaye amani itapotea.

MTANZANIA: Tabaka la walionacho na wasionacho, litaathiri vipi umoja?

WASIRA: Kuna tofauti za mapato, watu ni maskini kupindukia huku wachache wakiwa na kipato kikubwa.

MTANZANIA: Unadhani nini kifanyike ili kusiwe na hali hiyo?

WASIRA: Asilimia 75 ya Watanzania wanajishughulisha na kilimo, hivyo rasilimali zielekezwe kuwasaidia wakulima na wafugaji.

Viwanda viwasaidie watu wote mfano korosho, pamba, mahindi, viwanda vya kusaga unga na kusafirisha iwahusishe wananchi.

MTANZANIA: Unadhani yale aliyoyaasisi Mwalimu Nyerere, bado yanaishi?

WASIRA: Iko tofauti kati ya kuishi na kutenda. Fikra haziwezi kufa, wapo watu wanasema ujamaa umekufa. Ni fikra na hazifi na ndiyo maana kila tukio au jambo lolote wanamkumbuka Mwalimu.

Hivi sasa hata ukifuatilia mitandao ya kijamii utaona namna watu wengi wanavyomuenzi.

MTANZANIA: Kwa maoni yako unadhani uongozi wa sasa unayaenzi yale aliyoasisi Mwalimu Nyerere?

WASIRA: Wanajitahidi. Ni kukumbushia tu lakini si kulaumu…kulaumu ni rahisi kuliko kusolve matatizo ya Taifa letu na hakuna kiongozi ambaye atasolve matatizo yetu yote.

MTANZANIA: Ulipata kufanya kazi pamoja na Mwalimu Nyerere, pengine ni jambo gani ambalo hutalisahau?

WASIRA: Ninapomkumbuka Mwalimu Nyerere kama kiongozi wa Taifa, mimi ninamkumbuka kama Baba yangu, mlezi wangu.

Yeye ndiye aliyenifanya nisome digirii mbili katika Chuo Kikuu cha Amerika. Ikiwa kama kumbukumbu yake nikiwa huku Marekani, nimekitembelea kile chuo.

MTANZANIA: Unauzungumziaje uongozi wa bsasa ukilinganisha na awamu zilizopita?

WASIRA: Haiwezekani watu wote wawe na mtazamo sawa. Kuna siku niliulizwa swali kama hilo kuwa nimefanya kazi karibu na viongozi wote, nikaulizwa nani kafanana na nani na mimi nikasema hakuna anayefanana na mwingine.

Nikimaanisha kwamba kila kiongozi ana style yake ya kuongoza. JK (Jakaya Kikwete) alikuwa anapenda kushirikisha watu wote anaopingana nao, alikuwa akiwakaribisha wapinzani wake lakini pamoja na yote hayo alitukanwa, aliitwa dhaifu.

Amekuja JPM (Rais John Magufuli) wanasema ni mkali mara dikteta, lakini aliyekuwa mpole, msikilizaji wa maoni yao ni dhaifu. JPM anayesimamia misingi anayoiamini yeye wanasema ni dikteta…Kikwete aliwapa uhuru mwingi sana.

Rais kama kiongozi wetu ana wajibu wa kuwasikiliza wananchi wake na pale malalamiko yanapozidi lazima awasikilize na si lazima akakubaliana na kila kinachosemwa lakini ni wajibu wake kusikiliza.

Kwa kusikiliza wanachokisema anaweza kupata ukweli na uongo…atatofautisha pumba na mchele na katika kuwasikiliza anaweza akaujua ukweli ambao alikuwa haufahamu.

MTANZANIA: Nini mtazamo wako kuhusiana na viongozi wa vyama vya siasa wanaokamatwa na vyombo vya dola pale wanapoikosoa Serikali?

WASIRA: Akikamatwa si atakwenda mahakamani na baadaye mahakama itasema kama kuna kesi au laa.

Sasa Jeshi la Polisi pale linapoendelea kukamata watu wanaoikosoa Serikali na mahakama inapotoa uamuzi kuwa hakuna kesi, baadaye watapunguza ukamataji wa aina hiyo watawakamata wale wenye makosa tu.

MTANZANIA: Pengine nini ushauri wako kwa vyombo vya dola kuhusiana na hilo?

WASIRA: Lifanye kazi yake kwa uangalifu katika kukamata…sasa huwezi kusema marufuku kukamata, utaonekana wa ajabu. Lakini si jambo zuri kukamata bila makosa.

Ushauri wangu kwao; waendelee na kazi lakini wasikamate wasiokuwa na hatia.

Lakini jambo lingine nililotaka kulisema ni kwamba wakati mwingine tunaiga nchi zingine. Kwa mfano hapa Marekani hawaandamani kila mara, wanaandamana pale ambapo kuna kitu kinawakera.

Sasa nchini kwetu, mtu anatangaza eti atafanya maandamano yasiyo na kikomo sasa mtakula kikomo? Nchi zingine za wenzetu kama Ujerumani huwa wanaandamana siku ya Jumamosi na Jumapili lakini siku za kazi huwa hawaandamani.

MTANZANIA: Unazungumziaje tukio la kupigwa risasi Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu?

WASIRA: Watu wote tunaopenda amani, tunasikitishwa na tukio la Lissu. Ni tukio la kulaaniwa na wapenda amani wote.

Tukio la Lissu ni baya sana… tunasikitishwa, tunalipinga na kulilaani. Tunataka siasa ziendeshwe kwa hoja na hoja zijibiwe kwa hoja…tupingane kwa hoja.

Kutoa roho za watu na kukatisha maisha ya mtu hiyo si siasa, siasa za chuki na visasi hazipendezi, mauaji ni hatua ya juu kabisa ya visasi…haifai.

Mambo haya tulikuwa tunayasikia nchi zingine na tusiige mambo hayo, hatuyakubali kabisa. Hatutaki tena yatokee katika nchi yetu ambayo imesifika kwa amani kwa muda mrefu.

Jeshi la Polisi lina wajibu wa kujua watu hao waliofanya kitendo hicho kibaya ili kuwaondolea wananchi hofu. Lazima watoe taarifa za wahalifu wa matukio ya aina hii, isifike hatua watu wakaogopa katika nchi ambayo waasisi wetu walihangaika kuwa nchi ya mfano kwa amani na utulivu.

Na katika mazingira kama hayo, watu wabaya wanaweza wakaingia katikati kwa lengo la kuichonganisha Serikali na wananchi.

Watu wabaya wapo duniani; yaani kama Polisi haiwachukulii hatua wahalifu, watu hao wabaya wanaweza wakampiga Lissu na baadaye wakasema Serikali imefanya hivyo…sasa Jeshi letu la polisi lina wajibu wa kujua haya yanayoendelea.

MTANZANIA: Unayazungumziaje matukio mengine yenye sura kama hiyo, mfano kuhusu miili ya watu walioopolewa baharini?

WASIRA: Hayakubaliki kabisa ni kama nilivyosema hapo awali kwamba Jeshi la Polisi lina wajibu wa kulinda amani na utulivu pamoja na mali za watu, hivyo lina wajibu wa kutoa taarifa na kuwahakikishia amani Watanzania.

MTANZANIA: Ulikuwa mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba ambayo iliandaa Katiba Inayopendekezwa, unadhani kuna umuhimu wa Katiba Mpya kwa sasa?

WASIRA: Yapo mambo yanaenda kwa mahitaji ya wakati na kipaumbele cha Serikali. Rais Magufuli wakati analihutubia Bunge alisema amerithi kiporo cha Katiba Mpya, hivyo atalishughulikia kwa wakati.

Hivyo ni suala la wakati ambao Serikali imeona itafaa, lakini huwezi kusema haina mpango nao wakati tulikaa siku 120 kuandika Katiba Inayopendekezwa hivyo ghafla tu huwezi ukaibuka ukasema haihitajiki isipokuwa ni siku ya kuliendeleza.

Tunahitaji Katiba Mpya, maji, chakula, zote zinatokana na rasilimali, hivyo kupanga ni kuchagua.

MTANZANIA: Una maoni gani juu ya hatua ya Mbunge wa Chemba, Juma Nkamia kutaka kupeleka hoja binafsi bungeni ya kuongezwa miaka saba ya uchaguzi.

WASIRA: Bora umeniuliza hilo swali maana nilitaka niliseme. Huyu Nkamia amenishangaza sana, sijui ametoa wapi hiyo hoja ambayo haina manufaa kwa wananchi.

Anaitaka miaka saba ya nini? Maana kang’ang’ania saba, saba ili iweje! Mimi hata simwelewi sijui anataka ya nini na tayari nilimpigia simu nilimweleza kuhusu hiyo hoja yake, kwamba haina manufaa kwa Watanzania.

Katiba huwa inaamsha hisia za watu, atueleze miaka saba ya nini na hiyo mitano amefanya nini? Watanzania waulizwe…hamuwezi kubadili katikati ya mchezo haiwezekani kabisa. Tuzungumze Katiba kwa ujumla.

MTANZANIA: Hivi karibuni wakati akihojiwa na kituo kimoja cha redio, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole alisema hivi sasa chama hicho kitawapitisha wagombea ubunge ambao ni wakazi wa eneo husika, una maoni gani kuhusiana na hili?

WASIRA: Hilo ni jambo la kikatiba na kisheria. Kama Polepole amelisema litakuja katika vikao vya chama, tutalizungumza. Mimi nimeliona kwenye mitandao tu hivyo siwezi kutoa maoni kwa sasa, nasubiri lije kwenye vikao na mimi ni mjumbe wa Kamati Kuu ya chama.

MTANZANIA: Baada ya kushindwa ubunge katika uchaguzi mkuu uliopita, Je, bado una nia hiyo kwa siku zijazo?

WASIRA: Mwaka 2020 sina mpango wa kugombea,  Kwa sasa nagombea vyeo ndani ya CCM mfano nagombea mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), wanachama wenzangu wakinipitisha sawa.

MTANZANIA: Hivi sasa unajishughulisha na nini?

WASIRA: (Anacheka). Nabangaiza kama Watanzania wengine kwa mfano biashara ndogo ndogo, kulima kidogo. Lakini kwa sasa nipo huku Marekani nimekuja kuwatembelea wanangu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles