26.9 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Wasionyonyesha watoto hatarini kupata saratani ya matiti

NYONYESHA

Na Veronica Romwald, Dar es Salaam

WANAWAKE wanaotumia sindano za kukausha maziwa  kukwepa kunyonyesha watoto wakihofia kuanguka  maziwa na kunenepa mwili, wapo katika hatari  ya kupata saratani ya matiti.

Hayo yalielezwa mwishoni mwa wiki na Mtaalamu wa Masuala ya Lishe wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Ulumbi Kilimba alipozungumza na MTANZANIA katika mahojiano maalumu.

Mahojiano hayo yalijikita zaidi katika kuelekea maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji yanayotarajiwa kufanyika Agosti mosi hadi 7, mwaka huu, ambayo yamepewa kauli mbiu isemayo ‘Unyonyeshaji ni ufunguo wa maendeleo endelevu’.

“Wanawake wengi wa miaka ya sasa wamekuwa wakikwepa kunyonyesha watoto wao eti wanaogopa kunenepa na maziwa yao kudondoka, kwamba hali hiyo itasababisha waachwe na waume zao.

“Hii ni changamoto mojawapo inayosababishwa na utandawazi… umesababisha wengi wao kujifunza mbinu zisizofaa ikiwamo hiyo ya kujidunga sindano kukausha maziwa   wakwepe kuwanyonyesha watoto wao.

“Kitendo cha kuyazuia maziwa ambayo ndicho chakula pekee anachopaswa kupewa mtoto katika miezi sita ya ukuaji wake baada ya kuzaliwa ni cha hatari kwa afya ya mama husika,” alisema.

Kilimba alisema maziwa yanapozuiwa kutoka nje huchochea kwa asilimia kubwa mwili wa mama anayepaswa kunyonyesha, kutengeneza chembechembe ambazo baadaye husababisha saratani ya matiti.

“Maziwa yameumbwa na Mungu kwa ajili ya   kutumika baadaye katika kumnyonyesha mtoto. Sasa wapo  kina mama ambao hawataki kunyonyesha.

“…Kwamba watanenepa mno na maziwa yao yatadondoka… hivyo watapoteza umbo la mvuto ambalo wanaume wengi ndilo wanalolipenda.

“Na kwa sababu watapoteza umbo hilo la mvuto matokeo yake ni kwamba wanaume zao watakwenda kuoa wadada wengine warembo!” alisema.

Mtaalamu huyo alisema   mawazo hayo si sahihi kwa sababu  iwapo mwanamke atamnyonyesha mtoto wake kwa kuzingatia maelekezo anayopewa na mtaalamu wa afya hawezi kupoteza umbo lake la mvuto.

“Ni kweli mama anayenyoshesha anapaswa kula chakula cha kutosha   kusaidia kutengeneza maziwa ya kumlisha mtoto wake, lakini wakati wa kunyonyesha kuna maelekezo tunawapa, wanapaswa kuyazingatia.

“Kama wakiyazingatia, atamnyonyesha mtoto wake vizuri, atanenepa na tena wengine wanaofuata ushauri huo inawasaidia hadi kushiriki tendo la ndoa bila kutumia njia za uzazi wa mpango kwa kipindi kadhaa cha hatua ya unyonyeshaji,” alisema.

Alisema mbali na kina mama hao ambao huzuia maziwa kutoka, wapo wengine ambao hutumia vipodozi vyenye kemikali kali wakati wa kunyonyesha hali ambayo inahatarisha afya zao na watoto wao bila kujijua.

“Ni vizuri mwanamke anayejiandaa kushika mimba kuacha kutumia vipodozi vikali miezi mitatu kabla na katika kipindi chote cha kunyonyesha.

“Maana kemikali huenda kwenye maziwa na matokeo yake watoto wananyonya sumu badala ya maziwa na ndiyo maana siku hizi wengi wanakutwa na saratani mbalimbali,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles