Imechapishwa: Tue, Sep 19th, 2017

WASHEREHESHAJI WAPATA MAFUNZO TRA, KULIPA KODI KARIBUNI

Na KOKU DAVID

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), imeendelea na mikakati yake ya  kuhakikisha inapanua wigo wa upatikanaji mapato kwa kuongeza walipakodi wenye sifa za kulipa kodi kwa mujibu wa sheria.

Hivi karibuni Mamlaka hiyo ilikutana na Umoja wa Wakali wa Sherehe Bongo (WSB) jijini Dar es Salaam, lengo likiwa ni kuwapa elimu mbalimbali inayohusiana na masuala ya kodi.

Umoja huo wa WSB unajumuisha washereheshaji katika maharusi (MC), wapishi, wapambaji, wapigapicha pamoja na wapigaji wa muziki (DJs).

Ni mara ya pili kwa mamlaka hiyo kukutana na kundi hilo ambalo kwa mujibu wa sheria linatakiwa kuingia katika kundi la walipakodi.

Katika mkutano huo, TRA iliahidi kukutana na kundi hilo mara kwa mara ili kuweza kuwaelimisha kuhusiana na umuhimu wa kulipa kodi ambayo ndiyo itakayoisaidia Serikali kutekeleza majukumu yake katika jamii.

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo, anasema WSB iliiomba mamlaka hiyo kukutana nao kwa ajili ya kuwapa elimu ya kodi, kuwaelekeza namna ambavyo wanaweza kusajiliwa.

Sambamba na hayo, pia waliwafundisha namna ambavyo watakuwa wakilipa kodi na kwamba baada ya elimu hiyo wameonyesha utayari wa kulipa kodi kama sheria inavyowataka kufanya.

Anasema TRA imepewa jukumu la kuhakikisha linatekeleza wajibu wake kwa kuwaingiza katika wigo wa kodi wafanyabiashara kama ambavyo sheria ya fedha ya mwaka 2017 inavyoelekeza kuwa kila mfanyabiashara anayefanya biashara ambayo si rasmi anatakiwa kurasimishwa aweze kuingia katika wigo wa kodi ili alipe kodi.

Kayombo anasema hivi sasa mamlaka hiyo inafanya utaratibu wa kuhakikisha wanarasimisha wafanyabiashara ambao biashara zao si rasmi na kwamba wamelitaka kundi la WSB kufika katika ofisi za TRA kupewa maelekezo na kusajiliwa na kuwa miongoni mwa walipakodi wanaotambuliwa kisheria.

Anasema katika mafunzo waliyowapa, wamewaelimisha kuhusu umuhimu wa mashine za kielektroniki za kodi (EFDs) na ni mfanyabiashara yupi anatakiwa kutumia mashine hiyo katika biashara zake ikiwa ni pamoja na namna zinavyotumika na zinapopatikana.

Anasema pamoja na mafunzo, wamejadili changamoto mbalimbali wanazokutana nazo katika kazi zao na kuahidi kushirikiana ili kuhakikisha wanaziondoa.

Anasema ili kuweza kufanya nao kazi kwa urahisi pamoja na kutatua changamoto, wanatakiwa kuwa katika umoja unaotambulika ambao utaiwezesha mamlaka hiyo kuwafikia.

Anaongeza pia wamepokea mapendekezo kutoka kwa kundi hilo la WSB ambalo pamoja na kuomba kupatiwa elimu lilikuwa linazinduliwa kwa mara ya kwanza ili liweze kutambuliwa na mamlaka hiyo liweze kuingia katika wigo wa kodi.

Anasema pamoja na kupokea mapendekezo yao ambayo wanatarajia kuyafanyia kazi ili kuwarahisishia ufanyaji wao wa kazi, mamlaka hiyo imeweka utaratibu wa kukutana na kundi hilo mara kwa mara kwa lengo la kuendelea kuwapa elimu ya kodi.

Kayombo anasema, pia wamewataka kushirikisha wengine ambao hawakushiriki katika mafunzo hayo ili nao waweze kusogea karibu na mamlaka hiyo iweze kuwapa elimu ya kodi na baadaye waingie katika wigo wa kodi.

Anasema TRA imejiwekea utaratibu wa kutoa elimu ya kodi kwa walipakodi wake kabla ya kuwachukulia hatua za kisheria kutokana na kukwepa kodi.

Anasema ukusanyaji mapato inamgusa kila Mtanzania na kwamba wafanyabiashara wengine ambao biashara zao bado hazijarasimishwa wajitokeze ili waweze kurasimishwa na kuingizwa katika wigo wa kodi kwa maendeleo ya taifa.

Anasema maendeleo ya nchi yanategemea kodi ya kila mwenye kipato na kwamba kila mtu anatakiwa kuwa mzalendo kwa nchi yake kwani kodi hutozwa kulingana na kipato ambacho mtu anapata.

Anaongeza kuwa wafanyabiashara wanatakiwa kuweka utaratibu wa kutunza kumbukumbu za mapato pamoja na kumbukumbu za gharama za uendeshaji wa biashara ili kuepuka changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa ukadiriaji wa kodi.

Weka maoni yako

XHTML: You can use these html tags: <a href="" title=""> <abbr title=""> <acronym title=""> <b> <blockquote cite=""> <cite> <code> <del datetime=""> <em> <i> <q cite=""> <s> <strike> <strong>

YOUTUBE

WASHEREHESHAJI WAPATA MAFUNZO TRA, KULIPA KODI KARIBUNI