24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Wasanii wameisahau Dodoma?

nape-nnauyeNa MWANDISHI MAALUMU

KATIKA kipindi cha miaka ya 1970 wakati Serikali ikitangaza kuwa inahamisha makao makuu ya chama na serikali kwenda Dodoma lilikuwa ni jambo lililopokelewa kwa kishindo na makundi mbalimbali ya jamii.

Enzi hizo ilikuwa maamuzi ya chama yanapokelewa hima kwa kuwa ndicho kilichokuwa kimeshika hatamu ikimaanisha kuwa ilikuwa ni enzi za chama kimoja, itikadi moja na suala la kukinzana na maamuzi ya chama kiuhalisia ilikuwa ni mwiko.

Lakini ukweli unabakia kuwa maamuzi yale yalikuwa ni sahihi na yalikubaliwa kuanzia ngazi ya chini kabisa ya uongozi wa chama  hadi ngazi ya juu na matawi yote ya Tanu zaidi ya 1880.

Baada ya uamuzi huo maandalizi yalianza kwa kuundwa Mamlaka ya Ustawishaji wa Makao Makuu (CDA), licha ya kwamba mkakati huo baadaye ulidorora.

Lakini kama ambavyo inadaiwa kuwa Tanzania ina mambo mengi ambayo yanaigwa na nchi nyingine, kuhamia pamoja na kuendeleza makao makuu hayo ya nchi ni moja ya jambo yaliyozivutia nchi nyingine.

Nchi hizo mfano Nigeria ilibaini jambo hilo kwamba ni zuri na mara moja ikadodosa pamoja na kuja kujifunza mkakati huo unaendeshwaje na wapo wanaodai kuwa waliiomba ramani hiyo na kwa kasi kubwa wakaenda kuhamisha makao makuu ya nchi hiyo kutoka Lagos kwenda Abuja ambayo hivi sasa ni makao makuu ya nchi hiyo.

Pamoja na hali hiyo kwa kuliangalia suala la kuhamia Dodoma ambalo lilipongezwa na makundi mbalimbali ya jamii na si tu kupongezwa bali lilishangiliwa na hata  kuhamasisha makundi mengine kuunga mkono hatua hiyo.

Moja ya kundi ambalo limekuwa likitumiwa kuhamasisha jamii katika shughuli mbalimbali na hata katika maamuzi mengi yanayofanywa kisiasa ni kundi la wasanii.

Wakati maamuzi hayo yalipofanywa moja ya wasanii walioibuka na tungo zao za kuhamasisha na kuunga mkono hatua hiyo ni Mbaraka Mwinshehe Mwaruka  ambaye alitunga  wimbo wake uliohamasisha na kuunga mkono uamuzi huo wa chama cha Tanu kuhamia Dodoma.

Hata hivyo msanii mwingine ambaye  amewahi kuzungumzia au kusifia Dodoma ni pamoja na Remmy Ongala, akisema kuwa Dodoma ni fahari yetu pamoja na King Kiki  ambaye katika tungo yake moja alisifia kuwa Dodoma ni mji mkuu wa nchi.

Inaweza kuelezwa kuwa  kudodora kwa kasi ya kuhamia Dodoma ambako kunaelezwa kuwa kulikwama kutokana na mambo mengi ikiwemo vita ya Kagera.

Lakini tangu kuhuishwa kwa mkakati wa kuhamia Dodoma  ambayo ni maamuzi ya awamu ya tano imekuwa ni nadra kuwasikia wasanii wakitoa tungo zao za kuhamasisha au kuunga mkono.

Picha hiyo inatokana na sababu kuwa kila mara yanapotokea masuala makubwa ya kisiasa kama vile kampeni kama zile za uchaguzi mkuu mwaka jana, watu wanaokuwa mstari wa mbele kupigia debe masuala hayo ni wasanii.

Wengi walitarajia zingekuwepo tungo kwa ajili ya kuhamasisha au kuunga mkono jambo hilo lakini  hadi sasa kimya. Tafsiri yake inaweza kutafsiriwa wasanii hao hawajahamasika kulizungumzia jambo hilo kwa kuwa hawana miamko ya masuala ya kisiasa kama ilivyo katika miaka hiyo ambapo kuhamasisha kulikuwa ni kwa hiari bila kuweka mbele maslahi yao.

Lakini dhana nyingine inaelezwa kuwa inawezekana wasanii wameshabaini kwa mwenendo uliopo hata mtu ukijikomba bila kuonesha kuwa kujikomba kwako kuna tija hakutamtoa mtu.

Hivyo hoja inayobakia ni kwamba wasanii wameipotezea Dodoma katika tungo zao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles