23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Wasaidizi wa kisheria wamsaidia mjane kupata haki

Na Gurian Adolf-Nkasi

WASAIDIZI wa kisheria katika Kijiji cha Kirando wilayani Nkasi mkoani Rukwa, wamefanikiwa kumsaidia Lilian Ally kupata haki zake, baada ya ndoa yake kuvunjika na mume wake kuuza nyumba waliyokuwa wamejenga bila kumshirikisha.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Lilian aliwashukuru wasaidizi wakisheria kumsaidia kupata haki zake ambazo alikuwa amekata tamaa kuzipata kutokana na kutokuwa na fedha za kuwalipa mawakili.

Alisema mwaka 2015, alianza kupata mgogoro wa ndoa yake aliyofunga mwaka 2012, baada ya kukatishwa masomo akiwa kidato cha sita kwa kupewa ujauzito  na Hassan Abdul.

Alisema baada ya Abdul kupata mwanamke mwingine,alimtelekeza kwenye nyumba ya kupanga yeye na watoto wawili waliokuwa amezaa.

Alisema baada ya kupata mwanamke,aliamua kuhama nyumbani na kuacha kuwahudumia, huku akiwa na mipango ya kuuza nyumba waliojenga.

Alisema pamoja na changamoto hizo, aliamua kufanya biashara ambayo ingemuwezesha kuwatunza watoto,baadaye alirudi na kumlaghai kisha kuchukua mtaji alikuwa nao na kuuza samani za ndani  na nyavu za kuvulia samaki walizokuwa nazo.

Kutokana na changamoto alizopitia alifanikiwa kukutana na wasaidizi wa kisheria waliopo kijijini hapo ambapo waliweza kumsaidia na kufanikiwa kudai talaka.

Kwaupande wake, Filbeth Milambo,msaidizi wa kisheria aliyepo kijijini hapo, alisema alipata taarifa kuhusu mateso anayoyapata Lilian kutokana na kutelekezwa.

Alisema alimshauri taratibu za kufuata kwa mujibu wa sheria ili aweze kutendewa haki ambapo alifanikiwa kupata taraka kwa mujibu wa imani yake ya dini ya Kiislamu na kupata baadhi ya mali za familia ambazo mume wake aliamua kuziuza bila kumshirikisha.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Kirando, Wilbroad Nzumi alisema aliwashukuru wasaidizi wa kisheria na kusema wamekuwa msaada mkubwa kusaidia kutatua migogoro inayotokea.

Alisema mara kwa mara wameitisha mikutano ya hadhara na kutoa elimu kuhusiana na majukumu yao na kuwa wanatoa msaada wa kisheria bure.

Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali la Kaengesa Environment Society(KAESO) linalowajengea uwezo wasaidizi wa kisheria mkoani Rukwa, Ozem Chapita aliwasihi wananchi wenye migogoro mbalimbali ambao hawana uwezo wa kuwalipa mawakili kuwatumia wasaidizi  wa kisheria kwa sababu wanafanya kazi zao kwa mujibu wa sheria hivyo wanatambulika.

Mwisho

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles