23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

WARAKA WA JUMUIYA YA WANATAALUMA WA CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM KWA WATANZANIA

Na DK. GEORGE KAHANGWA

KATIKA siku za hivi karibuni Tanzania imeingia katika jaribu baya na hatari kubwa la kufifia kwa usalama wa wananchi.

Usalama katika taifa hili unazidi kuwa shakani, kutokana na ongezeko la matukio ya uhalifu. Kuna kila dalili kwamba, silaha kali nazo zimeongezeka mikononi mwa watu wasiofaa. Hali hii haiwezi kuachwa ikaendelea bila jitihada madhubuti za kuidhibiti.

Sisi Jumuiya ya Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDASA), hali tukitambua wazi kwamba nchi au jamii zilizopita njia hii ya kuongezeka kwa uhalifu na kuzagaa kwa silaha, hatimaye serikali zao zimeshindwa kutoa hakikisho la usalama kwa watu wa rika na madaraja yote, tumeona yafaa tutoe ujumbe wa tahadhari na kuionesha jamii haja ya kurejea na kuimarisha misingi ya usalama nchini.

Hapa, turejee yanayobainishwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Sura ya 3, hususan Ibara za 15 hadi 21 na 30 hadi 31.

Hivi leo duniani, zipo nchi ambazo zilianza kidogo kidogo kwa kushuhudia matukio kama yanayojiri kwetu wakati huu. Hivi sasa nchi hizo zimefikia hatua ambayo wakati wowote wahalifu wanaweza wakafanya mauaji ya mtu yeyote yule na pengine kuvamia taasisi kama vile shule na kuwaua wanafunzi wasio na hatia darasani.

Leo hii kuna nchi zisizotawalika tena kwa sababu vikundi vya wamiliki silaha vinazidi kuzaliwa. Mfano mbaya ni Somalia. Hao nao walianza kwa kufyatua risasi (moja) dhidi ya mtu (mmoja). Hivyo, kama Tanzania haitadhibiti ipasavyo haya yanayotokea sasa, tutakuwa tumetaka wenyewe kuelekea safari ya Somalia.

Tunayoyashuhudia leo yana athari kubwa sana ambazo inatubidi kuzitambua sasa na kutenda yatupasayo. Mathalani, sura na athari za jaribio la kumuua kasisi wa dini, ofisa wa jeshi au kiongozi wa kisiasa ni zaidi ya majeraha waliyoyapata mwilini na hatari ya mauti iliyowakabili.

Japo waliopigwa risasi ni mtu mmoja mmoja, kihoro na hofu iliyotokana na matukio hayo vimesambaa nchi nzima. Kwa maana hiyo, kilichofanyika ni ugaidi katika uhalisia wake. Mashambulizi hayo, pamoja na madhara mengine, yametufikisha mahali ambapo sasa nchi hii ina maeneo kadhaa ambayo wananchi wanaogopa kuyatembelea au kwenda kuishi huko kwa kuhofia usalama wao.

Hakika mashambulizi dhidi ya vikundi vya watu, mtu mmoja mmoja au dhidi ya viongozi, wawe wa kidini, kisiasa na kijamii, ni uchochezi wa hasira na chuki miongoni mwa wafuasi wao. Ni uibuaji wa visasi na ujenzi wa makundi makubwa ya mapambano ambayo baadaye nchi inaweza kushindwa kabisa kuyadhibiti.

Hata sauti zinazosikika kutoka taasisi mbalimbali na mtu mmoja mmoja zikilaani yanayotokea, ni sauti zinazochimbuka katika kusononeshwa na uhalifu, kuthamini sana uhai wa kila mtu na kwa kweli maana yake alaaniwaye kachukiwa na aliyechukia anaweza kuchukua hatua zaidi ya kulaani kwa kauli tu.

Haihitajiki kusisitiza sana kwamba usalama ni tunu yenye thamani sana si tu hapa Tanzania, bali katika mataifa yote ulimwenguni. Tuna kila sababu ya kuilinda. Kinyume chake kuuchezea ni kujitakia maangamizi sisi wenyewe.

Taifa hili lilijengwa katika misingi ya kwamba, usalama ni haki ya kila mwananchi (rejea katiba) bila kujali umri wake, jinsia, kabila, rangi, daraja la kijamii na itikadi zake kidini au kisiasa.

Kama tulivyooneshwa na waasisi wa taifa hili, umuhimu wa usalama uko katika mambo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na uwezo wa tunu hii kuchochea kujiamini, ubunifu, furaha, amani na utengamano katika jamii. Tunu hii itakapoendelea kuminywa, hayo mema tuliyoyafurahia kwa muda mrefu katika jamii yetu yatatoweka na itakuwa vigumu sana kuyapata tena.

Hivyo, UDASA tunapenda kulikumbusha taifa kwamba, kila mwananchi ana wajibu wa kulinda si tu usalama wake mwenyewe, bali na wa kila jirani yake. Mwananchi hapaswi kunyamaza au kutochukua hatua zilizo halali kisheria, anapoona usalama upo hatarini kwa namna yoyote ile.

Vile vile tunapenda kukumbusha kuwa, taifa lolote duniani lenye mwelekeo chanya, huunda taasisi na vyombo mbalimbali ambazo si kwa lengo jingine, bali kwa minajili ya kuwasaidia wananchi kuendelea kuwa salama.

Hivyo mihimili ya dola; Serikali, Mahakama na Bunge pamoja na vyombo vya mihimili hii, hususan vya Serikali vilivyoundwa nchini havina budi kuendelea kutambua kuwa, vina wajibu wa kulinda usalama wa kila raia bila kujali ana hali gani kimaisha au ana mtazamo gani kiitikadi.

Sababu pekee ya kwanini Tanzania tuna vyombo kama vile usalama wa taifa (Taifa ni Watanzania), majeshi ya ulinzi, polisi, vikosi vya zimamoto na jeshi la akiba, hata taasisi kama TFDA na nyinginezo, ni usalama wa kila mmoja wetu.

Vyombo hivi vinapaswa kufanya kazi ambazo zina matokeo yanayoongeza usalama wa watu. Litakuwa jambo la kusikitisha sana kwamba licha ya kuwapo kwa vyombo hivi, hali iendelee kuwa mbaya, hata watu walazimike kuhoji weledi na dhamira ya waliopewa dhamana ya kusimamia vyombo hivyo.

Kadhalika tunawahimiza na kuwasihi viongozi wote na kila mwenye mamlaka ya aina yoyote nchini waongeze juhudi katika kutekeleza kwa ukamilifu wajibu wa kulinda na kuheshimu (pasina chembe ya uzembe au hila) usalama wa watu wote. Wasikubali kuona nchi inachuruzika damu za wasio na hatia na wananchi wanakosa hakika ya usalama wao.

Aidha, hapana budi kila sheria inayotumika nchini sasa iangaliwe kwa lengo la kuhakikisha kuwa imelenga kuwahakikishia wananchi usalama au isikinzane kwa vyoyote vile na tunu hii.

Sheria zetu, viongozi na vyombo vyetu vitambue kuwa, Tanzania inastahili heshima ya kuwa nchi ambayo yeyote hawezi kuchezea usalama wa watu, uhai wa mtu, akaondoka na haki ya aliyetendewa vibaya.

Heshima hii ipatikane na kuonekana katika namna ambavyo wahalifu wanashughulikiwa kwa weledi na kwa kasi. Tanzania ifike mahali ambapo hakuna tukio jipya la uhalifu linalosahaulisha kushughulikiwa kwa ukamilifu tukio lililotangulia.

Kwa maneno mengine, kusiwe na kesi inayofifisha nyingine. Matukio ya mauaji ya wananchi katika maeneo kadhaa ya nchi yasiwekwe kando kwa sababu ya ofisi za taasisi fulani zimelipuliwa au kuvamiwa. Wala kulipuliwa ofisi kusifunikwe kwa sababu ya jaribio la kumuua mtu fulani maarufu na au asiye maarufu.

Hakika matukio ya hivi karibuni yanatukumbusha hayo. Yanatuweka katika hali ya kujitafakari na kurejea katika misingi itakayotuwezesha kuona pasipo shaka kwamba kila kinachofanywa na raia wa kawaida, kiongozi, taasisi na vyombo vya nchi kinalenga hakikisho la usalama wetu sote.

Kwa Watanzania wote, tunatoa wito kwamba, wakatae kwa nguvu zote kujengewa hofu. Wala watu wasiache kusimamia wanayoyaamini kwa kuchelea kukutwa na yaliyowapata wanaowasimamia hoja zao kwa ukamilifu.

Aidha, tunasisitiza ushauri wetu kwa Watanzania kwamba, katika nyakati hizi kila mmoja awe makini na kinachotokea jirani naye. Palipo na yanayotia shaka tuwe wepesi kuchukua hatua halali haraka (hususan kutoa taarifa mahali panapoaminika katika kujali uhuru na usalama).

UDASA tunaungana na Watanzania wote wenye mapenzi mema, kusikitishwa kwetu na mfululizo wa maovu yanayoendelea nchini.

Tunawatakia wote walioshambuliwa na kuumizwa vibaya katika matukio haya, wapate kupona mapema kimwili na kisaikolojia. Tutapenda kuona wahusika wa uhalifu unaoonekana wazi na uliofichama wanabainika, kukamatwa na kufikishwa haraka mbele ya vyombo vya haki.

Mungu aliye muumba wa taifa hili alijalie kutengemaa haraka kwa hali ya usalama wa kila mmoja.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles