27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Wape watu nafasi ya kuwa kioo chako

Na CHRISTIAN BWAYA

UNAJISIKIAJE pale unapogundua watu unaowaheshimu wanayafahamu mapungufu yako? Chukulia umebaini watu wanakuzungumza kwa namna inayoonesha kuwa una tabia zisizowapendeza.

Labda ni tabia yako ya uvivu kazini. Watu wanasema una tabia ya kusubiri kusukumwa ili utekeleze majukumu yako. Labda ni tabia yako ya kukosa uaminifu. Ukiaminiwa unatumia vibaya nafasi hiyo.

Pengine ni vile unavyoishi na watu. Watu wanasema wewe ni mtu mbinafsi usiyependa ushirikiano na watu. Je, ukipata mrejesho kama huo kwa watu utachukua hatua gani?

Ukweli ni kwamba hatupendi kusikia mapungufu yetu yakijadiliwa. Sababu ni kwamba tunafahamu pale udhaifu wetu unapofahamika, wakati mwingine, heshima yetu mbele ya macho ya jamii inakuwa shakani.

Ndiyo maana, pamoja na kuwa wapo baadhi yetu hudai hawajali watu wanawaonaje na wanasema vipi kinyume chao, lakini bado tunafahamu watu hawa hawa wakisikia mapungufu yao yanajadiliwa wanajisikia vibaya.

Tena saa nyingine wanajenga hadi uadui na watu hawa kwa sababu, kama nilivyotangulia kusema, wasingependa kusikia watu wanawatazama kwa picha mbaya.

Ukitafakari hayo, unajiuliza, hivi ni kweli tunaamini hatuna mapungufu kama yanavyoonwa na wengine? Je, ina maana tunafikiri tunajifahamu kuliko wanavyotufahamu watu wengine?

Ingawa tunapenda kujitazama kama watu wasio na mapungufu, bado ni kweli kuwa hatujifahamu vya kutosha. Kinachofanya tufikiri hivyo ni ile hulka yetu ya kupenda kujenga taswira chanya kwa kuonekana tu watu wema, waungwana tena wenye utu.

Inapotokea, mathalani, tumepata fursa kujielezea maisha yetu,tunachagua mambo mazuri ya kusema. Hata pale tunaposema mapungufu yetu, mara nyingine tunakuwa na nia iliyofichika.

Unaweza, kwa mfano, kumsikia mwanamume akieleza namna alivyoachwa na mpenzi wake lakini hafanyi hivyo kujidhalilisha. Ukimsikiliza kwa makini mwishowe anaweza kuishia kuonesha namna alivyokuja kupata mwanamke bora zaidi baadaye. Ndiyo kusema mapungufu aliyoyataja awali yametumika kama ngazi ya kuonesha tulivyo bora.

Kwa upande mwingine, wengi wetu hatuufahamu vizuri upande wa pili wa mapungufu yetu. Ingawa tunaweza kusema kila binadamu ana mapungufu yake, lakini bado inakuwa kama hatuamini na sisi ni hao hao binadamu wenye mapungufu yao. Unaweza kushangaa, kwa mfano, inakuwaje watu wanadai wewe ni mtu mgomvi wakati unavyojua wewe ni kwamba wao ndiyo wagomvi. Unajiuliza, mbona ninapofokeana na mtu mara zote na kuwa mhanga tu kwa maana ya kupambana na mtu ambaye kimsingi ndiye anakuwa mgomvi? Kwa nini ionekane mimi ndiyo mgomvi?

Huenda imewahi kukutokea. Mtu amekukosea unaona ni vizuri kuongea naye muondoe tofauti zenu lakini ghafla mwenzako anakubadilikia na kukugeuzia kibao. Kama mlikuwa mnazungumza kwa sauti ya chini, mathalani, anakujia juu kwa hasira, hataki kusikia unachomwambia, na anaweza hata kunyanyuka na kwenda zake.  Unajiuliza hajui anachokifanya?

Kwa nini apandwe na ghadhabu wakati kosa amelifanya mwenyewe? Kwa nini mtu mzima ajikute anafanya kitu ambacho kwa namna moja au nyingine kinamshushia heshima yake?

Huu ni mfano rahisi wa namna ilivyo vigumu kufahamu tabia zetu wenyewe. Tabia zetu ni sawa na kisogo ambacho japo kila mtu anacho bado huwezi kukiona bila msaada wa kioo.

Ni ajabu kwamba unaweza kuwa na uwezo mkubwa wa kuona visogo vya wenzako, lakini cha kwako mwenyewe huwezi kukiona. Ndivyo tulivyo tunapozitazama tabia zetu. Tunakuwa wepesi kuona kinachofanywa na wengine, lakini sisi hao hao tukifanya yale yale tunayoyaona kwa wengine tunakuwa kama hatuoni tulichokifanya.

Tunajipendelea. Hata pale tunapojua tumefanya jambo lisilokubalika kazi kubwa inakuwa ni kujitetea tukiamini tuna sababu ya msingi kuhalalisha kile tulichokifanya.

Bila shaka utakuwa na mifano mingi. Unakuwa mkali, kwa mfano, lakini unawashangaa wale wale wanaokushauri upunguze ukali kwa sababu wao ndiyo wanaoonekana kuwa wakali kuliko wewe.

Unakutana na mtu mwenye tabia ambayo yeye mwenyewe anailalamikia ikifanywa na watu. Mtu kama huyu anaamini kile anachokifanya yeye ni sahihi kwa sababu fulani fulani zisizokwepeka lakini wengine wakifanya yale yale anashangaa.

Hapa ndipo tunapohitaji kupata mrejesho wa watu wanaotuzunguka. Usipuuzie malalamiko ya watu kwako hata kama unaamini kinachosemwa hakina ukweli.

Usichukulie kirahisi mtazamo walionao watu kwako. Ingawa ni kweli wanaweza kuwa sahihi, lakini bado wanachokiona kwako kinaweza kuwa na kiasi fulani cha ukweli.

Ikiwa mke wako analalamika mara kwa mara kwamba humwelewi, usipuuze. Huenda kiburi chako cha uanaume kinakutuma kuamini anachokisema ni makelele. Kuwa mnyenyekevu msikilize. Lakini pia ikiwa mume wako analalamika una makelele usipuuze.

Usijipe haki ukapuuza kile anachokiona kwako. Tukirejea mfano wetu wa kisogo, inawezekana huyo anayekulalamikia kwa mapungufu usiyoyapenda kuyasikia anaona vizuri zaidi kuona kile usichokiona wewe. Mpe nafasi awe kioo chako.

Christian Bwaya ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Mawasiliano: 0754870815 Twitter @bwaya

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles