24.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

WANAWAKE SASA WANAWEZA KUPOKEZANA MJI WA MIMBA

JOSEPH HIZA NA MASHIRIKA YA HABARI


WANAWAKE watatu watakuwa wa kwanza nchini Uingereza kupandikizwa matumbo ya uzazi, ambayo wana matumaini hatimaye watatimiza ndoto yao ya kuitwa mama.

Watapitia upasuaji ndani ya miezi michache ijayo kwa kutumia miji ya mimba iliyotolewa na mama au dada zao.

Madaktari wanaamini mchakato huo katika siku za usoni utaruhusu maelfu ya wanawake kufikia ndoto zao za umama.

“Huu ni wakati wa kusisimua, tuna fursa ya kuleta tofauti,” anasema Richard Smith, mtaalamu mshauri wa masuala ya uzazi anayeongoza mradi huo.

“Ni hatua kubwa kwa wanawake wenye matatizo ya uzazi. Hadi sasa njia mbadala wanayotumia ni kuasili au kutumia mtu mwingine kuwazalia watoto, kitu ambacho daima si rahisi.

“Inamaanisha kuwa mtoto wa kwanza wa Uingereza atazaliwa kutokana na mchakato huu mpya wa upandikizaji tumbo la uzazi ifikapo mapema mwaka 2020. Upasuaji utafanyika katika Hospitali ya Churchill mjini Oxford.

Upasuaji wa kwanza uliofanikiwa wa kupandikiza wanawake tumbo la uzazi ulifanyika nchini Sweden mwaka 2013.

Ingawa Uingereza ndiyo iliyofungua njia kupitia utafiti wake juu ya uwezekano huo, lakini mitazamo ya jamii na uhaba wa fedha ulisababisha mataifa mengine yaitangulie.

Matibabu haya ambayo yanagharimu Pauni 30,000 za Uingereza sawa na zaidi Sh milioni 90 za Tanzania kwa kila mwanamke, yanagharimiwa na taasisi ya hisani ya Upandikizaji Tumbo la Uzazi Uingereza (Womb Transplant UK).

Sababu ya kufanya hivyo ni kwa kuwa mchakato huu bado upo katika majaribio kuweza kuwa chini ya Shirika la Taifa la Huduma za Afya Uingereza (NHS) linalohudumia wakazi wa Uingereza milioni 65.

Kwa Smith, mshindi wa tuzo ya upasuaji kutoka Chuo Kikuu cha Imperial London, ni matokeo ya utafiti wa miaka 20 alioufanya na timu yake bila kutengewa fungu la fedha.

Wanawake watatu watakaochaguliwa ndani ya wiki chache zijazo watatokana na orodha ya wanawake 50 waliopo katika foleni ya kupandikizwa.

Wote wanataka watoto lakini walizaliwa bila kuwa na tumbo la uzazi au liliondolewa kutokana na maradhi kama vile saratani.

Wakiwa na umri wa miaka kati ya 24 na 38 wanawake hao wanapaswa kuwa wawe wanaotokana na uhusiano wa ndoa wa muda mrefu, wenye afya na bado wana mayai yao. Pia watapitia mtihani wa kisaikolojia.

Wakati wa kuelekea upasuaji huo, wenzi watakaofanikia watapitia tiba ya IVF ambayo ni utungishaji mayai nje ya na kuyarejesha katika mji wa uzazi baada ya miezi sita.

Mtoto atahitaji kuzaliwa kwa njia ya kisu kwa sababu mji wa mimba uliopandikizwa una uwezekano wa kujiondoa wakati wa uzaaji mtoto.

Mara familia ya mgonjwa inapokuwa kamili, tumbo litaondolewa ili kuzuia hitaji la kuchoma sindano ya dawa inayozuia tumbo kukataliwa.

Watoto 11 tayari wamezaliwa duniani kama matokeo ya michakato 42 ya upandikizaji mji wa mimba, mengi yakiwa nchini Sweden, Marekani na Mashariki ya Kati.

Mwaka 2014, Malin Stenburg, alikuwa mwanamke wa kwanza duniani wakati akiwa na miaka 36 kupata mtoto  baada ya kupandikizwa tumbo la uzazi lililotolewa na rafiki wa familia mwenye umri wa miaka 61.

Vincent alizaliwa miezi miwili kabla ya wakati kufuatia matibabu katika Chuo Kikuu cha Gothenburg, Sweden ambacho kina kiwango cha juu cha mafanikio kuliko mfumo wa kawaida wa IVF.

Ijapokuwa idhini ilitolewa nchini Uingereza mwaka 2015 kupandikiza matumbo ya uzazi kutoka kwa wafu, wataalamu wa afya hupendelea zaidi matumbo ya uzazi kutoka wanafamilia walio hai ili kupunguza uwezekano wa kiungo hicho kukataliwa ndani ya mwili.

Wakati upandikizaji wa huko nyuma ulifanya upasuaji kuchukua hadi saa 13.

Watoto wawili tayari wamezaliwa kwa kutumia njia hiyo ifahamikayo kwa kitaalamu– abdominal radical trachelectomy. Asasi ya Womb Transplant UK sasa imeruhusiwa na NHS kuijaribu njia hiyo kwa wagonjwa wa Uingereza.

Ijapokuwa wagonjwa wengi walio katika foleni wana ndugu walio tayari kutoa tumbo la uzazi, taasisi ya hisani ina fedha za kutoshelezea michakato mitatu tu.

Lakini baada ya tangazo hili jipya, kuna matumaini itachochea uchangijaji wa Pauni 400,000 zinazohitajika kwa upandikizaji mwingine miwili zaidi kipindi cha miaka miwili ijayo.

Iwapo mchakato utaenda vyema, wataalamu wa afya wana matumaini utaingizwa katika mipango ya NHS ifikapo mwaka 2022 na hivyo kunufaisha wengi zaidi.

Hata hivyo, Smith alionya kuwa mchakato mzima hautakuwa kitu rahisi kwa waliochagua kubadili maisha.

Lakini baba huyo wa watoto wanne aliongeza: “Mtu yeyote ambaye anaona maumivu wapitiayo wanawake – si tu hawawezi kubeba watoto lakini pia husiano na wenzi wao zimeharibika, wamevunjika moyo na kujihesabu si watu waliokamilika– atajua haya ni makundi ya wanawake ambao wako katika shida kweli kweli.

“Ni juu yangu na madaktari wengine kufanya kila linalowezekana kuwasaidia wanawake hawa kuwa wazazi na kupata faraja itakayoondoa hali ya kujiona dhalili.”

Lakini pia baadhi ya madaktari wameonya upandikizaji mji wa mimba unahitaji majaribio ya hali ya juu kimaabara kabla ya kuweza kutumika kwa watu wengi zaidi.

Wataalamu kutoka Japan walipitia matokeo waliyopata kutokana na tafiti zao na walisema mbinu hiyo inatoa matumaini makubwa kwa wanawake, lakini kuna masuala ya kuangalia hasa vikwazo vilivyopo.

Walisema njia nzuri zaidi inapaswa iwapo kuna uhusiano wowote baina ya visababishi kama vile umri wa mtoaji wa tumbo la uzazi na wapokeaji na hali nyingine za kiafya na kukwama kwa mchakato.

Wakiandika katika jarida la Kimataifa la  Ukunga na Jinaikolojia (elimu uzazi), walisema matatizo yanayojitokeza ni pamoja na katika njia ya mkojo, uambukizo na kuganda kwa damu (thrombosis) katika mishipa na kuvuja kwa damu ndani ya tishu (haematoma) kwa wale wapandikizwao.

Waandishi hao wanasema dawa zinazopunguza uwezo wa mwili kukataa viungo vya kupanzikizwa (Immuno-suppressants) zinaweza kuchochea kuibuka kwa kifafa cha mimba (pre-eclampsia) na usimamizi wa hali ya juu wa mimba unahitajika.

Hatua za kusimamia matibabu ya kukataliwa kwa mji wa mimba uliopandikizwa wakati wa ujauzito unahitajika na unabakia kuwa shughuli kubwa zaidi.

Aidha, wataalamu hao wa Japan wanasema kuna mafanikio yenye ukomo tangu kupandikizwa kwa mji wa kwanza wa mimba mwaka 2013.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles