26.9 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

WANAWAKE HUPATA SARATANI SHINGO YA KIZAZI KWA KUCHANGIA WANAUME

Na Editha Karlo, Kigoma


TAKWIMU za Shirika la Kimataifa la Atomiki la Utafiti wa Saratani (IARC), na za Shirika la Afya Duniani (WHO), zinaonesha kuwa kila mwaka kuna wagonjwa wapya wa saratani milioni 14.1.
Inakadiriwa kuwa ifikapo mwaka 2035 idadi ya wagonjwa hao wataongezeka hadi kufikia milioni 24 katika nchi zinazoendelea, Tanzania ikiwamo.

Wataalumu wa masuala ya afya wanasema saratani ya shingo ya kizazi hutokea katika chembechembe za shingo ya kizazi, ambayo ni sehemu ya chini ya mji wa mimba (uteri), inayoungana na uke.
Saratani ya shingo ya kizazi inaongoza kwa kuwashambulia wanawake ikifuatiwa na saratani za ngozi, matiti na koo.

Takwimu za Kituo cha Kudhibiti Maradhi Duniani (CDC), za mwaka 2008 zinaonesha kuwa katika kila wanawake watatu, wawili kati yao wanashambuliwa na saratani ya aina hii duniani.
Hapa nchini inakadiriwa kuwa zaidi ya wanawake milioni 14 walio katika umri wa kuzaa kuanzia miaka 18 hadi 25 wapo hatarini kupata maambukizi ya saratani ya shingo ya kizazi.

Takwimu zinaonesha wanawake wanaopata saratani hii kwa mwaka ni 7,304 kati yao wanaofariki ni 4,216.
Daktari Bingwa wa magonjwa ya akina mama kutoka Hospitali ya Mkoa wa Kigoma (Maweni), Dk. Lameck Mdengo anasema miongoni mwa visababishi vya ugonjwa huo ni kuanza kufanya ngono katika umri mdogo.

Dk. Mdengo anasema kuwa kuolewa kwenye umri mdogo, kuwa na wapenzi wengi, kusafisha sehemu za siri kwa bidhaa zenye kemikali na kuzaa mara kwa mara kunachangia wanawake kupata saratani ya shingo ya kizazi.
Chanzo kingine cha ugonjwa huo ni uvutaji wa sigara na kutumia vidonge vya kupanga uzazi kwa muda mrefu.
“Zamani wazazi wetu walikuwa wanazaa hadi watoto 18 lakini hawakuwa na haya maradhi, ni kwa sababu maisha ya zamani na sasa ni tofauti.

“Katika kiwango cha kimataifa, wastani wa mwanamke kuzaa bila kupata saratani ya shingo ya kizazi ni watoto watatu hadi wanne,” anasema.
Anasema saratani ya shingo ya kizazi inatokana na aina 40 ya virusi, ambapo aina mbili ikiwa ni virusi vinavyosambaa kwa njia ya ngono ambavyo ni ‘Human Papilloma Virus (HPV) Squamos Cell Carcinoma, kirusi namba 16 na Adenocarcinoma namba 18 ni kati ya virusi 40 vinavyosababisha saratani ya kizazi.

Anasema saratani ya kizazi sasa hivi ndiyo inayoongoza ikilinganishwa na nyingine nchini, huku asilimia 80 ya wagonjwa wakiwa wameambukizwa kwa njia ya ngono.
“Saratani hiyo usambaa kwa njia ya ngono kutoka kwa mwanamke mmoja kwenda kwa mwingine. Mwanamke mwenye saratani kizazi anapofanya ngono, mwanamume huchukua virusi na kumwambukiza mwingine atakayefanya naye ngono,” anasema.

Mtaalamu huyo anasema pia kuna wanaume ambao tayari wameshakuwa na maambukizi ya HPV ambapo hutembea na virus vinavyoitwa ‘high risk sexual male patner.’ Wanaume wa aina hii unakuta kila akioa mwanamke anakufa kwa saratani ya shingo ya kizazi, lakini virus hivyo yeye havimuathiri.

“Wanawake wengi wamekutwa na saratani ya shingo ya kizazi wakiwa katika umri mdogo kuanzia umri wa miaka 35 na kuendelea, hii inamaanisha kwamba walipata maambukizi wakiwa na miaka kuanzia miaka 20 hadi 25,” anasema daktari huyo.

Anasema mgonjwa anaweza kupata maambukizi hayo na akagundua tatizo hilo hata baada ya miaka 10 hadi 15 ambapo tatizo hujitokeza hadharani.

“Maambukizi ya saratani ya shingo ya kizazi huchukua muda mrefu hadi kujulikana, kwa kawaida mwanamke anaweza kuishi na maambukizi hata kwa miaka 15 ndipo anagundua tatizo. Hata hivyo huwa inategemea pia na kushuka kwa kinga zake za mwili, ikitokea akapata ugonjwa mwingine kama Ukimwi basi na saratani nayo itajitokeza,” anabainisha.

Anasema kuwa wanawake wanaoishi na maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) wapo hatarini zaidi kupata saratani ya shingo ya kizazi kuliko wale wasiougua ugonjwa huo.
Anasema ili kujikinga na ugonjwa huo ni muhimu kuwa mwaminifu katika uhusiano wa kimapenzi na kutumia kinga pindi unapokutana kimwili.

Anazitaja dalili za ugonjwa huo kuwa ni pamoja na kutokwa damu na uchafu ukeni, kupata hedhi bila ya mpangilio maalumu, kutokwa na damu ukeni baada ya tendo la ndoa na maumivu wakati wa kujamiiana.
Mtaalamu huyo anataja tiba za magonjwa ya saratani kuwa ni mionzi, dawa na upasuaji.

“Ni vema wasichana wakajitunza na kuacha kufanya ngono wakiwa katika umri mdogo ili kujiepusha na uwezekano wa kupata mimba na saratani ya shingo ya kizazi siku za mbeleni,” anawaasa vijana.

Mratibu wa Chanjo ofisi ya Mganga Mkuu Hospital ya Mkoa Kigoma (Maweni), Silas Kasanga anavitaka vyombo vya habari kusaidia kuelimisha jamii kuondokana na imani potofu kuhusu chanjo ya saratani ya shingo ya kizazi.
“Wapo wanaodhani kwamba serekali inafanya zoezi hili la kutoa chanjo kwa majaribio au mbinu za kutaka kuua watoto, ninawaomba wazazi waachane na dhana potofu, chanjo hii ni salama kabisa,” anasema.
Kasanga anawahimiza wanawake kwenda hospitalini mapema kwa ajili ya kufanyiwa vipimo kwa kuwa saratani ya shingo ya kizazi inatibika.

Naye Ofisa Mpango wa Chanjo Taifa, Consolatha Njako anasema chanjo hiyo ni salama na imethibitishwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto pamoja na WHO.
Anasema chanjo hiyo itasaidia kupunguza saratani ya shingo ya kizazi kwa kiwango kikubwa.

“Chanjo hii tutatoa kwa wasichana waliofikisha umri wa miaka 14; hawa tunaamini bado hawajaanza kujihusisha na uhusiano wa kingono hivyo, tutawapa chanjo ili kuwakinga.

“Itatolewa kwa dozi mbili ili kupata kinga kamili ambapo dozi ya pili itatolewa baada ya miezi sita,” anasema Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Dk. Paul Chawote.
Anasema ni muhimu kukamilisha dozi zote ambazo itatolewa bure.

Anasema utoaji wa chanjo hiyo mkoani Kigoma utafanyika Aprili 30 mwaka huu katika Wilaya ya Uvinza, eneo la Kazuramimba ikiwa ni wiki ya chanjo.

“Serekali yetu inafanya juhudi za kupambana na ugonjwa huu, ambapo tunatarajia kuwapatia chanjo watoto 33,000 kwa mwaka huu,” anasema na kuwaasa wananchi kujenga tabia ya kupima afya mara kwa mara ili kubaini maambukizi mapema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles