24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Wanawake 56 wawekewa matiti bandia

Bosco Mwinuka (TUDARCO) Na Tunu Nassor –Dar es salaam

HOSPITALI ya  Aga Khan (AKHD) kwa kushirikiana na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na shirika la kimataifa la kusaidia wanawake la Reconstructing Women International (RWI), wamefanya upasuaji wa kuboresha viungo na ngozi bure kwa wanawake na watoto wa kike 56 walioungua moto, ajali za barabarani na majanga majumbani.

Sambamba na hilo, wamefanikiwa kupunguza matiti kwa mwanamke mmoja ambayo yalikuwa makubwa na kumsababishia usumbufu na maumivu ya mgongo na shingo.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Daktari Bingwa wa upasuaji wa AKHD, Dk. Aidan Njau, alisema lengo la upasuaji huo kwa wasiokuwa na uwezo, ni kuwarudishia uwezo wa kutumia viungo vyao vilivyoharibika.

Alisema katika matibabu hayo baadhi ya wagonjwa watapatiwa mazoezi ya viungo pamoja na kuchomwa sindano ya kulainisha ngozi iliyokakamaa ili iruhusu kiungo chake kufanya kazi tena.

“Leo (jana) tunamsaidia mwanamke mwenye matiti makubwa ambayo yanamsababishia maumivu ya mgongo na shingo, hivyo tunapunguza ukubwa ili aweze kuwa na mwonekano mzuri na kuondokana maumivu,” alisema Dk. Njau.

Alisema katika awamu ijayo itakayofanyika Novemba, wanatarajia kufanya upasuaji wa kupunguza matiti kwa wanawake wanne.

Dk. Njau alisema katika kambi hiyo ya matibabu, walipokea wagonjwa 150 ambao walihitaji huduma hiyo ambapo baada ya kuwafanyia uchunguzi walipata wagonjwa 56 wenye uhitaji wa haraka wa matibabu hayo. 

Alisema wanawake wanne waliokatwa matiti kutokana na ugonjwa wa saratani ya titi, wamewatengenezea mbadala wake ili waweze kuwa na mwonekano mzuri mbele ya jamii.

“Wagonjwa waliopewa kipaumbele katika huduma awamu hii ni wale wenye matatizo zaidi ya moja, kwani wengi wao wanajinyanyapaa wao wenyewe kwa kujiona wapo tofauti na wenzao,” alisema.

Akizungumzia changamoto walizokutana nazo, Daktari Bingwa wa upasuaji kutoka RWI, Andrea Pusic, alisema uelewa mdogo wa jamii unasababisha kuwaficha watoto waliokumbwa na majanga kwa kuwaona kuwa hawafai katika jamii.

“Bado jamii haijawa na uelewa wa kutosha katika masuala haya, jambo linalosababisha kuongeza unyanyapaa kwa watu waliokumbwa na hali hiyo,” alisema Dk. Andrea.

Meneja wa Idara ya Masoko na Mawasiliano, Olayce Lotha, alisema wametumia Sh milioni 285 kutoa huduma hiyo kwa wananchi.

“Huduma hii imefanikiwa kutokana na kupata msaada mbalimbali kutoka kwa wadau wa afya, wakiwamo benki ya DTB, Jubilee Insurance, Sadaka, watu binafsi na Mpango wa Hospitali ya Aga Khan Dar es Salaam kusaidia wagonjwa,” alisema Olayce.

Alisema tangu kuanza kwa kambi hizo hospitalini hapo mwaka 2016 hadi msimu huu, wamefanikiwa kusaidia wanawake na watoto wa kike 199 kurudi katika hali zao za kawaida.

“Tumezunguka hadi mikoani kutoa elimu na kuchukua wagonjwa ambao wana uhitaji wa huduma hii, lakini hawana uwezo wa kulipia matibabu kwani ni gharama kubwa,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles