30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Wanaume vinara unywaji pombe K’ndoni

Unywaji pombe
Unywaji pombe

NA ESTHER MBUSSI, DAR ES SALAAM

UTAFITI uliofanywa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), umeonyesha asilimia 55.5 ya wanaume katika Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam ni vinara wa ulevi wa pombe.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana wakati wa uzinduzi wa ripoti ya utafiti huo, Msimamizi wa Utafiti, Dk. Severine Kessy, alisema kukithiri huko kwa ulevi kumesababisha ongezeko kubwa la vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Alisema hali hiyo inatokea kwa kuwa kuna uhusiano mkubwa kati ya pombe na vitendo hivyo.

Dk. Kessy alisema katika utafiti huo, wamebaini asilimia 45.4 ya wanaume wengine hawatumii kabisa.

Kwa upande wa kinamama, alisema ulevi umefikia asilimia 40, wakati asilimia 60 hawatumii pombe.

Alisema katika utafiti huo, imebainika asilimia 44 ya watu wenye umri wa miaka 18-24, bila kujali jinsia ndio wanaokunywa zaidi pombe kuliko umri wowote.

Dk. Kessy alisema utafiti huo uliofanyika katika Wilaya ya Kinondoni pekee, ulijikita zaidi maeneo makuu mawili; athari za pombe, upatikanaji na uelewa kuhusu ulevi huo.

“Asilimia 48 ya watu waliohojiwa imeonyesha wana uelewa kuhusu pombe, wakati asilimia 51 hawajawahi kutumia.

“Kwa upande mwingine, katika utafiti wetu tulibaini ongezeko la wasomi linawiana na ongezeko la unywaji pombe ambapo wanafunzi na wale waliohitimu kidato cha nne, cha sita na vyuo wanakunywa zaidi kulingana na hatua za kimasomo.

“Tuliangalia namna watu wanavyoanza kutumia pombe na vishawishi, tukabaini mengi.

“Kwa msingi huu, asilimia 39 walisema walianza wenyewe, asilimia 13 walijifunza kutoka kwa wazazi wao, asilimia 38 walifundishwa na marafiki wa kawaida na asilimia 9 walishawishiwa na wapenzi wao,” alisema Dk. Kessy.

Pamoja na mambo mengine, alisema asilimia 19 hadi 12 waliohojiwa ni watumiaji wa pombe kila siku.

Alisema asilimia 19 inaonyesha wanakunywa mara mbili hadi nne kwa wiki na kila wanapokwenda kunakouzwa pombe wanakunywa chupa mbili hadi nne.

Dk. Kessy alisema asilimia 63 ya walihojiwa walisema nyumba zao ziko chini ya hatua 100 kutoka sehemu ambazo pombe zinauzwa.

Alisema utafiti huo pia ulibaini athari za unywaji pombe ambapo asilimia 30.8 waliwahi kunyanyaswa na watu waliokunywa pombe, asilimia tisa waliwahi kufanya ngono baada ya kunywa pombe na asilimia tano walipewa talaka kutokana na pombe.

“Kundi la watoto ambao waliwahi kupigwa na mzazi au mlezi aliyekunywa pombe ni asilimia 23, asilimia 26 ya walio kwenye ndoa waliwahi kupigwa na watalaka wakati asilimia 44 waliwahi kupigwa wakiwa kwenye ndoa,” alisema Dk. Kessy.

Alisema kwa upande wa afya, watumiaji wengi wameathirika kiafya.

Ofisa Ustawi wa Jamii wa chama hicho, Gladness Munuo alisema wamekuwa wakitoa fedha kusaidia watoto waliotelekezwa na wazazi wao.

Alisema kuanzia Aprili hadi Agosti, mwaka huu asilimia 60 ya watu walioripoti kesi zao kwenye chama hicho zimetokana na ulevi pombe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles