WANAUME IRINGA WATAKA MAREKEBISHO YA NDOA KUWATALIKI WAKE WALIOWATELEKEZA

0
784

|Francis Godwin, IringaBaadhi ya wanaume mkoani Iringa wameomba sheria ya ndoa ifanyiwe marekebisho na kutamka kuwa pale mke anapotelekeza  familia asiwe tena mke halali wa ndoa.

Rai hiyo wameitoa jana katika mkutano wa utoaji elimu ya fursa sawa kwa wote na haki za wanawake na watoto wa kike katika umiliki  wa mali, ulioandaliwa na Asasi isiyo ya  Serikali ya Iringa Civil Society Organization (ICISO) kwa vijiji vya Makifu, Mahuninga na  Kisilwa.

Akizungumza kwa niaba ya wanaume katika  mkutano huo, mmoja wa wanaume hao, Ally Mdapo amesema baadhi ya wanawake   wamekuwa na tabia ya  kuzitelekeza familia  kwenda mijini ambako hukaa miaka zaidi ya sita.

“Akishakaa muda wote huo anarudi kijijini, kitendo hicho kimesababisha wanaume kuoa mke mwingine na wakati huo huo yeye akirudi anataka atambulike kama mke, tunaomba  sheria irekebishwe mwanamke huyu asiwe  tena mke halali wa ndoa tofauti na ilivyo sasa,” amesema.

Kwa upande wao baadhi ya wanawake katika Kata ya  Mahuninga  wilayani, Iringa mkoani humo waliokuwapo katika mkutano huo,  wamesema hawako tayari kurithiwa kwa kuachiwa mali  ikiwamo ardhi na nyumba pindi wanapofiwa na waume zao.

“Zamani vitendo vya wajane kulazimishwa kuolewa na ndugu upande wa  kiume baada ya mume kufariki lilikuwa kubwa jambo lililosababisha vifo vinavyotakanavyo na magonjwa ya kuambukiza kama Ukimwi.

“Ndugu upande wa  kiume wakiona mume  wako amefariki mara tu baada ya kuzika unaona mdogo mtu wau kaka mtu  anatanguliza koti na kiti nyumbani kwa mjane na baada ya  muda analeta sanduku la nguo  zake ukipokea koti ama kiti ujue tayari  anakuwa mume wako,” amesema mmoja wa wanawake hao, Matrida Myovela.

Kwa upande wake mwezeshaji  wa  ICISO, Ahazi Sibale, amesema: “Kuhusu wanawake wanaotengana na  waume zao na baadaye kurudi, sheria ya ndoa inatambua hao ni wake halali na sheria  inamtambua mke halali ni yule aliyeolewa kwa ndoa au wale walioishi pamoja kwa muda wa miaka mitatu na kuachana kwao hadi mahakamani na si vinginevyo, hata hivyo  mali zote zilizopatikana wakati huo ni mali  za wanandoa hao.”

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here