24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

‘Wanaume 28’ wa FDL kuanza kupimana ubavu leo

Damian Masyenene

LIGI Daraja la Kwanza Tanzania Bara (FDL) msimu huu inatarajiwa kuanza rasmi leo, kwa timu 16 kushuka dimbani kufungua pazia.

ligi hiyo  ilishaanza kusisimua kuanzia kwenye dirisha la usajili, huku timu za Dodoma Jiji, Pamba SC na Gwambina zikiteka hisia za mashabiki kutokana na usajili zilioufanya.

FDL imegawanywa katika makundi mawili yenye timu 12 kila moja,  na kufanya kuwa na jumla ya timu 28 zinazosaka nafasi mbili za kufuzu Ligi Kuu  moja kwa moja na nafasi nyingine mbili za kucheza hatua ya mtoano.

MTANZANIA limeitazama kwa undani michezo nane ya kwanza itakayopigwa leo ikihusisha mechi tatu za kundi B na tano za kundi A, ambapo viwanja vya Gwambina, Kaitaba, Mkwakwani, Kipija Arena, Highland Estates, Jamhuri, Sabasaba na Uhuru vitawaka moto.

Gwambina Vs Arusha FC

Ni mchezo namba moja wa kundi B na ni mechi ya kisasi inayowakutanisha ndugu wa zamani ‘waliotengana’, kwani timu zote zilikuwa za Arusha kabla ya Gwambina iliyokuwa ikijulikana kama Arusha United kubadilisha makazi na kuhamia wilayani Misungwi mkoa wa Mwanza.

Gwambina wanaofundishwa na kocha wa zamani wa timu za Namungo FC, Mbao FC, Toto Africans na timu ya taifa ya Tanzania (Taifa stars), Fulgence Novatus,  ni moja ya timu zinazopigiwa chapuo kufanya vyema msimu huu.

Usajili wao ulizua gumzo, baada ya kuwanasa nyota kadhaa wa Ligi Kuu, akiwemo mkongwe Jacob Masawe (Stand United), Kelvin Sabato (Mtibwa), Raizin Hafidh (Coastal Union), Malika Ndeule, Ibrahim Job na Yusuph Kagoma.

Geita Gold FC vs Mashujaa

Baada ya msimu uliopita kuikosa nafasi ya kupanda daraja baada ya kuondoshwa na Mwadui FC katika mchezo wa mtoano, Geita Gold FC wamejipanga kivingine na sasa wanaitaka nafasi hiyo wakianza kwa kucheza na Mashujaa FC ya mkoani Kigoma katika dimba la Kiataba mjini Bukoba.

Mashujaa haipewi nafasi sana lakini kila msimu imekuwa ikisaka nafasi ya kusalia kwenye ligi hiyo na kukwepa kudondokea daraja la pili, msimu huu inayo kazi ya kuhakikisha inafanya vyema.

Sahare All Star vs Transit Camp

Mchezo huu utapigwa katika dimba la Mkwakwani Tanga, ambapo wenyeji (Sahare All Star) waliokuwa kundi A msimu uliopita, safari hii wamehamishiwa kundi B lilitawaliwa na timu kutoka Kanda ya Ziwa pamoja na mbili kutoka Dar es Salaam, tayari ni mtihani mwingie kwao.

Kipimo ni Transit Camp ambao hawaonekani lakini wamo kila msimu.

Boma FC Vs Mlale FC

Mchezo huu namba moja wa kundi A utapigwa kwenye uwanja wa Kipija Arena mkoani Mbeya, ambapo Boma FC watakuwa na kibarua kizitos cha kuhakikisha wanaanzia walipoishia msimu uliopita.

Msimu uliopita waliuanza vyema wakiwa na mshambuliaji wao, Gaudence Mwaikimba na Kocha Muhibu Kanu aliyetimkia Pamba SC ya Mwanza na baadhi ya nyota wao wameondoka.

Mwaka jana walikuwa kundi B na sasa wamehamishiwa kundi A, wakikutana na maafande wa JKT Mlale kutokaSongea nao wakiisaka nafasi ya kucheza ligi kuu kwa udi na uvumba.

Ihefu FC Vs Majimaji FC

Ni mchezo mwingine wa kundi A utakaochezwa leo kwenye Uwanja wa Highland Estates, ambapo Ihefu FC ya Mbeya itawakaribisha Majimaji FC ya Songea.

Ihefu ni wageni wa Ligi hiyo wakitokea daraja la pili (SDL) msimu uliopita,  ni mchezo wao wa kwanza wa FDL wakiwakaribisha wenyej’ wa mikiki mikiki ya ligi hiyo, Maji Maji FC ambao wamewahi kucheza Ligi Kuu kwa nyakati tofauti, na sasa wanataka kuutumia msimu huu kurejea kwenye purukushani za VPL.

Dodoma Jiji FC Vs Reha FC

Klabu ya Dodoma Jiji ni miongoni mwa timu zilizofanya usajili mzuri na wa uhakika na kuwa miongoni mwa wanaopigiwa chapuo ya kupanda daraja msimu huu, wanaikaribisha Reha FC ambayo ina misimu miwili tu kwenye ligi hiyo.

Usajili wao ni pamoja na Abubakar Ngalema,Hassan Kapona (Mbao), Ally Shiboli (JKT Tanzania), Hamis Mcha Vialli (Ruvu Shooting), Joseph Mapembe (Biashara United), Rajabu Kibera na Jamal Mtegeta (Alliance).

Mchezo huo utapigwa kwenye uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma saa 10 jioni, ambapo Dodoma wanaongozwa na kocha aliyezipandisha daraja timu za Polisi Tanzania na Alliance FC.

Njombe Mji vs Friends Rangers

Njombe Mji tangu iliposhuka daraja misimu miwili iliyopita imeendelea kuhangaika kuhakikisha inarejea tena, wanawakaribisha wazoefu wa ligi hiyo, Friends Rangers wanaonolewa na kocha wa siku nyingi, Henry Mzozo.

Unatarajiwa kuwa mchezo wa kuvutia na wa kusisimua kutokana na uwezo wa mwalimu huyo kupata wachezaji wenye vipaji ambao hawana majina.

Friends Rangers huenda wakawa na msimu mzuri,  baada ya kuyatumia mapumziko ya dirisha la usajili kushiriki michuano ya Ndondo Cup, jijini Dar es Salaam na kufika hatua nzuri.

Ashanti United na Mbeya Kwanza

Ashanti United bado inasuasua kurejea Ligi Kuu tangu iliposhuka daraja misimu kadhaa iliyopita, inaanza ligi kwa kuikaribisha Mbeya Kwanza kutoka mkoani Mbeya, mchezo ukipigwa dimba la Uhuru jijini Dar es Salaam.

Mbeya Kwanza ni miongoni mwa timu zilizofanya vyema msimu uliopita,  ikishika nafasi ya pili katika kundi A,  nyuma ya Namungo FC iliyopanda daraja, lakini wakatolewa katika michezo ya mtoano na Pamba SC.

Michezo mingine itakayopigwa katika raundi ya kwanza ni African Lyon dhidi ya Mufindi United, Pamba SC dhidi ya Stand United, Green Worriors ikiikaribisha Mawenzi Market pamoja na Gipco FC na Rhino Rangers, ambapo zaidi ya wachezaji 20 kutoka Ligi Kuu watazitumikia timu za daraja la kwanza msimu huu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles