27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

WANASIASA WATUMIA KAMPENI ZA UDIWANI KUTEMA NYONGO

Na AGATHA CHARLES – DAR ES SALAAM

KAMPENI za uchaguzi mdogo wa udiwani zinazoendelea katika kata 43 nchini, zimegeuzwa kuwa majukwaa ya mikutano ya vyama vya siasa iliyokosekana kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa baada ya kuzuiwa.

Wanasiasa kutoka vyama vyote vyenye wagombea katika uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Novemba 26, wamekuwa wakitumia muda mrefu katika kampeni hizo ‘kutema nyongo’, wakizungumza hoja zinazohusu mwelekeo wa nchi, hali ya siasa ilivyo na kukosoa baadhi ya mambo, huku muda kidogo ukitumika kunadi wagombea.

Vyama vyenye wagombea katika uchaguzi huo ni Chama Cha Mapinduzi (CCM), Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na ACT-Wazalendo.

Hali hiyo inatokea baada ya Juni, mwaka jana Rais Dk. John Magufuli kupiga marufuku vyama vya siasa kufanya ushindani wa kisiasa katika mikutano ya hadhara hadi mwaka 2020.

Marufuku hiyo ya Rais Magufuli, ilikaziwa Novemba, mwaka jana na Jeshi la Polisi baada ya kuzuia mikutano na maandamano ya vyama vya siasa.

Kutokana na sababu hiyo, makada, wanachama na wafuasi wa vyama vyenye wagombea, wamekuwa wakijitokeza kwa wingi katika mikutano hiyo ya kampeni, kuwasikiliza viongozi wao baada ya kutowaona kwa muda katika majukwaa ya mikutano ya hadhara.

Katika mikutano mbalimbali ambayo viongozi wa ngazi za juu wa Chadema, wakiwamo Mwenyekiti Freeman Mbowe, Mjumbe wa Kamati Kuu, Edward Lowassa na Mwenyekiti wa Kanda ya Pwani, Frederick Sumaye, walienda kuwanadi na kuwaombea kura wagombea wao wa nafasi za udiwani, pia walitumia majukwaa hayo kuzungumzia masuala mbalimbali ya nchi.

EDWARD LOWASSA

Akiwa Kata ya Moita jijini Arusha, Lowassa, alikumbusha mjadala wa Katiba mpya kwa kumwomba Magufuli kusikiliza maoni ya watu.

Katika hoja hiyo, Lowassa alisema nchi itakwenda vyema iwapo itakuwa na Katiba bora kama ya Kenya inayoruhusu matokeo ya urais kupingwa mahakamani.

Pia Lowassa alisema hakuna chama kinachotawala peke yake duniani kwa sasa na nchi ina shida ya kitu alichokiita ‘coalition’, yaani muungano wa vyama.

Akitoa mfano huku akirejea matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka juzi, Lowassa aliyepata kura milioni sita na kushika nafasi ya pili nyuma ya Magufuli, alisema kwa nchi nyingine, mwenye kura hizo anapata nafasi ya kuchangia wabunge, huku akitolea mfano Ufaransa kuwa ni nchi ya kibepari, lakini inaongozwa na ujamaa kutokana na aina ya wabunge iliyonao.

Alisema ni bora Katiba ikafuatwa kwa sababu katika muungano, vyama vya siasa ni vingi na ukifika wakati wa uchaguzi, vinatumika vibaya.

Pia alinukuliwa akisema kuwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, Chadema lazima ichukue nchi.

FREEMAN MBOWE

Wakati Lowassa akizungumzia hayo, Mbowe, aliyeanzia Kimara Suka, Dar es Salaam katika Kata ya Saranga, aliomba wanaohamia Chadema kuacha kuambiwa kuwa ni mafisadi na badala yake kama ni kweli wahusika wawafikishe mahakamani kwa hatua zaidi.

Pia Mbowe alizungumzia hatua ya kuzuiwa kwa mikutano ya kisiasa na kudai kuwa si sahihi na Chadema itaendelea kupigania haki hiyo na ikiwezekana kuna siku wataingia barabarani kuandamana.

Katika hatua nyingine, akiwa Mtwara, Mbowe alizungumzia zaidi namna aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa na Mwenyekiti wa CUF anayetambuliwa na ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba, walivyojiengua katika Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka juzi.

Pia hakuacha kugusia mchakato wa upatikanaji wa Katiba mpya kuwa uko pale pale, huku akirejea maneno aliyosema kuwa yalipatwa kuzungumzwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, kuwa kwa Katiba iliyopo mtawala akiamua kuwa dikteta anaweza kutokana na madaraka makubwa ya rais.

MWIGULU NCHEMBA

Kwa upande wake, Mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM, Mwigulu Nchemba, akiwa katika Kata ya Saranga, Dar es Salaam, aliwashangaa wanaodai kuna utawala wa kidikteta nchini na alisema watu hao wameshindwa kutofautisha dhana hiyo na utawala wa sheria.

Katika hoja hiyo, Mwigulu ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, alisema Magufuli anajali zaidi utawala wa sheria na ndiyo sababu aliamua kuwa na mahakama ya mafisadi, huku akisimama kuwatetea wanyonge.

Pia alitaka maneno ya wanasiasa wa upinzani kupuuzwa, huku akidai kuwa Magufuli analazimika kuwa mkali kutokana na uonevu dhidi ya wanyonge.

TUME YA UCHAGUZI

Kutokana na mwenendo na hoja za wanasiasa hao, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilivionya vyama vya siasa kutogeuza kampeni za uchaguzi huo kuwa mikutano ya vyama vya siasa.

Onyo hilo lilitolewa mwanzoni mwa wiki hii na na Mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijage.

Jaji Kaijage, alisema vyama vya siasa vinatakiwa kufanya kampeni kwa kuzingatia maadili na taratibu zilizoainishwa katika uchaguzi kupitia kifungu cha 53 cha Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa sura ya 292.

Pia alisema NEC ina mamlaka ya kuruhusu kampeni za uchaguzi kwa nia ya kushawishi watu na si mikutano ya vyama vya siasa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles