27.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

WANASHERIA WATAKA ROBOTI ZIDHIBITIWE KULINDA AJIRA ZA BINADAMU

 

JOSEPH HIZA Na MASHIRIKA YA HABARI,

UDHIBITI wa kiwango cha juu unahitajika kuzuia roboti kupora ajira za binadamu, hii ni kwa mujibu wa taasisi maarufu ya kimataifa ya wanasheria.

Wataalamu wa sheria wana wasiwasi kuwa kasi ya maendeleo ya mashine hizo za kielektroniki zenye akili kama ubongo wa kibinadamu (AI) ina athari hasi pia.

Wanasema kasi hiyo inatishia na kupiku uwezo wa serikali duniani kutengeneza sheria za kukabiliana na athari zinazotokana na maendeleo ya mashine hizo za kutengenezwa.

Pia wana wasiwasi kuwa hilo linasababisha pengo kati ya sheria za sasa na zijazo- ikiwamo 'idadi stahili za ajira za binadamu zinazopaswa kulindwa– kwamba wanahisi ni lazima kuwalinda watu dhidi ya kuporwa kwa ajira zao na mashine hizo.

Chama cha Kimataifa cha Wanasheria (IBA) kimetoa ripoti ikioredhesha tishio kwa ajira za watu linaloletwa na mashine hizo.

Wanasheria wana wasiwasi kuwa maendeleo ya mashine zenye bongo (AI) yanakuja kwa kasi kuliko namna, ambavyo serikali za kidunia zimejipanga kushughulika na sheria na athari za mwelekeo huo.

Chama hicho cha wanasheria kinaonya theluthi moja ya ajira za wahitimu wa vyuo duniani zinaweza kutwaliwa na mashine hizo zenye akili.

Miongoni mwa ajira zilizoelezwa kuwa hatarini katika ripoti hiyo yenye kurasa 120 ni pamoja na zile zenye kuajiri watu wengi kama vile uhasibu na ukarani wa mahakama.

Ripoti ya IBA inatoa mapendekezo kadhaa ili kulinda ajira za binadamu zisipotee kwa ‘viumbe’ hao wa kutengenezwa.

Mapendekezo hayo ni pamoja na kuhakikisha uwapo wa kiwango cha chini cha ajira za watu kinachopaswa kutovukwa katika sekta husika.

Madai hayo yanakuja katika ripoti mpya kutoka IBA, ambayo hujikita katika athari za maendeleo ya teknolojia.

Maendeleo hayo ya haraka yamechagia mapinduzi ya nne ya viwanda –maarufu ‘Industry 4.0’ –ambayo IBA inasema yanatishia kufanya theluthi mbili ya ajira za wahitimu wa vyuo vya elimu ya juu kunyakuliwa.

Neno ‘Industry 4.0’ linamaanisha mjumuisho wa kiufundi wa mifumo ya AI katika uzalishaji na lojistiki.

Pia linahusisha matumizi ya vitu vya intaneti  – muunganiko wa takwimu baina ya vitu vya kila kitu.

Waraka huo wenye kurasa 120 unaeleza uwezekano wa mabadiliko yatakayoletwa na AI katika siku za usoni na uwezekano wa athari katika mifumo iliyopo katika mahali pa kazi.

Pia inatabiri kuonesha kwamba bidhaa zilizotengenezwa na binadamu – kuwapatia wateja chaguo la kuunga mkono sekta ya bidhaa zilizotengenezwa na binadamu– pamoja na kuzitoza kodi kubwa kampuni za AI katika biashara zao.

Udhibiti wa kina pia utahitajika kuzuia ajali, majeraha na hata vifo vinavyoweza kusababishwa na AI katika mahala pa kazi.

Na tunaweza hitaji fikira za kina kwa aina ya ajira ambazo tusingependa roboti zifanye – ikiwamo kulea watoto wachanga na wadogo.

Mratibu wa ripoti wa IBA, Gerlind Wisskirchen anasema: “Kiuhalisia mapinduzi ya teknolojia si kitu kipya, lakini huko nyuma kilikua kikienda taratibu.

Hii si mara ya kwanza kuwapo vitisho vya AI kwa ajira na kuzua mijadala na vichwa vya habari.

Ripoti hiyo iliyochapishwa Machi mwaka huu ilibaini kuwa asilimia 38 ya ajira nchini Marekani zitachukuliwa na AI ifikapo mwanzoni mwa miaka ya 2030.

Ndani ya kipindi cha miaka mitano ijayo, inatarajiwa kwamba mashine zaidi ya bilioni 50 zitakuwapo kote duniani kwa mujibu wa ripoti ya utafiti huo ulioendeshwa na taasisi ya Price Waterhouse Coopers (PWC) yenye makao makuu London, Uingereza.

Mapinduzi ya awali ya viwanda yalipangwa katika makundi ya nguvu ya mvuke na utengenezaji mashine; mwanzo wa kuelekea nguvu za umeme mwishoni mwa karne ya 19 na kusambaa kwa kompyuta na intaneti kuanzia miaka ya 1970 na kuendelea.

“Kilicho kipya kuhusu mapinduzi haya ya sasa ni kasi ambayo mabadiliko yanatokea na upana wa athari zinazoletwa na AI na roboti.

Uchambuzi unafichua kwamba ajira za huduma za kifedha uko katika hatari kubwa zaidi na asilimia 61 zinaweza kuchukuliwa na mashine hizi. Ilibaini pia asilimia 30 ya ajira za Uingereza, asilimia 35 ya ajira za Ujerumani na asilimia 21 ya ajira za Japan ziko katika hatari.

PwC iligundua kwamba Marekani na Uingereza zina kiwango karibu sawa cha hatari wakati ujao, lakini sekta katika nchi hizo zitakazoangukia mikononi mwa wafanyakazi mashine hizo ni tofauti.

PWC ilisema kwamba wafanyakazi wa sekta za kifedha na bima nchini Marekani hujikita zaidi katika soko la rejareja la ndani na wana kiwango cha chini cha elimu kulinganisha na wataalamu wa Uingereza.

Wengi wa wafanyakazi nchini Uingereza wako katika hatari kubwa katika sekta za usafirishaji na uhifadhi, rejereja, uzalishaji na utawala na huduma, wataalamu walibaini.

Ripoti inasema ajira milioni 10.4 ikiwa ni asilimia 30 ya zile za Uingereza zinatarajia kuporwa ifikapo mapema miaka ya 2030.

Ripoti nyingine iliyotolewa mapema mwaka jana ilionya umwagaji wa mashine hizo kwa wingi mahali pa kazi.

Ripoti hiyo ya asasi ya kimataifa ya ING-Diba, ilisema kuruhusu hilo wanadamu hawataweza kushindana nazo kwa vile si tu zitaongeza ufanisi, kufanya kazi saa nyingi bila kuchoka bali pia kupunguza gharama za kuajiri wanadamu.

Kumbuka pia roboti moja huweza kufanya kazi ya watu wengi kwa wakati mmoja.

Kwa kufanya hivyo sekta mbalimbali zitaongeza mapato na faida kubwa kulinganisha na ile ambayo ingezalishwa iwapo wafanyakazi ni wanadamu.

Ilisema hilo ni jambo zuri kiuchumi kwa sekta husika lakini baya kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya mtu mmoja mmoja ambaye ajira iliyochukuliwa na roboti ingemsaidia kuondokana na matatizo yanayosababishwa na kuikosa.

Kwa mujibu wa ING-Diba, asilimia 59 ya nguvu kazi ya Ujerumani itaondoshwa kutoka soko la ajira na mashine hizo miongo michache ijayo.

Kwa maana hiyo, karibu theluthi mbili ya nguvu kazi yake itakosa ajira. Kati ya watu milioni 30.9 ambao kwa sasa wana ajira ya kudumu au ya muda nchini Ujerumani, milioni 18 wataporwa ajira zao na ujio wa teknolojia hizo zilizoboreshwa zaidi, ripoti imedai

Ijapokuwa utafiti umetazama zaidi athari ambazo teknolojia zilizoboreshwa zitaleta mahali pa kazi katika nchi kadhaa ikiwamo Finland na Uholanzi, ni Ujerumani ambayo inaonekana itaathirika zaidi.

Utafiti unadai kuwa hiyo ni gharama, ambayo Ujerumani inatarajia kuilipa kwa kubarikiwa na sekta yenye nguvu ya viwanda barani Ulaya.

Kwa mfano, wafanyakazi wa viwanda na maeneo ya utawala katika viwanda vikubwa vya magari na vifaa kama vile Volkswagen na BMW haitachukua muda watapukutishwa na mashine zilizoboreshwa zaidi, ambazo zitafanya kazi zao kwa haraka na kwa ufanisi zaidi.

Wafanyakazi wa utawala kama vile makatibu muhtasi, wa mapokezi wanatarajia kujikuta kazi zao zikichukuliwa na roboti. Asilimia 86 yao watapoteza ajira kwa teknolojia hizo, utafiti umedai.

Habari ni mbaya pia kwa mafundi makenika, waratibu na mafundi wa mashine hizo, ambao pia wanatarajia nafasi zao kuchukuliwa na teknolojia mpya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles