30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Wanasayansi 250 waandika waraka wadai spika za masikioni chanzo cha saratani

HASSAN DAUDI NA MASHIRIKA YA HABARI

SPIKA za masikioni zisizounganishwa na waya (wireless headphones), zimetajwa kuwa moja kati ya vyanzo vya ugonjwa hatari wa saratani, kwa mujibu wa wataalamu wa afya.

Teknolojia hiyo iliyoanza miaka ya hivi karibuni, imejizolea umaarufu mkubwa ulimwenguni kote, ambapo watu wapatao milioni 28 wameshafikiwa nayo.

Huku biashara ikionekana kuwa nzuri kwa kampuni ya Apple, wanasayansi 250 wamefikisha malalamiko yao kwa Shirika la Afya la Kimataifa (WHO), wakilitaka kusimamia usitishaji wa matumizi ya spika hizo za masikioni.

Wanacholilia zaidi wataalamu hao ni kwamba vifaa hivyo vina mawimbi-redio aina ya electromagnetic frequency (EMF), ambayo huzalisha joto linaloathiri ukuaji wa chembe hai za damu za binadamu.

Aidha, kinachowatia hofu ni ukaribu uliopo kati ya ‘wireless’ hizo na fuvu la kichwa, wakiamini inaweza kuwa na madhara kwa afya ya mtumiaji.

Katika mahojiano yake na kituo cha televisheni cha Medium, Profesa wa Chuo Kikuu cha Colorado, nchini Marekani, Jerry Phillips, anasema:

“Wasiwasi wangu ni kwamba, zinavyowekwa katika sikio, zinaifanya mishipa ya kichwa kuwa karibu zaidi na mionzi.”

Mwanasayansi huyo ni mmoja kati ya wale 250 walioiomba WHO kusitisha mara moja matumizi ya teknolojia hiyo, ambapo katika waraka wao wanaelezea kuwa mbali ya saratani, mionzi ya spika hizo za ‘wireless’ inaharibu vinasaba (DNA) vya mtumiaji.

“Mashirika mbalimbali yanayohusika katika viwango vya usalama yameshindwa kuweka vizingiti vya kuilinda jamii, hasa watoto ambao ndio wepesi kukumbana na madhara haya ya EMF,” inasomeka sehemu ya waraka huo.

“Kwa kutochukua hatua, WHO imeshindwa kutekeleza wajibu wake, ikiwa ndiyo taasisi yenye dhima ya afya duniani.”

Kwa upande wake, kampuni ya Apple, ambayo kimsingi ndiyo wazalishaji wa teknolojia hiyo ya spika za masikioni, wamejitetea kwa madai kuwa vifaa vyao vimetengenezwa kwa kufuata vigezo vyote kwa masilahi ya afya ya watumiaji wake.

Wakati huo huo, si wanasayansi wote wanaokubaliana na waraka wa wanasayansi hao 250 kwani Profesa wa Chuo Kikuu cha Pennsylvania, Kenneth Foster, anasema hakuna madhara yanayosababishwa na mionzi iliyopo katika spika za masikio zisizo na waya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles