25.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Wanaodaiwa kujimilikisha nyumba za umma mikononi mwa DCI

Leonard Mang’oha -Dar es salaam

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, amemtwisha Mkurugenzi wa Mashtaka (DCI) jukumu la kufuatilia watu waliojimilikisha nyumba za mashirika mbalimbali ya umma kinyume cha sheria wakiwamo watu wawili wanaodaiwa kujimilikisha nyumba hizo katika eneo la Morocco na Upanga jijini Dar es Salaam.

Lukuvi alitoa maagizo hayo Dar es Salaam jana alipotembelea nyumba ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) eneo la Morocco Square inayodaiwa kumilikiwa kinyume cha utaratibu na raia mmoja wa Ghana pamoja na Shirika la Bima la Taifa (NIC) iliyopo kata ya Upanga ambayo inadaiwa kubadilishwa umiliki licha ya kuwapo zuio la mahakama.

Kuhusu nyumba iliyopo Morocco Square Waziri Lukuvi alieleza kuwa mtu anayedaiwa kumiliki nyumba hiyo alikuwa mpangaji wa NHC lakini baadaye taarifa zikanesha kuwa yeye ndiyo mmiliki wa nyumba hiyo, umiliki ambao alidai kuwa una utata.

“Sasa nimeagiza watu wa shirika la National Housing wamfuatilie naona wanachelewa lakini jambo lenyewe naona liko nje ya uwezio wao. Sasa nataka ninyi (ofisi ya DCI) mumfuatilie, kwa sababu ana mikataba ya kupanga mara ya kwanza kama mpangaji wa Shirika la Nyumba la Taifa lakini baadaye inaonekana ameuziwa.

“Katika process hiyo kuna majina mengine utakuta makubwa kidogo yameshiriki katika jambo hili lakini msijali lazima irudi serikalini. Kwa hiyo nimekuja kukuonesha na kukukabidhi kazi hii DCI kuanzia leo ufanye uchunguzi hii nyumba kwanini imehama mkono kutoka Shirika la Nyumba hadi kwa mtu binafsi na mtu binafsi mwenyewe ni mgeni kutoka Ghana,” alisema Waziri Lukuvi.

Waziri Lukuvi aliitaka ofisi ya DCI kuhakikisha watu waliohusika kummilikisha raia huyo wa kigeni nyumba hiyo wanashughulikiwa hata kama wanatoka NHC, serikalini au katika wizara yake.

Akiwa katika eneo la Upanga, Waziri Lukuvi aliiagiza ofisi ya DCI kufuatilia umiliki wa nyumba hiyo iliyouzwa kwa Sh milioni 130 licha ya thamani yake halisi kuwa zaidi ya Sh bilioni 1.2.

“Sasa hawa wenzetu wa Jeshi la Polisi wanao uzoefu wa kuchunguza nataka wachunguze ilikuwaje pamoja na kuwapo zuio la mahakama kwamba nyumba isiuzwe, pamoja na kwamba Serikali imelipa na uuzaji ukaendelea lakini pia watu wangu waliohusika kwanini waliendelea kuuza wakijua kuna amri ya Mahakama.

“Kwa hiyo Jeshi la Polisi nawakabidhi leo ili wachunguze hii nyumba ya Serikali, lazima hii nyumba ya irudi serikalini na kwangu mimi itakuwa ni mara ya pili kwa huyu na bado kuna watu wanatajwatajwa,” alisema Waziri Lukuvi.

Waziri Lukuvi aliliitaka ofisi ya DCI kuhakikisha wote waliohusika kulimikisha nyumba hiyo ambao alidai kuwa wanapatikana ofisini kwake washughulikiwe huku akisisitiza kuwa nyumba hizo ni mfano kwani atamkabidhi DCI orodha ya majina ya watu wengine wanaojimilikisha nyumba za umma.

Katika hatua nyingine Lukuvi aliagiza kuchukuliwa hatua watu wote walioanzisha mashirika madogo ndani ya NHC na kuyatumia kupangisha nyumba za shirika hilo badala ya shirika lenyewe.

Akielezea uhalali wa umiliki wa nyumba hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Bima la Taifa (NIC), Dk. Elirehema Doriye, alisema kuwa mwaka 1996 shirika hilo lilipelekwa mahakamani likidaiwa Sh milioni 10 ambapo Agosti mwaka 2006 kesi hiyo hiyo iliyosikilizwa kwa upande mmoja na Mahakama ilimpa ushindi mdai.

Dk. Doriye alisema kutokana na uamuzi huo wa mahakama Septemba mwaka huo huo shirika lililipa kiasi hicho cha fedha kupitia akaunti namba ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kupewa stakabadhi ili kuzuia nyumba hiyo isiuzwe, lakini Oktoba mwaka  huohuo ikapigwa mnada na kununuliwa na kampuni ya Ham Import and Export kwa Sh milioni 130.

“Wakati huo inauzwa ilikuwa na thamani ya Sh Bilioni 1.2 lakini mwezi wa 11 shirika likapeleka Wizara ya Ardhi zuio kwamba hati ya nyumba hiyo isihamishwe kwa kutoka kwa shirika kwenda kwa mtu binafsi, pia mwezi wa 12 Mahakama ikaridhia kuzuia kuuzwa kwa nyumba hii lakini mwaka 2007 Aprili nyumba hii ikabadilishwa title na ikahamia kwa mmiliki wa mnunuzi.

“Lakini kwa kuwa wakati huo shirika lilikuwa katika harakati za kubinafsishwa haikufuatiliwa tena mpaka hivi karibuni nilipomwona waziri na kumwonesha nyaraka ambazo tunazo na wizara inazo ndiyo maana tuko hapa,” alisema Dk. Doriye. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles