23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Wanane mbaroni kwa ubakaji, mauaji ya wanawake

Na JANETH MUSHI-ARUSHA

JESHI la Polisi Mkoa wa Arusha linawashikilia watu wanane wanaodaiwa kuhusika na matukio ya ukatili ya ubakaji na mauaji ya wanawake katika Kata ya Olasiti, huku baadhi yao wakidaiwa kukutwa na vielelezo ikiwemo simu za mikononi za marehemu.

Wakati jeshi hilo likiwashikilia watuhumiwa hao, baadhi ya wananchi wa kata hiyo, wameendelea kutoa kilio chao kwa serikali kutokana na hofu ya usalama wao inayosababishwa na kukithiri kwa matukio hayo katika eneo hilo.

Akizungumza na MTANZANIA Jumapili, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha, Jonathan Shanna,  alisema kuwa watuhumiwa hao wamekiri kuhusika na matukio hayo ambapo wengine wamekutwa vielelezo zikiwamo simu za mkononi za marehemu.

“Hadi sasa tumeshakamata watuhumiwa wanane wakiwa na vielelezo ikiwemo simu za marehemu na wamekiri kuhusika na matukio hayo. Tukikamilisha upelelezi tutapeleka jalada kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili wafikishwe mahakamani na tunaendelea na ulinzi katika eneo hilo ili kukomesha vitendo hivyo,” alisema Kamanda Shanna

KILIO CHA WANANCHI

Kwa upande wao baadhi ya wanawake wakizungumza na gazeti hili kwa masharti ya kutokutajwa majina yao kwa kuhofia usalama wao, walidai matukio hayo yanahusishwa na imani za kishirikina.

Mbali na hilo pia mauaji hayo kuhusishwa na imani za kishirikina, wengine wanadai kuwa ulevi na matumizi ya dawa za kulevya kwa baadhi ya vijana ni miongoni mwa sababu zinazoweza kuchangia kukithiri kwa matukio hayo.

“Matukio haya mengine yanahusishwa na imani za kishirikina kwamba kuna vijana wanatafuta vizazi vya wanawake na ndiyo maana wanawabaka kabla ya kuwauwa kisha wanachukua vizazi vyao,inadaiwa wanatafuta utajiri.

“Kiukweli wakiuwawa wale watu wanawekwa uchi wa mnyama kama tulivyowaambia maiti zinakuwa uchi,huku ni zaidi ya kudhalilisha na kuogopesha kwani wakati mwingine watoto wadogo hushuhudia matukio hayo na kukuta miili ya wamama hao ikiwa uchi wa mnyama,” alidai mmoja wa wanawake wa Mtaa wa Burka 

Alidai kuwa kukithiri kwa matukio hayo kunatishia usalama wa wanawake kwani hawajawahi kusikia wanaume wakikumbwa na matukio hayo katika eneo hiyo.

“Kiukweli licha ya kuwa mwenyeji wa eneo la Olasiti, matukio haya yanatutisha sana hasa sisi ambao tuna watoto wa kike, tunaumia na tunahofia sana na tunaambiwa huwa yanatokea kuanzia jioni hadi alfajiri hatujawahi kusikia yametokea mchana,” alisema 

Walidai kuwa ni muhimu kuendelea kuwepo vikao kwa ajili ya kuimarisha ulinzi kwani ikifika usiku watu huhofia kutoka nje ambapo kwa mwaka huu inadaiwa tukio la kwanza lilitokea Machi ambapo mwili wa marehemu ulikuwa eneo la Burka, lingine shamba la Kambaine eneo la mwisho wa Hiace Olasiti, mwingine kukutwa pembezoni mwa Mto Burka.

KAULI YA DIWANI

Naye Diwani  wa Olasiti, Alex Martin (CCM), alisema katika kipindi cha kuanzia mwaka jana hadi sasa wanawake saba walibakwa na kuuawa katika kata hiyo yenye mitaa mitano.

Alisema kutokana na hali hiyo kwa sasa wanalazimika kutoa elimu kwa jamii kupitia mikutano ya hadhara ikiwemo ya kuanzisha ulinzi shirikishi kupitia ulinzi wa jadi (sungusungu) kwa kushirikiana na polisi.

“Idadi kwa sasa wamefika saba, ndani ya kata yetu peke yake ni idadi kubwa ila hivi karibuni imeongezeka zaidi kwani kwa mwaka huu pekee wanawake wanne walibakwa na kuuwawa tena kwa kipindi cha karibu karibu. Japo kuna mwingine naye hivi karibuni alifanyiwa vitendo hivyo katika eneo la Darajani, Kata ya Osunyai ambapo ni jirani kabisa na sisi,” alidai.

Alisema mwishoni mwa wiki iliyopita walifanya mkutano wa hadhara ambapo aliwasihi wananchi wa eneo hilo kutoka nje wanaposikia kelele kwani licha  na baadhi ya matukio hayo kutokea usiku, watu wanaposikia kelele hushindwa kutoka nje.

Alitaja mkakati mwingine waliojiwekea katika kupunguza na kumaliza matukio hayo ni pamoja na wenye nyumba kufahamu wapangaji wao ikiwa ni pamoja na shughuli wanazofanya ili waweze kulindana.

MTO WA MBU

Hilo ni eneo la pili kukumbwa na matukio hayo ya kikatili mkoani Arusha ambapo eneo la Mto wa Mbu wilayani Monduli, ambapo kuanzia mwaka jana hadi mwanzoni mwa mwaka huu kuliibuka matukio hayo ambapo Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola alilitaka Jeshi la Polisi kuhakikisha linafanya uchunguzi wa kina na kukamata wahusika wa vitendo hivyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles