30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

WANANCHI WALILIA SHULE YA CHEKECHEA

Na LILIAN JUSTICE-MOROGORO

WAKAZI wa Kitogoji cha Misufini, Kata ya Bwakila Chini wilayani Morogoro, wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa shule ya awali.

Kutokana na hali hiyo, wananchi hao wanalazimika kuwaanzisha darasa la kwanza watoto wao wakiwa na umri mkubwa.

Malalamiko hayo yalitolewa na wananchi hao walipokuwa wakizungumza na MTANZANIA katika kitongoji chao.

Baadhi ya wananchi hao, Monica Koa, alisema kitendo cha kitongoji hicho kutokuwa na shule ya awali kinaathiri watoto wao kwa kuwa wanakosa elimu waliyotakiwa kuipata.

“Hii elimu ya awali ni muhimu kwa watoto wetu, lakini tunasikitika hawaipati kwa sababu hatuna shule ya elimu hiyo.

“Yaani kutokana na tatizo hilo, tunalazimika kuwapeleka watoto wetu shuleni wakiwa na umri mkubwa, jambo ambalo halifai kwa maendeleo ya watoto,” alisema Koa.

Naye Akimu Kipayu, aliunga mkono hoja hiyo na kuitaka Serikali ifanye kila linalowezekana ili kitongoji chao kiwe na shule hiyo ya awali.

“Tunaiomba Serikali ituangalie kwa jicho la pekee kwa sababu ukosefu wa shule hii, unaathiri watoto wetu kwani elimu ya awali ni muhimu sana kwao,” alisema.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Bwakila Chini, Pesa Mohamad, alisema tayari ameshaitisha kikao na wafugaji wa kitongoji hicho na kuwashauri kuuza ngombe wachache ili waweze kujenga jengo la shule ili kuondokana na kero hiyo.

“Ni kweli hilo tatizo lipo ndiyo maana nililazimika kuitisha kikao cha wafugaji na kuwaeleza umuhimu wa kujenga shule hiyo badala ya kuisubiri Serikali iwajengee.

“Katika hili, niliwashauri wajitolee kuuza ng’ombe hata watatu ili fedha zitakazopatikana, zianze rasmi ujenzi wa shule ya awali kwa ajili ya watoto  kusoma  mapema wakiwa na umri wa miaka mitano au sita,” alisema diwani huyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles