27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Wananchi wajengwe kisaikolojia kukabili corona

Na FARAJA MASINDE-DAR ES SALAAM

KIPINDI hiki kinaweza kutafsiriwa kama moja ya nyakati ngumu kuweza kupitiwa na dunia ukiachailia mbali vita kuu ya dunia iliyowahi kutokea karne kadhaa huko nyuma.

Hatari hii ni kutokana na kuendelea kuwapo kwa maambukizi ya virusi vya corona ambavyo wakati vikianza mwishoni mwa mwaka jana, huko katika jimbo la Hubei nchini China, ilichukuliwa kama ugonjwa wa muda mfupi ambao huenda ulisababishwa na baadhi ya tamaduni za taifa hilo kupenda kula vyakula ambavyo ni vigumu kukuta vikiliwa na raia wa mataifa mengine.

Lakini jambo la kushtua ni kwamba kadiri muda ulivyokuwa ukizidi kwenda ndipo dunia ilipoanza pia kushtuka na kuhamaki baada ya kuona virusi hivyo vikizidi kuenea kila kukicha na kuleta hatari zaidi katika kila pembe ya dunia.

Jambo la kushtua zaidi ni kuwa Tanzania nayo imekuwa miongoni mwa nchi zilizopoteza mpendwa wao kutokana na virusi hivyo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa mapema wiki hii Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, ilileza kuwa kifo hicho ni cha mwanaume (47) kilichotokea katika kituo cha matibabu cha wagonjwa wa (Covid-19) kilichoko Mloganzila.

Ni jambo la kushukuru kuona kuwa serikali imeendelea kuchukua hatua stahiki za kuhakikisha kama taifa tunakabiliana na janga hili hatari.

Miongoni mwa hatua hizo ni pamoja na ile ya kufunga shule na vyuo kwa muda wa siku 30 na ile ya kuhakikisha kuwa magari ya abiria yanakuwa na idadi ya watu walioketi kwenye viti tu  ikiwamo ile ya kila sehemu kuwa na maji na sabuni kuhakikisha watu wananawa mikono ili kupunguza maambukizi.

Lakini wakati hali ikiwa hivyo nchini Tanzania, mambo ni tofauti kwenye mataifa mengine jirani kama Kenya, Uganda na hata Afrika Kusini ambako mamlaka za nchi hizo kutumia nguvu kuhakikisha kuwa raia wake wanasalia majumbani ili kujikinga na maambukizi ya virusi hivyo.

Mwishoni mwa juma lililopita picha zilisambaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii zikionyesha namna ambavyo askari walivyokuwa wakipambana na raia kuhakikisha wanatekeleza agizo la serikali la kusalia majumbani.

Hata hivyo uamuzi huu kwa sasa unatazamwa kama tatizo ndani ya tatizo hatua ambayo inaweza kuongeza hatari zaidi ya mlipuko wa virusi hivyo.

Kwani kwa nguvu kubwa ambayo inachukuliwa na mamlaka husika katika kuwatawaywa kwa kuwapiga baadhi ya wale wanaokaidi agizo la serikali kitendo kinachotafsiriwa kuwa ni sawa na kuzalisha chuki nyingine miongoni mwa raia.

Hivyo badala ya raia kunza kupambana na virusi vya corona badala yake wataanza kupambana na serikali hatua ambayo inaweza ikaibua hatari kubwa kwani nguvu nyingi watazielekeza kwa serikali na kusahau kuchukua hatua muhimu ya kujikinga na virusi vyenyewe.

Ilikuwa ni jukumu la serikali kuweza kuwajenga kisaikolojia raia wake juu ya janga hili uamuzi ambao ungeweza kuelekeweka kwa haraka kuliko kutumia nguvu ambayo kwa namna moja ama nyingine ikitokea mmoja wa wazua gasia ana virusi basi inakuwa ni ngumu kwa watu kuweza kupona kwani wanaweza kuandamana kwa makundi.

Hivyo sasa inafanya adui mkubwa wa raia hao kuwa serikali na si corona hatua mbayo haina tija.

Tumeshuhudia mataifa kama Italia ambayo baada ya kuona changamoto ya ugonjwa huo imekuwa kubwa walitumia akili kuhakikisha kuwa wanawatuliza raia wao nyumbani licha ya kwamba idadi ya vifo bado iko juu lakini kwa namna moja ama nyingine imeweza kuwa na manufaa.

Uamuzi ambao pia tuliushuhudia ukichukuliwa na Taifa la China kuwatuliza raia wake na hatimaye maambukizi yemeanza kupungua.

Binafsi napongeza mbinu na hatua ambazo zimekuwa zikitumiwa na Serikali ya Tanzania hususan Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, ambaye kwa nafasi yake amekuwa akijitahidi kuwajenga Watanzania kisaikolojia juu ya hatari ya ugonjwa huu hatua ambayo imeleta ahueni ikilinganishwa na hofu iliyokuwapo awali.

Pia kwa mlengo uleule tumeona kwa nyakati tofauti Rais Dk. John Magufuli alipokuwa akiongea na taifa juu ya virusi hivyo akiwaondolea hofu Watanzania hatua ambayo imekuwa na matokeo chanya zaidi.

Virusi hivyo vinazidi kumaliza raia katika hatua ambayo tunashuhudia mataifa makubwa kiuchumi kama vile China na Marekani yakiendelea kuzozana.

Rais wa Marekani, Donald Trump, amekaririwa kwa nyakati tofauti akisema kuwa hivyo ni virusi vya China na kwamba vimetengenezwa, huku China nayo ikisema virusi hivyo vimezuka hatua ambayo imewaacha wengi njia panda.

Virusi hivyo vimesababisha masuala mengi ya kisiasa kusitishwa ikiwamo mikutano kwani mapema mwaka huu tumeshuhudia Chama cha Kikomunisti cha China (CCP) ambacho ni chama kikuu nchini humo kikiahirisha mkutano wake mkuu wa mwaka.

Nchini Marekani tayari tumeshuhudia namna ambavyo kumekuwa na mageuzi makubwa katika kufanya kampeni huku ikielezwa kwamba virusi vya corona huenda vikaathiri kwa kiwango kikubwa kampeni za mwaka huu ikikumbukwa kuwa nchi hiyo iko mbioni kufanya uchaguzi wake mkuu.

Kwa upande wake Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. George Kahangwa, anasema changamoto hiyo inaonyesha picha halisi ya maisha ya watu wengi hususan barani Afrika kwani kuna pengo kubwa kati ya watu wenye nacho na wasionacho ukinganisha na mataifa mengine.

“Mfano wenzetu wa mabara mengine wamefanikiwa kwenye hilo kutokana na uchumi wa watu wao kuwa mzuri na hata msaada wa serikali zao umekuwa mkubwa, tofauti na Afrika ambapo viongozi wengi wanaiga mfumo huo kuuleta hapa wakati hata uwezekano wa kuweza kutoa huduma zinazotafutwa na watu hao walau kwa mwezi mmoja ni changamoto.

“Kungekuwa na uwezekano basi kukawa na kikosi maalumu ambacho kingeweza kusambaza chakula angalau mara moja kwa wiki, lakini bado ni changamoto kwamba wapo baadhi ya watu ambao hata makazi yao ni shida, hivyo hata upataji wa msaada ni ngumu.

“Kwa hivyo janga hili libaki kuwa fundisho kwa viongozi wa Afrika juu ya kuweka miundombinu inayofaa kwa raia wake ili hata inapotokea changamoto kama hii unakuwa na namna nzuri ya kuweza kuwamudu watu kuliko ilivyo hivi sasa. Wengi wanategemea kutoka majumbani mwao ndiyo mkono uweze kwenda kinywani, kwa namna hiyo ukimwambia abaki itakuwa ni ngumu kukuelewa,” anasema Dk. Kahangwa.

Anasema suala la kutulia nyumbani kwa baadhi ya watu linawezekana na kwa wengine haliwezekani, kwani wapo watu ambao wanaweza kuishi hata mwezi mzima bila  kufanya kazi na maisha yakaenda lakini kwa wengine inakuwa ni ngumu.

“Kimsingi unapomwambia mtu wa namna hii ambaye hali bila kutoka akae nyumbani ni sawa na kumchagulia aina ya kifo, aidha afe kwa njaa nyumbani au atoke kwa njia ya corona hatua ambayo inawafanya baadhi kutoka na kwenda kutafuta kula yao, na badala yake kuibua tatizo ndani ya tatizo,” anasema  Dk. Kahangwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles