27 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Wananchi Meatu wasaidiwe tatizo la ukosefu wa maji

MOJA ya habari iliyopewa uzito katika toleo la jana la gazeti hili, ilikuwa ni ile iliyowahusu wakazi zaidi ya 30,000 wilayani Meatu mkoani Simiyu.

Habari hiyo ilipewa uzito kutokana na tatizo kubwa la ukosefu wa maji linalowasibu wananchi hao kwa muda mrefu sasa.

Hali hiyo inatokana na chanzo kikuu cha maji ambacho wanakitegemea kukauka kutokana na ukame mkali uliopo hivi sasa.

Chanzo hicho kutoka bwawa la Mwanyahina kimekauka na kusababisha wananchi wengi kutaabika usiku na mchana kusaka huduma ya maji, bila mafanikio.

Pamoja na hatua kubwa zinazochukuliwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanhuzi (MWANHUZI-UWSSA), hali imezidi kuwa tete kutokana na kuwapo na tope zito lililosababishwa na ukame.

Pamoja na maeneo mengi ya nchi hivi sasa kuwa na mvua za kutosha, hali katika wilaya hii imezidi kuwa mbaya na kusababisha wanafunzi wengi kushindwa kwenda shule kutokana na kuamka kwenda kusaka maji.

Hivi sasa wananchi wanalazimika kushinda kwenye mito wakichimba visima vidogo ili kupata maji ambayo hata hivyo si salama kwa matumizi mbalimbali.

Wapo ambao wao wamelazimika kununua dumu moja la maji lenye ujazo wa lita 20 kwa Sh 1,000 hadi 2,000 kutoka kwa wauzaji wa mtaani, kiwango ambacho ni kikubwa kulingana na hali halisi ya maisha ilivyopanda.

Kwa kweli kama hakutakuwa na juhudi kutoka mamlaka husika, wananchi hawa wataendelea kutaabika.

Tunasema hivi kwa sababu wanatumia muda mwingi kusaka maji, hasa nyakati za usiku ambako wanakutana na wanyama wakali na kuhatarisha maisha yao.

Kwa hakika hii ni hatari ambayo inapaswa kuchukuliwa hatua haraka.

Tunaamini siku zote hakuna binadamu anaweza kuishi bila maji, umefika wakati mamlaka kuangalia njia sahihi ya kuwanusuru wananchi hawa.

Tunasisitiza hili kwa sababu kukosekana kwa maji kuna athari kubwa, ikiwamo ya kutokea kwa magonjwa ya mlipuko.

Uzoefu unaonyesha sehemu nyingi ambazo hazina huduma ya maji, hukumbwa na magonjwa kama kipindupindu na mengi mengine kutokana na kuwapo uchafu mwingi, wananchi kukosa maji ya kusafisha au kuosha vyombo.

Tunatambua Serikali inachukua hatua kubwa kupata suluhu ya tatizo hili, lakini kuna kila sababu ya kuangalia uwezekano wa kuvuta maji kutoka umbali wa kilometa 15 wilayani Kishapu ili kuwasaida wananchi hawa.

Katika hili tunatambua waathirika wakubwa ni wanawake na watoto ambao mchana kutwa wanahaha huku na kule kutafuta maji, bila kujali jua kali linalowaka.

Pamoja na juhudi kubwa zilizochukuliwa na Mbunge wa Meatu, Salum Hamis kupeleka boza la lita 24,000 na kuwagawia wananchi bure, tunasema kunahitajika kupata suluhu ya jambo hili.

Sisi MTANZANIA tunamshauri Mkurugenzi wa Halmshauri hiyo, Fabian Manoza kuwasiliana na Wizara ya Maji ili kupata fedha za kutosha kuchimba visima virefu ambavyo vitasaidia wananchi kuondokana na tatizo hili kila mwaka.

Kwa kufanya hivi kutasaidia kupunguza matatizo  sehemu nyeti kama shule za bweni, hospitali na maeneo mengi muhimu ambayo sasa huduma zinasimama.

Tunamalizia kwa kuushauri uongozi wa mkoa na wilaya kuhakikisha unachukua hatua haraka ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea.

Lakini pia tunawashauri viongozi wetu kuwaelimisha wananchi umuhimu wa kuchimba visima ambavyo tunaamini gharama zake ni kawaida, kwani vikichimbwa vizuri huwa vigumu kukauka tofauti na kutegemea mabwawa kama ilivyo sasa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles