24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

WANAMCHUKIA RAIS BUHARI SABABU WANAPENDA RUSHWA

Rais wa Nigeria, Mohammed Buhari

 

NA HAFIDH KIDO,

HIVI karibuni niliamua kutafuta ukweli kuhusu kinachoendelea nchini Nigeria. Inaonekana kuna hali ya kutokuwa na imani na Rais Mohammed Buhari kutokana na baadhi ya watu kuzuiliwa kula nchi.

Rais Buhari tangu aingie madarakani mwaka 2015 kwa kumzidi kura mpinzani wake Goodluck Jonathan aliyekuwa makamu wa rais kipindi cha Rais Ummar Yar’Adua ambaye alifariki madarakani, amevumishiwa kifo zaidi ya mara nne.
Lakini taarifa zilizovuma zaidi ni mbili; ile ya Januari 22, mwaka huu na Februari 3, mwaka huu pamoja na ile ya Mei 14, mwaka huu. Kitu gani kipo nyuma ya haya yanayoendelea:

Rais mstaafu wa Nigeria, Olusegun Obasanjo, baada ya kupata taarifa za kifo cha Buhari Februari mwaka huu, alisema ni wapuuzi wanaosambaza taarifa hizo.

“Kitu anachohitaji rais wetu ni maombi yatakayomfanya awe imara zaidi na kupona ugonjwa wake. Ikiwa humtaki subiri hadi uchaguzi mkuu ufike umchague unayemtaka na si kumuombea kifo,” alisema Obasanjo.

Raia wa Nigeria wanaoishi Uingereza baada ya kupata taarifa hizi waliudhika na kusema wajinga wachache wanaotaka kendeleza rushwa na matumizi mabaya ya madaraka ndio wanaomchukia Buhari kutokana na misimamo yake.

Wanashangaa kwa kusema wananchi wa Nigeria ni ajabu hawaoni mabadiliko yaliyopatikana tangu Buhari akae madarakani kwa miaka miwili tu.

Kwa upande wa watu wanaomchukia Buhari, wanadai ni bora rais huyo akae pembeni kuangalia afya yake, kwa sababu wananchi wanamchukia kutokana na aliyoyafanya mwaka 1983-85 alipoiongoza Nigeria kwa mkono wa chuma.

Itakumbukwa Desemba 31, mwaka 1983 hadi Agosti 27, mwaka 1985, Buhari ambaye ni mwanajeshi mstaafu mwenye cheo cha Meja Jenerali, alifanya mapinduzi ya kumuondoa Rais Shehu Shagari na kuongoza nchi kibabe kwa miaka miwili, lakini aliporejea kuomba kura mwaka 2015, alisema zama hizi si za kibabe na ataongoza nchi kwa kutumia demokrasia, hata hivyo wale waliowekwa vizuizini na kunyanyasika kipindi cha utawala wake wa kwanza bado wapo na wana maumivu vilevile. Ndio wanaompeleka puta kwa sasa.

Madai wanayotoa ni kuwa Rais Buhari anaishi kifahari, ana ndege binafsi na magari ya anasa na amejiwekea bajeti kubwa kuangalia masilahi binafsi, huku wananchi wanakufa kwa njaa.

Mmoja wa wanaopinga utawala wa Buhari ambaye alificha jina lake halisi na kuweka jina la Philip Thomas, ameandika kwenye mtandao wa kijamii kuwa hadi sasa wananchi wanaishi kwa hofu, uchumi umeanguka na rais hajali kitu.

Vilevile kuna uvunjifu wa haki za binadamu, ubinafsi na sera za ovyo zinazokandamiza watu wa hali ya chini. Hata uhuru wa kujieleza umefinywa.

Mwanaharakati huyo anasema: “Hizi taarifa za kuvumishiwa kifo kwa Buhari inatakiwa zimfungue macho kuwa wananchi wamemchoka, aamue mawili ima kuondoka madarakani au abadili mfumo wake wa kiuongozi.”

Siku kadhaa kabla ya Buhari kuvumishiwa kifo kwa mara ya nne, mhariri mkuu wa gazeti la Vanguard aliandika tahariri Mei 8, mwaka huu ikisema: “Kwa mara ya nne tangu aingie madarakani miaka miwili iliyopita, Rais Buhari amepeleka barua kwa Bunge (NASS) kuwaeleza kuwa amekabidhi madaraka ya urais kwa makamu wake, Profesa Yemi Osinbajo, kwa kutumia kifungu cha 145 cha Katiba ya nchi hiyo, inayotamka kuwa rais akiondoka anamwachia madaraka makamu wake kufanya shughuli zote za kirais.”

Tahariri hiyo ikarejea miaka kadhaa nyuma wakati Rais Ummar YarAdua alipokuwa akienda nje ya nchi kwa matibabu hakuwa akimwachia madaraka makamu wake Goodluck Jonathan, kama anavyofanya Buhari.

Hii ni ishara kuwa YarAdua hakumwamini Jonathan ambaye alikuwa na hamu ya urais na kweli akawa mgumu kuachia madaraka hadi aliposhindwa kwenye sanduku la kura.

Tafsiri yake ni kuwa Buhari amenusa harufu ya watu walio nje ya Serikali kutaka kumpindua, ndio maana anampa mamlaka yote makamu wake ili ailinde nchi kama rais kamili.

Kwa muda mrefu wananchi wamekuwa wakipiga kelele Ikulu itoe taarifa ya afya ya rais wao, kelele zilipokuwa nyingi wiki iliyopita akalazimika kutoa hadharani kwenye sala ya Ijumaa na hata alipowapokea wanawake waliotekwa na Boko Haram, alionekana akizungumza kwa shida.

Mshauri wa Rais katika masuala ya habari, Femi Adesina, alilazimika kuongea na Buhari kwa njia ya simu huku akionyesha ana afya tele baada ya kuvumishiwa kifo Februari mwaka huu.

Lakini hadi leo hakuna chochote kilichozungumzwa. Huenda wakati nikiandika haya labda Adesina anafanya mambo kwa kusaidiana na Tunde Sabiu, msaidizi binafsi wa rais ili kuwaondoa hofu wananchi.

Nilichojifunza hawa wanaomchukia Buhari wanalazimisha kujua afya ya rais ili kama hali yake ni mbaya, basi akae pembeni kwa sababu kikatiba rais anapougua na kushindwa kuongoza nchi lazima akae pembeni.

Ndiyo maana mwaka juzi Rais Jakaya Kikwete alipokwenda nje ya nchi kufanyiwa upasuaji wa Tezi Dume, wananchi walipokea taarifa hizo kwa hofu, bahati nzuri Mkurugenzi wa Habari Ikulu wa wakati huo, Salva Rweyemamu, alifanya haraka kueleza hali ya rais kuwa inaridhisha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles