30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Wanafunzi waanza kurejea vyuoni, Mzumbe waja na utaratibu mpya kuwakinga

 MWANDISHI WETU

AGIZO la Rais Dk. John Magufuli kutaka wanafunzi wote kurejea vyuoni kuanzia Juni 1 mwaka huu limeanza kutekelezwa baada ya wanafunzi wa vyuo mbalimbali kuanza kuwasili vyuoni mwao.

Miongoni mwa vyuo hivyo ni Chuo Kikuu cha Mzumbe ambako baadhi ya wanafunzi wamekwishawasili kuendelea na muhula wa pili wa masomo utakaoanza Juni 1, 2020.

Wanafunzi hao wamerejea baada ya likizo ndefu iliyosababishwa na maambukizi ya virusi vya corona.

Kutokana na hilo baadhi ya wanafunzi waliowasili wameeleza kuridhishwa maandalizi yaliyofanywa na chuo hicho kuwakinga na virusi hivyo. 

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Waandishi wa Habari waliofika chuoni hapo kukagua maandalizi ya maeneo watakayotumia wanafunzi kusomea, Wanafunzi hao wamesema wamefurahishwa na mazingira waliyoyakuta, na hivyo kuwaondoa hofu waliyokuwa wamejijengea kabla ya kufika chuoni hapo. 

“Tahadhari kubwa imechukuliwa, ukifika getini lazima kwanza kupimwa joto la mwili, mbali na uwepo wa vifaa vya kunawa mikono kila sehemu, matangazo ya tahadhari; huku tukisisitizwa kuvaa barakoa muda wote tunapokuwa kwenye mikusanyiko,” alisema Aney Daniel mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Shahada ya Sayansi katika Maendeleo ya Watu

Naye Hassan Salim, Mwanafunzi wa Mwaka wa Tatu anayechukua masomo ya Sayansi na ICT, alisema hana hofu tena na usalama wa afya yake akiwa chuoni hapo kwani maandalizi yaliyopo yanamuhakikishia usalama na kuwataka wanafunzi wenzake kila mmoja kuchukua hatua katika ulinzi binafsi wa afya, na kwamba kwa kufanya hivyo Jamii nzima ya chuo itakuwa salama na masomo yao yatakamilika kama ilivyokusudiwa.

“ Naomba niwatoe hofu wanafunzi wenzangu; kwakweli mawazo niliyokuja nayo na nilichokikuta ni tofauti, niliamua nije mapema nione kwanza hali, lakini kwakweli mazingira ni rafiki sana kwa sisi kusoma na endapo kila mmoja wetu atachukua tahadhari basi usalama ni mkubwa kwetu sote” alieleza.

Awali akizungumza na Waandishi wa Habari waliofika Chuoni hapo kujionea maandalizi ya mapokezi ya Wanafunzi, Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, Rose Joseph alisema Chuo kimezingatia miongozo yote iliyotolewa na Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Wizara ya Afya na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania, kwa kuhakikisha tahadhari zote zinachukuliwa ikiwa ni pamoja na kuandaa kwa wingi vyombo vya maji tiririka, sabuni, vitakasa mikono, elimu pamoja na kuandaa timu ya wataalamu wa afya, watakaotoa huduma kwenye Kituo chao cha Afya.

“Pamoja na kuandaa vipeperushi, mabango, na maelekezo maalumu ambayo yataendelea kutolewa kwa wanafunzi mmoja mmoja kadiri wanavyowasili na wakati wa madarasa, Chuo tumeunda timu maalumu ya kushughulikia janga la Corona, ambayo itakuwa inafanya kazi saa 24 kukagua, kuboresha na kushughulikia changamoto zote zitakazojitokeza, kuhakikisha wanafunzi na watumishi wanakuwa salama.” alisisitiza

Ameziomba Mamlaka zinazohusika na usimamizi wa vyombo vya usafiri wa umma kwa kipindi hiki ambacho wanafunzi wanasafiri kutoka maeneo mbalimbali ya nchi kuelekeza Chuo, kuelekeza wasafirishaji kuchukua tahadhari zote za kuwakinga wasafiri na maambukizi, pamoja na kuwakumbusha wanafunzi kuchukua tahadhari binafsi zinazozingatia kanuni na miongozo ya Afya katika kujikinga na maambuzi wakati wote wanapokuwa safarini. 

Aidha; amewahakikishia wazazi na walezi kutokuwa na hofu kuhusu usalama wa watoto wao kwakuwa tahadhari kubwa imechukuliwa katika kuhakikisha wanakuwa salama wakati wote wakiendelea na masomo.

 “Tuna namba ya simu maalumu kwa ajili ya kutoa taarifa wakati wa dharura, hivyo wanafunzi wataweza kuzitumia iwapo watahisi kuwa na dalili zozote au kuwepo wahisiwa ambao watapelekwa katika kituo maalum kwa vipimo vya awali kabla ya hatua zingine za matibabu kuendelea kama ulivyo mwongozo wa Wizara ya Afya” alisisitiza 

Zaidi ya wanafunzi elfu kumi na moja (11,000) wanatazamiwa kuripoti kwa Kampasi zake zote (Morogoro, Mbeya na Dar-es- salaam) kuendelea na masomo kwa ngazi mbalimbali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles