27.5 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Wanafunzi 618 washindwa kufanya mtihani darasa la saba

TUNU NASSOR NA CHRISTINA GAULUHANGADAR ES SALAAM

JUMLA ya wanafunzi 618 wa Darasa la saba katika Mkoa wa Dar es Salaam wameshindwa kufanya mtihani kwa sababu mbalimbali ikiwamo utoro, vifo na ugonjwa.

Akizungumza na MTANZANIA jijini Dar es Salaam jana, Ofisa Elimu Mkoa huo, Hamis Lissu  alisema idadi hiyo ni sawa na asilimia 0.82 ya watahiniwa wote.

Alisema wavulana wasiofanya mtihani huo ni 385 na wasichana 233 ambapo watoro walikuwa  557, waliopoteza maisha ni 22, wagonjwa 20 na sababu nyinginezo ikiwamo mmoja kufungwa jela ni 19.

“Jumla ya wanafunzi 75,495 walisajiliwa ila waliofanya mtihani ni 74, 877  sawa na asilimia 99.18  ambapo wasiofanya ni 618 sawa na asilimia 0.82,” alisema Lissu.

Alisema baadhi ya wanafunzi waliugua katika kipindi cha mitihani na baada ya kupewa huduma ya kwanza waliendelea na mitihani hiyo.

“Wapo baadhi yao ambao wameshindwa kufanya mitihani  kwa sababu ya ugonjwa ambao wataandaliwa  utaratibu wa kufanya mitihani hiyo ya kumaliza elimu ya msingi baadaye,” alisema Lissu.

Alisema wahitimu hao walitoka katika wilaya tano za mkoa huo, ambapo aliwapongeza wasimamizi  wote walio simamia mtihani huo kwa kutii sheria zilizopo na kuhakikisha mtihani unamalizika bila dosari yeyote.

Alisema matarajio katika mkoa wake ni kuongezeka kwa kiwango cha ufaulu  na kushika alama za juu zaidi kwa sababu ya maandalizi mazuri waliyoyapata.

Alisema mwaka  juzi na mwaka jana mkoa huo ulifanya vizuri ambapo wanafunzi walipata alama za juu na kusababisha mkoa huo kushika nafasi ya kwanza mfululizo.

“Matarajio yetu mwaka huu mkoa wetu unaweza kung’ara katika matokeo ya mtihani wa darasa la saba kwa sababu tulijipanga vyema na tuna imani tutashinda kwa kishindo,” alisema Lissu.

Wiki iliyopita, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ilitangaza jumla ya watahiniwa 947,221 waliotakiwa kufanya  mtihani wa kumaliza elimu ya msingi (PSLE).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles