24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

WANAFUNZI 2,600 WASHINDA RUFAA YA MIKOPO

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM


BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), imetangaza orodha yenye wanafunzi 2,679 ambao wamepata mikopo ya elimu ya juu yenye thamani ya Sh bilioni 9.6 baada ya kukamilika kwa uchambuzi wa rufaa walizowasilisha.

Taarifa iliyotolewa jana na kusainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru, ilieleza kuwa kati ya wanafunzi hao, 1,847 ni wa mwaka wa kwanza ambao mikopo yao ina thamani ya Sh bilioni 6.84 na wengine 832 ni wale wanaoendelea na masomo, lakini hawakuwa na mikopo katika miaka iliyopita.

Wanafunzi wanaoendelea na masomo wamepata mikopo yenye thamani ya Sh bilioni 2.76.

Orodha kamili ya wanafunzi waliofanikiwa kupata mikopo kupitia dirisha la rufaa pamoja na fedha za wanafunzi hao zimetumwa katika vyuo walipo hivi sasa.

“Hatua hii inafanya jumla ya wanafunzi 33,200 wa mwaka wa kwanza kuwa wamepangiwa mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 108 kwa mwaka wa masomo 2017/18 hadi sasa. Bajeti ya jumla kwa wanafunzi wote kwa mwaka 2017/2018 ni  Sh bilioni 427.54,” ilieleza taarifa hiyo.

Dirisha la rufaa lilifunguliwa kwa siku saba kuanzia Novemba 13  hadi 19, mwaka huu ili kuwapa fursa waombaji wote ambao hawakuwa wameridhika na upangaji wa mikopo na kuwasilisha rufaa kupitia vyuo walivyopata udahili.

 

MIKOPO YAHAMISHWA

Wakati huohuo, Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu imeanza kuhamisha mikopo iliyokuwa imeelekezwa katika vyuo tofauti na waliko kwa sasa.

Mikopo ya wanafunzi 590 wa mwaka wa kwanza yenye thamani ya Sh bilioni 1.78 ambayo awali ilikuwa imepelekwa katika vyuo tofauti na walipo wanafunzi, imehamishwa.

Wanafunzi hao waliohamishiwa mikopo yao, ni wale ambao walipangiwa mikopo na kupelekewa fedha zao katika vyuo ambavyo walipata udahili awali, ila baadaye wakaamua kujiunga na vyuo vingine ambavyo nako walipata udahili.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa orodha kamili ya wanafunzi hao na fedha zao zimetumwa katika vyuo walipo hivi sasa.

 

MIKOPO KWA WAHADHIRI

Mbali hilo, Badru alisema katika taarifa hiyo kuwa jumla ya wanafunzi 45 wa shahada za uzamili na uzamivu ambao ni wanataaluma na waajiriwa wa vyuo mbalimbali nchini, wamepata mikopo yenye thamani ya Sh milioni 441.4 katika mwaka wa masomo 2017/18.

Mikopo hiyo hutolewa na Bodi ya Mikopo kwa wanataaluma hao ili kuvijengea vyuo uwezo wa kitaaluma chini ya makubaliano kati ya Bodi ya Mikopo na vyuo hivyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles